Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
By Elias Msuya, Mwananchi emsuya@mwananchi.co.tz
Wanafunzi 10 wa
kike wa Shule ya Msingi Mandakerenge iliyopo zaidi ya kilomita 30 kutoka
Namanyere wilayani Nkasi Mkoa wa Rukwa wanaingia katika ofisi ya
mwalimu mkuu wakiwa wamembeba mwenzao aliyezimia.
Wanamuweka
chini na kuanza kumpepea ili azinduke. Mwalimu mkuu msaidizi, Yona
Nkwamba anatoa nafasi kwa wanafunzi hao kumuhudumia mwenzao.
Ni
kawaida kwa wanafunzi hao wa shule hiyo iliyopo katika Kisiwa cha
Mandakerenge kuhudumiana katika masuala yanayohusu jinsi yao yakiwemo
hedhi kwa kuwa hakuna mwalimu wa kike ambaye angewahudumia kama ilivyo
kwa shule nyingine nchini.
Kukifikia kisiwa
hicho ni lazima uikate barabara ya vumbi kutoka Namanyere inayoelekea
pwani ya Ziwa Tanganyika ambako vipo visiwa vingine vyenye changamoto
lukuki kiasi cha kutishia baadhi ya watumishi wa umma kwenda kufanya
kazi.
Usafiri katika barabara hiyo inayopita kwenye mabonde na
milima kuelekea vijiji vya Katongolo na Kipili unapatikana mara moja
asubuhi na jioni.
Unapofika Kijiji cha Kipili ambako
kumechangamka, bado kuna safari ya kufika ziwani ambako kuna mitumbwi ya
kienyeji ya kukupeleka visiwani.
Japo kuna mtumbwi wenye injini
unaofanya safari kati ya visiwa vya Mvuna, Mandakerenge na mji wa
Kirando ambao hupita asubuhi na jioni, bado watu wengi hutumia mitumbwi
ya kupiga makasia jambo ambalo ni hatari kiusalama.
Mandakerenge
kimejaa miamba na mawe mengi na hakina barabara, hivyo kukifanya
kisifikike kwa urahisi kutokana na kukosa miundombinu ya kuwezesha
kupita magari, pikipiki wala baiskeli. Njia rahisi ya kuvifikia
vitongoji vya kijiji cha kisiwa hicho ni kutembea kwa miguu au kutumia
mitumbwi kwa kuzunguka ziwani.
Mazingira hayo ndiyo yamesababisha
Shule ya Msingi ya Mandakerenge kukosa kabisa walimu wa kike kwa karibu
miaka 30 sasa na kuwafanya watoto wa kike wakose huduma muhimu ambazo
zingetolewa na watumishi wa kike hususan wanapokuwa katika hedhi.
Sababu
kubwa inayotajwa kuifanya shule hiyo, iliyojengwa na wakoloni wa
Kijerumani miaka ya 1800, ikose walimu wa kike ni kadhia za mazingira ya
kazi zinazochochewa na ugumu wa kufikika kutoka makao makuu ya Wilaya
ya Nkasi, Namanyare.
Malalamiko ya wanafunzi
Esther John
anayesoma darasa la saba katika shule hiyo anasema wangetamani kupata
walimu wa kike ili wawaeleze shida zao zinapowakuta lakini inashindikana
kwa sababu walimu wote ni wanaume.
“Wakati mwingine tunakuwa na
shida zinazotuhusu wasichana kama kuwa na hedhi lakini hatuwezi
kuwaeleza walimu wa kiume. Tunapenda hata kuelimishwa mambo ya wanawake,
lakini hatuna mtuwa kutufundisha. Wenzetu wavulana wanafaidika zaidi,”
anasema Esther.
Wengine ambao hawawezi kujisitiri wenyewe wakiwa
shule kama Mwajuma Hamza hulazimika kurudi nyumbani huku wakiacha masomo
yakiendelea.
Mwajuma anayesoma darasa la sita anasema wanapokuwa
na shida za hedhi kama imewatokea wakiwa nyumbani huairisha shule ili
wasaidiwe makwao na mama au walezi wao wa kike.
“Tunapopata shida
kama hedhi, tunaaga na kurudi nyumbani, walimu wanatuelewa kwa sababu
hakuna mwalimu wa kike hapa. Tungepetamani kupata walimu wa kike ili
watusaidie zaidi tukiwa shule,” anasema Mwajuma.
Wazazi wakabiliana na hali
Elizabeth
Mnazi, mzazi ambaye mtoto wa kike anasoma shule hiyo, anasema wanajua
changamoto hiyo ya uhaba wa walimu wa kike ndiyo maana huwa karibu na
watoto wao kuwasaidia.
“Ni kweli shule haina walimu wa kike,
lakini ikitokea shida watoto wanarudi nyumbani haraka. Ikiwa kuna
ulazima wa kwenda shule tunakwenda kuwachukua. Tumeshaueleza uongozi wa
kijiji, lakini tumeambiwa ni mpaka Serikali iajiri walimu,” anasema
Elizabeth.
Mwalimu mkuu msaidizi, Nkwamba anasema mazingira
magumu ni sehemu ya kazi na ikitokea shida kwa wasichana huwa
wanawaruhusu waende nyumbani haraka.
Anasema tatizo kubwa linalowakabili kiasi cha kuchangia walimu wanawake kukimbia ni ukosefu wa nyumba bora za kuishi.
“Kuna jumba moja tumepanga halina madirisha wala milango ndiyo tunaishi humo kwa kutenganishwa na mapazia,” anasema Nkwamba.
Kuhusu
vifaa, Nkwamba anasema awali hakukuwa na madawati ya kutosha, lakini
kwa kampeni iliyofanywa na Rais John Magufuli wamepata madawati mengi
japo bado kuna uhaba wa madawati 53.
“Inabidi darasa la kwanza
wasome kwa zamu ili madawati yatoshe. Vitabu hasa vya sayansi havipo
kabisa licha ya Serikali kubadilisha mtaala, inabidi tufundishe kwa
uzoefu tu,” anasema.
Shule hiyo inakosa walimu wa kike licha ya
takwimu za msingi za elimu za mwaka 2016 (BEST 2012-2016) zilizotolewa
na Ofisi ya Rais-Tamisemi hadi mwaka jana kubainisha kuwa shule za
awali, msingi na sekondari nchini zilikuwa na walimu wa kike wengi
zaidi wapatao 106,085 ikilinganishwa na walimu wa kiume 100,744.
Diwani
wa Kata ya Kipili, Wilbrod Chakukila aliyekuwa mwalimu mkuu wa shule
hiyo tangu mwaka 1993 anasema Serikali imeshindwa kupeleka walimu wa
kike kisiwani humo akitaja ushirikina kuwa moja ya sababu mbali na
mazingira magumu.
“Nimezaliwa katika kisiwa hiki na nimekuwa
mwalimu wa shule hii kwa zaidi ya miaka 20 hadi nilipostaafu. Mwaka 1993
walimu wote zaidi ya 10 waliokuwa wakifundisha shule hii waliacha kazi
wakidai kuwa wanarogwa. Shule ikabaki bila walimu,” anasimulia Mwalimu
Chakukila.
“Ilibidi Serikali itafute walimu ambao ni wazawa wa
maeneo haya. Mimi nilikuwa nafundisha huko Sumbawanga, nikaitikia wito
wa kurudi nyumbani na baadhi ya walimu, lakini walimu wa kike walikataa.
Tangu wakati huo nikawa mwalimu mkuu hapa.”
Anasema kutokana na
kukosekana walimu wa kike, kumekuwa na changamoto za kuwasaidia
wanafunzi wa kike hasa wa madarasa ya juu waliovunja ungo wanapopata
hedhi.
“Kuna changamoto kubwa wanapoingia mwezini, inabidi tu
utumie wanafunzi wenzao kuwasaidia na kuwarudisha nyumbani. Walimu wa
kike wangeweza kuwasaidia na kuwatia moyo, lakini ndiyo hawapo,” anasema
na kuongeza:
“Ilinitokea mara kadhaa nikiwa mwalimu shuleni
hapo. Kuna wakati nikiwa nafundisha mtoto wa kike aliugua ghafla, kwa
kuona aibu ikabidi niwatoe nje wavulana wote nikawaambie wakanisubiri
ofisini kwangu, wakati huo wanafunzi wa kike walimsafisha na kumpeleka
kwao mwanafunzi huyo wa kike.”
Mbali na walimu wa kike, Chakukila
anasema kwa ujumla mazingira ya kisiwa hicho ni magumu kuzoeleka kwa
wageni na hivyo kuchangia walimu wengi kushindwa kufanya kazi.
“Walimu
wanapenda mazingira yenye motisha ili kuongezea kwenye mshahara ulio
mdogo. Sasa umlete mwalimu hapa, kisiwa chote ni mawe matupu, hakuna
barabara hivyo hakuna gari wala pikipiki. Mwalimu hata akija hapa atakaa
mwaka mmoja kisha anaondoka kwa visingizio vingi,” anasema.
“Walimu wa kiume wanaishi hapa kwa ugumu tu, kwa ujumla Serikali imeshindwa kuleta walimu wa kike huku.
Ofisa
Mtendaji wa kijiji hicho, Clarence Msemakweli anasema shule hiyo ina
wanafunzi 622 ambapo kati yao wasichana ni 308 na wavulana ni 414 ina
walimu saba wa kiume na upungufu wa walimu sita.
Tatizo la uhaba
wa walimu wa kike linaathiri wilaya baada ya takwimu kutoka katika
halmashauri hiyo kuonyesha kuwa kati ya walimu 171 walioajiriwa na
kuripoti mwaka 2015 ni walimu 39 ndiyo walikuwa wanawake.
Hii ina maana kuwa kwa kila walimu 10 walioripoti, ni watatu tu walikuwa wanawake.
Wilaya
hiyo ina upungufu wa walimu wa shule za msingi kwa asilimia 38 baada ya
kuwepo walimu 1,084 kati ya 1,696 wanaojihitajika.
Wadau wa afya
na watetezi za haki za wasichana wanasema kuwa ukosefu wa ushauri wa
masuala ya maumbile kwa watoto wa kike una athari katika makuzi na afya
zao.
Ofisa wa Sera na Utetezi wa Mtandao wa usafi wa mazingira na
maji (Tawasanet), Darius Mhawi anasema kuna tatizo kubwa la afya ya
wasichana wanaopevuka kwa kukosa huduma na ushauri wa kujitunza.
“Sisi
ni wadau na role (jukumu) yetu ni kufanya utafiti na kuishauri Serikali
kuhusu usafi wa mazingira. Tulifanya utafiti katika wilaya za Temeke
kwa maeneo ya mijini na Kilomero kwa maeneo ya vijijini. Nadhani tatizo
la Nkasi litakuwa linafanana na changamoto tulizoziona vijijini,”
anasema.
“Tumeishauri Serikali kuongeza usimamizi na utoaji wa
pedi za kike kwa wanafunzi, kuboresha vyoo vya wanafunzi, kuweka huduma
ya maji na matibabu kwa sababu wengine wakiwa kwenye hedhi wanapata
maumivu. Vilevile tumewahusisha wabunge akiwemo Sophia Mwakagenda ambaye
ni mhamasishaji wetu kinara,” anaongeza Mhawi.
Mkurugenzi wa
Halmashauri ya wilaya ya Nkasi, Julius Kaondo anasema tatizo la walimu
wa kike siyo kwa shule hiyo pekee, bali ni kwa wilaya nzima na wanafanya
mikakati ya kuongeza walimu.
“Siyo kweli kwamba walimu hawataki
kwenda vijijini, ila wilaya ya Nkasi yote ina uhaba mkubwa wa walimu
hasa wa kike. Nimetoka mkoani Dodoma hivi karibuni ambako tumejadili
tatizo hilo na Serikali imeahidi kutuongeza walimu wakiwemo wa kike,”
anasema Kaondo.
0 comments:
Post a Comment