SERIKALI YAANZA KUTUMIA MFUMO WA NYOTA KATIKA KUVIPIMA VITUO VYA AFYA NA HOSPITALI NCHINI.

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
 Naibu Waziri wa Afya, maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt. Faustine Ndugulile (MB) akikagua Bin Kadi ambayo inaonesha idadi ya Dawa zilizoingia na zilizobaki katika stoo ya dawa ya Kituo cha Afya Nkomolo Mkoani Rukwa.
 Naibu Waziri wa Afya, maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt. Faustine Ndugulile (MB) akikagua jokofu la Chanjo wakati alipotembelea katika Kituo cha Afya cha Nkomolo kilichopo Nkasi Mkoani Rukwa wakati wa Ziara yake ya kukagua Huduma za Afya Mkoani Rukwa.
 Naibu Waziri wa Afya, maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt. Faustine Ndugulile (MB) akikagua Idadi ya watu waliohudhuria Kituoni hapo kupitia mfumo wa Kompyuta katika stoo ya dawa ya Kituo cha Afya Nkomolo Mkoani Rukwa.

Naibu Waziri wa Afya, maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt. Faustine Ndugulile (MB) akipokea maelezo kutoka kwa Mtaalamu wa Majengo Mhandisi Mwakyembe kutoka Ofisi ya Mkoa wa Rukwa.

 Naibu Waziri wa Afya, maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt. Faustine Ndugulile (mwenye tisheti ya mistari) akipokea maelekezo ya ramani ya jingo jipya la Mama na Mtoto katika kituo cha Afya Nkomolo, anaemfuatia ni Mganga Mkuu wa Mkoa Dkt. Boniface Kasululu na wa mwisho ni Mhandisi Mwakyembe.
Naibu Waziri wa Afya, maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt. Faustine Ndugulile akiendelea na ziara yake katika kituo cha Afya Nkomolo, anaemfuata ni Mhandisi Mwakyembe na Mbunge wa Nkasi kaskazini Mh.Kessy Ally.Na WAMJWW. RUKWA-NKASI

Serikali yaanza kutumia mfumo wa nyota kupima huduma zitolewazo na Vituo vya Afya, Hospitali na Zahanati nchini ili kupima utendaji kazi wa watumishi wa Sekta ya Afya katika kutoa huduma kwa wananchi.

Hayo yamesemwa na Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt. Faustine Ndugulile alipotembelea Kituo cha Afya cha Nkomolo Wilaya ya Nkasi Mkoani Rukwa, ikiwa ni muendelezo wa Ziara yake ya kukagua shughuli za utoaji wa huduma za Afya na kuamsha hali kwa wananchi katika kujihusisha na shughuli za maendeleo katika maeneo yao.

“Tumeanza utaratibu wa kutoa nyota katika vituo vya Afya, imeanzia nyota sifuri mpaka nyota tano, sifuri maana yake kituo hicho hakifai kutoa huduma ya Afya na nyota tano maana yake kinafanya vizuri sana” Alisema Dkt. Ndugulile.

Kwa upande mwingine Dkt. Ndugulile aliridhishwa na hali ya upatikanaji wa Dawa katika kituo hicho, hivyo kuwatoa hofu wananchi na kusisitiza kuwa hawapaswi kuuziwa dawa zote muhimu kwani Serikali imeboresha hali ya upatikanaji wa Dawa katika vituo vyote vya Afya nchini.

“Dawa zote za msingi tunazo zakutosha, hivyo hatutarajii kuona mtu aje hapa kutibiwa kisha aambiwe akanunue katika vituo binafsi, Hali ya upatikanaji wa Dawa ni nzuri katika kituo hiki na ni asilimia 85 ” aliendelea Dkt. Ndugulile.

Aidha, Mbunge wa Jimbo la Nkasi Kaskazini Mh. Ally Kessy aliupongeza uongozi wa Mkoa kwa kusimia vizuri ujenzi wa kituo hicho, uliojumuisha Thieta, Wodi ya mama na mtoto mochwari na maabara mpaka hatua ya kupaua kwa jumla ya kiasi cha shilingi Bilioni 290 kwa kutumia nguvu kubwa ya wananchi (fixed akaunti).

Akiwasilisha taarifa ya Mkoa, Mganga Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Dkt Boniface Kasululu amesema kuwa Mkoa wa Rukwa umeendelea kuboresha huduma za Afya ya mama na mtoto katika maeneo ya vijijini kama juhudi za kupunguza tatizo la vifo vya wanawake na watoto wachanga vitokanavyo na matatizo ya uzazi.

Dkt. Boniface aliendelea kusema kwamba, Zaidi ya vituo 214 kati ya 223 vilivyopo, vinatoa huduma muhimu za mzazi na mtoto jambo linalosaidia kwa kiasi kikubwa kupunguza vifo vya kina mama wajawazito na watoto wachanga licha ya upungufu mkubwa wa vituo hivyo.

Kwa upande mwingine Dkt. Boniface Kasululu alisema kwamba Mkoa unaendelea kuelimisha jamii kuhusu umuhimu wa kuwapeleka watoto katika vituo vinavyotoa huduma za chanjo, Hadi kufikia Mwezi Novembe 2017 jumla ya Watoto 48,494 wenye umri wa chini ya mwaka mmoja walipewa chanjo, kati ya watoto 50,245 waliotarajiwa ambao ni sawa na asilimia 96 jambo lililoufanya mkoa kuvuka lengo la kitaifa la asilimia 90.

MVUA KUBWA YASABABISHA WATU KUKIMBIA JENEZA

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399. 
 
 
Na   Walter  Mguluchuma
Nkasi
HALI ya Taharuki na hofu imezuka katika kijiji cha Katani kata ya Nkandasi wilayani Nkasi mkoani Rukwa na kupelekea waombolezaji kutimua mbio na kuacha jeneza lenye mwili wa marehemu baada ya mvua kubwa kuanzakunyesha na kubomoa nyumba za wakazi wa kijiji hicho.

Tukio hilo lilitokea Juzi majira ya saa 6 mchana mara baada ya kuanza kunyesha mvua kubwa zilizoambatana na radi na upepo mkali ulioezua baadhi ya nyumba za wanachi hao ambao walikuwa wakiomboleza msiba wa mwananchi mwenzao aliyefaniki baada ya kuugua siku chache zilizopita. 

Akizungumza na gazeti hili mwenyekiti wa serikali ya kitongoji cha Kaungo, Robert Kanoni alisema kuwa wakiwa wanaelekea kufanya maziko ya marehemu Dismas Kanoni aliyefari Jana, ghafla ilianza kunyesha mvua kubwa ikiambatana na radi na upepo mkali hali iliyosababisha baadhi ya waombolezaji kutimua mbio na kurejea majumbani kutokana na hofu iliyoibuka kufuatia tukio hilo.

Baadhi ya wananchi walivumilia nakurejea na jeneza lililokuwa na mwili wa marehemu nyumbani na kuahilisha maziko kwamuda ili kupisha hali hiyo uweze kutulia na walikwenda kuzika baadaye katika makaburi yaliyopo kijijini hapo. 

Alisema kuwa tukio hilo limezua hisia za kishirikina  kwa wananchi wa kijiji hicho kwani miezi miwili iliyopita baba yake na marehemu huyo alifariki baada ya kugongwa na gari la kampuni ya ujenzi wa barabara na walipofanya maziko siku iliyofuata walikuta ngozi ya kondoo juu ya kaburi la marehemu kitendo kilicho washangaza wakazi hao.

Kanoni alisema kuwa kutokana na mvua hiyo nyumba zipatazo 10 zimebomoka kabisa na zinatakiwa kujengwa upya huku nyumba nyingine Saba,  zikiwa zimeezuliwa paa na kuwaacha wakazi wake wakiwa hawana sehemu ya kukaa licha ya kuwa wamepata hifadhi na misaada ya kibinaadamu kwa wenzao.  

Naye Peter Kalale mkazi wa kijiji hicho akizungumzia tukio hilo  alisema kuwa mara kwa mara kijiji hicho kimekuwa kikikumbwa na dhoruba pindi mvua zinaponyesha kwakua kimepitiwa na mkondo wa upepo mkali ambao unasababisha hali hiyo. 

Alisema changamoto iliyopo ni tabia ya wananchi kukata miti kwaajili ya mashamba  na hivyo kusababisha pepo zinapovuma hazikuti kizuizi chochote na hivyo imekuwa sababu ya kuezuliwa nyumba zao na hata kubomoka kabisa. 

Kwaupande wake mwenyekiti wa kamati ya maafa ya wilaya hiyo ambaye ni mkuu wa wilaya  hiyo Said Mtanda ilikiri kutokea kwa tukio hilo na kutoa wito kwa wananchi kujenga makazi bora kwani miongoni mwa nyumba  hizo zipo ambazo zimeezekwa kwa nyasi.

Alisema kuwa sera ya serikali ya awamu ya tano ni  kuwahimiza wananchi wajenge nyumba bora na zakisasa ili waweze kuepuka majanga yanayotokana na tabia nchi kwani bila kufanya hivyo wananchi wataendelea kupata hasara.


KATEKISTA AFARIKI BAADA YA KUENDESHA IBADA YA MAZISHI

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399. 
 Imeandikwa na Peti Siyame, Tanganyika
MWALIMU wa dini wa Kanisa Katoliki Jimbo la Mpanda, Noel Sitemele amefariki dunia muda mfupi baada ya kumaliza kuongoza ibada ya mazishi ya muumini wake yaliyofanyika katika makaburi ya Mchakamchaka Kijiji cha Majalila wilayani Tanganyika mkoani Katavi.
Katekista huyo alikuwa akitoa huduma ya kiroho katika Kigango cha Mchakamchaka kilichopo katika Parokia ya Mpanda Ndogo katika Wilaya ya Tanganyika mkoani Katavi. Akizungumzia mkasa huyo, Diwani wa Kata ya Mpanda Ndogo, Hamad Mapengo alisema licha ya Sitemele kuwa mwalimu wa dini, katika uhai wake alikuwa pia Mwenyekiti wa Kijiji cha Majalila kilichopo katika Halmashauri ya Mpanda wilayani Tanganyika.
Mapengo ambaye pia ni Mwenyekiti wa Halmashauri ya Mpanda, alisema Katekista alifariki dunia juzi saa 11 jioni muda mfupi baada ya kufikishwa zahati ya kijijini Majalila kutibiwa.Alisema kabla ya kukutwa na umauti, Katekista huyo alikuwa mwenye siha njema na aliongoza ibada ya mazishi ya muumini wake hadi mwisho katika makaburi ya Kigango cha Mchakamchaka kilichopo katika Kijiji cha Majalila ambapo alianza kujisikia vibaya.
“Baada ya kumaliza ibada hiyo ya mazishi, alianza kujisikia vibaya hivyo akalazimika kurejea nyumbani kwake na kuwaacha waombolezaji makaburini,” alieleza Mpaengo. Alisema, baada kufika nyumbani kwake, hali yake iliendelea kuwa mbaya na aliomba msaada kutoka kwa majirani zake wamkimbize kwenye kituo cha afya kwa matibabu.
Inaelezwa zahanati hiyo haiko mbali kutoka alikokuwa akiishi mwalimu huyo wa dini. Mwenyekiti alisema, taarifa za kifo cha Katekista huyo zilizagaa haraka kijijini humo na kuwafikia waombolezaji waliokuwa nyumbani kwa marehemu aliyeongozewa ibada ya mazishi na Katekista huyo waliopata simanzi kubwa wengine wakiwa hawaamini jambo hilo.
Maziko yake yalifanyika jana makaburi ya kigango cha Mchakamchaka Kijiji cha Majalila. Padri Paschal Kipenye wa Parokia ya Mpanda Ndogo aliongoza ibada ya mazishi yaliyohudhuriwa na mamia ya waombolezaji akiwemo Mbunge wa Mpanda Vijijini, Selemani Kakoso.
CHANZO HABARI LEO 

RC WANGABO AZIHIMIZA HALMASHAURI KUONGEZA MASHINE ZA MAPATO KUONGEZA UKUSANYAJI

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399. 

 Mkuu wa Wilaya ya Sumbawanga Dk. Khalfan Haule akitoa maelezo ya kumtambulisha Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Mh. Joachim Wangabo kwa wananchi wa kijiji cha Zimba kata ya Mtowisa, Wilayani Sumbawanga. wakati walipofika kwenye kijiji hicho kuona kiwanda cha kukamulia alizeti. 
 Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Mh. Joachim Wangabo (wa tatu kutoka kulia) akiuliza swali kwa mhandisi wa maji wa Wilaya Patrick Ndimbo (wa kwanza kushoto) wakati walipotembelea mradi wa maji wa kutumia umeme wa jua mji mdogo Laela Wilayani Sumbawanga wenye thamani ya Shilingi Bilioni 1.8. 
 Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Mh. Joachim Wangabo akishiriki kutumia ala ya kigoda kuchekecha juu ya mtungi na kuzalisha sauti inayowezesha kuleta mlio kwaajili ya kunogesha nyimbo, Ni ala ya asili inayotumiaka katika ngoma za kitamaduni za Kifipa muda mfupi kabla ya kufanya mkutano na wananchi wa mji mdogo wa Laela. 
 Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Mh. Joachim Wangabo akimsalimia mmoja wa kinamama wa kikundi cha ngoma Laela Odila Maufi wakati alipokuwa akiingia katika viwanja vya shule ya Msingi Laela kwaajili ya Mkutano wa hadhara kujitambulisha kwa wananchi na kuongea nao.  


Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Mh. Joachim Wangabo amewasifu wananchi wa kata ya Mtowisa, Tarafa ya Mtowisa, Wilayani Sumbawanga kwa kuonyesha mshikamano katika ujenzi wa shule ya Sekondari Vuma pamoja na ujenzi unaonendelea wa kituo cha polisi kitakachohudumia tarafa ya mtowisa.

Tarafa hiyo yenye kata 4 ina shule moja ya kidato cha tano na sita jambo alilosifu Mh. Wangabo kuwa imetimiza ilani cha Chama Tawala kwa kuwa na Shule moja ya aina hiyo kwa kila tarafa.

Amesema kuwa ataendelea kusisitiza kauli ya serikali ya awamu ya tano ya kuwa maendeleo hayana vyama, hivyo alisisitiza wananchi hao kutobaguana kwa itikadi zao bali wahimizane katika kutatua changamoto na kuleta maendeleo katika tarafa yao.

“Mmenivuti mliponieleza kwamba mnashirikiana katika nyanja mbalimbali, kuna majengo yale ya shule mnashirikiana na jengo hili la polisi mnashirikiana ili kuhakikisha kwamba changamoto mbalimbali zilizopo ndani yenu mnazitatua, hili limenifurahisha na ningependa muendelee nalo, na umeoja na mshikamano uliopo muudumishe bila ya kujali vyama vyenu.” Alisifu.

Ameyasema hayo katika Mkutano wa hadhara katika Kijiji cha mtowisa, kata ya mtowisa Wilayani Sumbawanga katika ziara yake ya siku mbili katika Halmashauri ya Wilaya ya Sumbawanga yenye lengo la kutembelea miradi mbalimbali na kujitambulisha kwa wananchi.

Kwa upande wake diwani wa Kata ya mtowisa Mh. Edgar Malini alisema kuwa wananchi wa mtowisa hawana tabu wa kutoa ushirikiano ili kujiletea maendeleo wenyewe isipokuwa wamekuwa na kilio cha muda mrefu kuhusu umeme na maji.

RC WANGABO AMUAGIZA RPC AWAPUMZISHE DTO NA MSAIDIZI WA RTO KUPISHA UCHUNGUZI

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Mh. Joachim Wangabo akizungumza na madereva wa Bodaboda na Bajaji wa Manispaa ya Sumbawanga katika uwanja wa Nelson Mandela.
Baadhi ya Bajaji zikiwa zimepaki katika uwanja ulipofanyikia Mkutano wa madereva wa Bajaji na Bodaboda na Mkuu wa Mkoa.
Kamanda wa polisi Mkoa wa Rukwa ACP George Kyando akitoa elimu ya usalama barabarani na kujibu baadhi ya kero zilizotolewa na madereva wa Bodaboda na bajaji wa Manispaa ya Sumbawanga.
Baadhi ya bodaboda zikiwa zimepaki uwanja wa Nelson Mandela Mjini Sumbawanga.


Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Mh. Joachim Wangabo amemuagiza Kamanda wa Polisi Mkoa wa Rukwa George Kyando kuwaweka pembeni Mkuu wa Usalama barabarani wa Wilaya Inspector Suleiman Africanus pamoja na Msaidizi wa Mkuu wa Usalama barabarani Mkoa Inspector Michael Mwakasungula ili kupisha uchunguzi kufuatia tuhuma kadhaa zilizoelekezwa dhidi yao.


Agizo hilo amelitoa wakati akijibu kero za madereva wa bajaji na bodaboda wapatao 4352 kwa mkoa mzima waliowakilishwa na wenzao wa mjini Sumbawanga baada ya kukutana nao na kusikiliza vilio vyao katika Mkutano uliofanyika katika Viwanja vya Nelson Mandela mjini Sumbawanga.
Madereva 13 walipata nafasi ya kumuelezea Mh. Wangabo kero wanazopata wakiwa barabarani huku miongoni mwa kero hizo ambazo ni pamoja na kupokea rushwa, uonevu usio wa lazima barabarani na kuwaweka mahabusu kwa visingizio mbalimbali zilielekezwa kwa maafisa hao wa usalama barabarani.
“Hawa wawili hawa na tuhuma mlizozitoa huenda zina ukweli, RPC nakuagiza nenda kazichunguze hizi tuhuma zote zilizotolewa hapa kwa kina na nyinyi muwe mashahidi kwenda polisi kutoa shuhuda zenu, halafu uchukue hatua stahiki, lakini wakati huo huo unapozichunguza hizi tuhuma wao uwaweke pembeni, uwape kazi nyingine,”


Amesema kuwa hakuna mtendaji wa serikali ambaye amepangiwa sehemu akae milele na milele na kuwa mtumishi asijidanyanye kwamba bila ya yeye kazi za serikali haziwezi kwenda huku akijitolea mfano kuwa yeye ni Mkuu wa Mkoa wa 15 tangu kuanzishwa kwa Mkoa huu mwaka 1974, wote walionitangulia wamepiga kazi wameondoka nae ataondoka.


Aidha, Mh. Wangabo amewasisitiza madereva hao kusomea sheria za barabarani na kupata leseni ilikupunguza ajali za barabarani katika Mkoa wa Rukwa huku akiwapongeza kwa takwimu zinzoonyesha kupungua kwa ajali hizi ukilinganisha na mwaka 2016.


Katika kulisisitiza hilo Mh. Wangabo alimualika mwalimu wa mafunzo ya usalama barabarani ili kutoa mafunzo hayo ya siku 3 bure kwa madereva hao kwa lengo la kutokuwa na ajali katika Mkoa wa Rukwa.huku akimpa miezi 7 kamanda wa polisi mkoa kuhakikisha bodaboda wote 4352 wanakuwa na leseni na vitambulisho.


Kwa upande wake kamanda wa polisi Mkoa ACP George Kyando ameeleza kuwa kwa ajali za bajaji na bodaboda mwaka 2016 kulikuwa na ajali 18 huku 11 zikisababisha vifo vya watu 20 wakati mwaka 2017 kuemtokea ajali 9 huku 5 zikisababisha vifo vya watu 7.


Yona Mwangoka ni mmoja wa madereva wa bodaboda aliyedai kuwa na ushahidi wa video unaoonyesha ukusanyaji wa shilingi 40,000 kuwapa polisi ili kuachiwa kwa makosa mbalimbali huku risiti zao zikionesha shilingi 30,000, fedha ambazo zilikusanywa na kiongozi wa boda boda baada ya boda boda hao kukamatwa kwa kosa la kumpiga askari wa usalama barabarani tukio lililotokea siku mbili kabla ya Mkutano huo.

AHUKUMIWA KIFUNGO CHA MAISHA KWA KUBAKA MWANAFUNZI

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399. 
 Imeandikwa na Pety Siyame, Mpanda
MAHAKAMA ya Wilaya ya Mpanda mkoani Katavi imemhukumu mkazi wa Kijiji cha Sibwesa katika Wilaya ya Tanganyika, Peter Ngomalala (50) kifungo cha maisha baada ya kutiwa hatiani kwa kosa la kumbaka mtoto wa kike mwenye umri wa miaka tisa, mwanafunzi wa darasa la pili katika shule ya msingi wilayani Tanganyika huku mtoto mwenzake wa kike mwenye umri wa miaka saba akishuhudia.
Hakimu Mkazi Mfawidhi wa mahakama hiyo, Chiganga Ntengwa alisoma hukumu hiyo jana alisema ameridhishwa na ushahidi wa upande wa mashtaka bila kuacha shaka kuwa mshtakiwa alitenda kosa hilo.
Upande wa Mashtaka ukiongozwa na Wakili wa Serikali, Flavian Shiyo uliwaita mashahidi kadhaa akiwemo mtoto huyo aliyebakwa na pia mama yake mzazi. Hakimu alisema mshitakiwa alitenda kosa hilo kinyume cha kifungu cha Sheria namba 130 (1)(2) na kifungu cha Sheria 131 (3) kanuni ya adhabu.
Alisema mtoto mwingine aliyeshuhudia na aliyebakwa wote pamoja na kuwa na umri mdogo, bado walitoa ushahidi kwa ufasaha ambao haukuacha shaka yoyote kuwa mshtakiwa alitenda kosa hilo.
Hakimu alisema mahakama hiyo ilijiridhisha na ushahidi wa muuguzi wa zahanati ya Sibwesa mtoto huyo alikofanyiwa uchunguzi wa kitabibu na kupewa dawa za kufubaza makali ya Virusi vya Ukimwi (ARVs).
Awali Mwendesha Mashtaka, Wakili wa Serikali, Shiyo alidai mshtakiwa alitenda kosa hilo Oktoba 12, 2016 saa 4 asubuhi kijijini Sibwesa ambapo alimkuta mtoto huyo akicheza na mwenzake jirani na kwao akawalaghai watoto hao wamfuate nyumbani kwake akawape fedha wanunue biskuti na vinywaji baridi.
Wakili Shiyo alidai kabla hajafika nyumbani kwake alimvuta mtoto huyo kwa nguvu na kumpeleka eneo la tangi la maji na kumbaka huku mwenzake akishuhudia tukio hilo na licha ya watoto hao kupiga kelele za kuomba msaada hakumwachia.
Ilidaiwa watoto hao waliwataarifu wazazi wao ambako mshtakiwa alitiwa nguvuni na askari mgambo wa kijijini humo na kumfikisha katika kituo cha polisi. Mshitakiwa alijitetea akidai hakumfanyia mtoto huyo unyama huo, bali mama yake mzazi amemsingizia kwa kuwa alikuwa akimdai fedha alizomkopesha hivyo kuomba mahakama imwachie huru.
CHANZO HABARI LEO

RC RUKWA APIGA MARUFUKU MAHINDI KUTOKA ZAMBIA

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au W
Imeandikwa na Pety Siyame, Sumbawanga
Mkuu wa Mkoa wa Rukwa, Joachim Wangabo.
MKUU wa Mkoa wa Rukwa, Joachim Wangabo amewapiga marufuku wafanyabiashara wanaoingiza mahindi kwa magendo kutoka Zambia na kuyauza kwa bei ya kutupa akitaka waache mara moja.
Wangabo alisema mahindi hayo yanayoingizwa kwa magendo mkoani Rukwa kutoka Zambia ndiyo yamesababisha kurundikana kwa mahindi lakini pia kuendelea kuanguka kwa bei ya mahindi yaliyovunwa na wakulima mkoani humo katika msimu huu wa kilimo na hivyo kuathiri soko lao.
Alipiga marufuku hiyo akijibu kilio cha wazee mkoani humo waliomweleza mahindi yamerundikana katika kila nyumba ya wakulima na wameshindwa kununua pembejeo za kilimo katika msimu huu.
“Kila nyumba imefurika mahindi, hakuna pa kuyapeleka kwa sababu ya kutokuwepo kwa soko la uhakika na la ushindani .... Basi tumebakia kula asubuhi, mchana na jioni hata zaidi ya mara nne ....wasiwasi tutashindwa kununua pembejeo za kilimo kwani fedha hatuna kila mtu analia tu ...pia kuna hatari wakulima wakashindwa kulima msimu huu,” Mzee Joseph Ngua alimweleza RC huyo.CHANZO HABARI LEO
hatsapp namba +255765056399.

NG'OMBE WAPATAO 692 WAMEKUFA BAADA YA KUKOSA MATUNZO BORA.

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
NG’OMBE  wapatao  692 ambao  ni miongoni  1,332 walioshikiliwa na kuzuiliwa  katika Hifadhi ya Pori la Akiba la Rukwa – Lukwati  kwa zaidi  ya mwaka mmoja wamekufa kwa kukosa matunzo bora imefahamika
 .
Kufuatia hilo Waziri  wa Mifugo na Uvuvi ,Luhaga Mpina  ameagiza uongozi wa hifadhi hiyo kurejesha  mara moja  ng’ombe waliosalia wapatao 640 ambao ni mali ya wafujaji watatu kwa kuwa wanashiliwa kinyume cha sharia .
 
Waziri Mpina alitoa agizo hilo  wakati alipotembelea hifadhi hiyo iliyopo katika Bonde la Ziwa Rukwa wilayani Mlele  mkoa wa Katavi  kwa lengo la kutatua mgogoro wa muda mrefu baina ya wafugaji hao watatu na uongozi wa hifadhi hiyo .
 
Alisema kuwa ameshutushwa na taarifa iliyosomwa na Meneja wa Hifadhi hiyo , Paschal Mhina  ambapo alimweleza kuwa ng’ombe wapatao 1,332 waliovamia hifadhi walikamatwa  na kushikiliwa  kwa  mwaka mmoja na miezi tisa ambapo ng’ombe wapatao 692 wameshakufa  na waliobakia ni 640 .

 Aidha aliuagiza uongozi  wa Serikali ya mkoa wa Katavi kuhakikisha  inahakikia mifugo hiyo na kuwakabidhi wenye mali kwamba wale wote watakaobainika kusababisha  vifo vya ng’ombe hao waliokufa kwa uzembe wachukuliwe hatua kali za kinidhamu na kijinai . 
“ Hakukuwa na sababu yoyote  ile ya  msingi ya kuendelea  kuishilikia  mifugo hiyo baada ya  wenye mali hiyo kufungua   mashitaka  mahakamani  ambapo  katika kesi ya awali watuhumiwa watau ambao ndio mwenye mai hiyo  walifungua mashataka  katika  katika    Mahakama ya  Wilaya ya  Mpanda   ambapo  mahakama hiyo iliamuru  itaisishwe na  iwe  mali ya  Serikali” alieleza  .
Alimtaka   Meneja wa  pori la  Akiba  amwonyeshe  hati yoyote  inayowapa   mamlaka ya  kuendelea kuwashikili ngombe hao wakati  wafugaji   walikuwa  wanatuhumiwa  walikata rufaa   Mahakama Kuu Kanda ya Sumbawanga  kupiga  kutaifishiwa  ngombe zao .
Alisema isitoshe  Mahakama Kuu  ilitengua  hukumu iliyotolewa na  Mahama ya  Wilaya ya Mpanda na kuamuru  wafugaji hao watatu warejeshewe  mifugo yao  na faini ya Sh  500,000/- walizotozwa  .
Wafugaji hao watatu  ni pamoja na Shigela Mayunga , Charles Mtokambali na Kelenja Makuja .
 “Nimesikishwa  sana na  kitendo cha  uongozi wa hifadhi ya pori la akiba la Rukwa – Lukwati kwa kuendelea kuishikilia mifugo hiyo  ambapo idadi kubwa ya  mifugo hiyo imekufa kwa magonjwa  ….nataka  kujua  kwanini mifugo  waliendelea kushikiliwa  ndani ya hifadhi hiyo  likiwa ni eneo maalumu lililotengwa  kwa ajili ya wanyamapori  na sio ng’ombe “ alihoji   kwa hisia .
Kwa upande wake  Meneja wa  Pori la   Akiba  la  Rukwa   Rukwati   Mhina  alieleza  kuwa mifugo hiyo ilendelea  kushikiliwa  kwa  kile   alichodai  kuwa   baada  ya uongozi wa hifadhi hiyo kukata rufaa kupinga hukumu iliyotolewa  na   Mahakama  Kuu  Kanda ya Sumbawanga   Sumbawanga.
Aliongeza kuwa ungozi wa hifadhi hiyo ulipewa maelekezo  na Mwanasheria wa Serikali  kuwa waendelea kuitunza mifugo hiyo  kama sehemu ya kielelezo cha kesi hiyo ..
Kwa upande wake ,  Katibu  Mkuu  wa  Chama cha Wafugaji  Tanzania Makoye Nkonosinema alisema kuwa mifugo  iliyokufa  ikiwa mikononi mwa uongozi wa hifadhi hiyo  wataendelea  kuidai .
Aidha alitaka kupewa maelezo ya kina  katika kipindi hicho chote ambacho ng’ombe hao walikuwa wameshikiliwa  ni ndama  wangapi waliozaliwa .
Nae  Ofisa Utafiti wa  Magonjwa ya   Mifugo wa  Mikoa wa Katavi  na Rukwa , Protus Reshola alisema kuwa idadi hiyo ya ng’ombe iliyokufa ni kubwa sana kwamba  imesababishwa na dosari kadhaa  ikiwemo waliokuwa wakiwachunga walikuwa sio wafugaji .
Aliongeza kuwa kutopatiwa matibabu stahiki na kutokuwepo na josho kwenye hifadhi hiyo  kumesababisha ng’ombe hao  kufa kutokana na ugonjwa wa homa ya mapafu .
Habari imeandikwa na Walter Nguruchuma wa Rukwa yetu Blog

“HAKUNA MWANDISHI WA HABARI ATAKAYEFUNGWA WALA KUZUIWA KUFANYA KAZI YAKE,” RC WANGABO

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Mh. Joachim Wangabo akitoa nasaha kwa wazee wa Mkoa wa Rukwa na waandishi wa habari (hawapo pichani) alipokwa akizungumza na wazee hao.

Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Mh. Joachim Wangabo amewatahadharisha wakuu wa Wilaya na wapenda maendeleo wote Mkoani Rukwa wasiwanyanyase waandishi wa habari pindi wanapohitaji habari za kutangaza fursa zilizomo katika Mkoa.

Ameonya kuwa kuna baadhi ya viongozi wamekuwa wazito kutoa ushirikiano kwa waandishi wa habari jambo linalopelekea wadau wa maendeleo walio nje ya Mkoa kutofahamu fursa zilizomo katika mkoa na changamoto zinazopatikana ili watoe ushirikiano katika kuzitatua changamoto hizo.

“Kwa Mkoa huu wa Rukwa waandishi wa habari Ruksa kufanya kazi yenu vizuri, Vyombo vya habari ni fursa, wao ndio watakaoiambia dunia kuwa Rukwa iko hivi, hakuna mwandishi atakayewekwa ndani katika mkoa huu, wao ni wadau muhimu sana katika maendeleo na sio watu wa kuwaweka pembeni katika kufikisha ujumbe kwa jamii,” alisisitiza


Ameyatamka hayo wakati wa kikao chake na wazee wa Mkoa wa Rukwa pamoja na baadhi ya viongozi wa dini kilichowaalika waandishi wa habari ili kuijua mipango na mikakati yake katika kuonafursa za  Rukwa zinatangazwa kitaifa na kimataifa.

Lakini pia hakusita kuwatahadharisha waandishi hao kuwa anayekwenda kinyume na miiko ya uandishi na kugeuza misingi ya kazi yake, hatokuwa na nafasi ya kufanya kazi katika Mkoa na kuongeza kuwa mwandishi wa habari hapaswi kuwa wakala wa vyama vya kisisasa na kuacha kuandika mazuri yanayotendwa na serikali ya awamu ya tano.

RC Rukwa awaasa watumishi kutotumia vyeo kuwanyanyasa wananchi

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
Mkuu wa Mkoa wa Rukwa, Mh. Joachim Wangabo akifafanua namna mtumishi anavyotakiwa kuwajibika pindi anapowahudumia wananchi  (aliyekaa) kaimu Katibu Tawala Mkoa wa Rukwa David Kilonzo. 
 Viongozi wa mashirika ya ya umma na mamlaka mbalimbali za seikali Mkoani Rukwa Waliohudhuria kwenye kikao hicho kilichowakutanisha wakuu wa mamlaka na mashirika ya umma. 
Mkuu wa Mkoa wa Rukwa, Mh. Joachim Wangabo amewaasa watumishi wa mashirika ya umma na wakala wa serikali mkoani Rukwa kutotumia vyeo vyao kuwanyanyasa wananchi wanaowahudumia na badala yake wawasaidie kwa kuzingatia misingi ya haki na usawa bila ya kujali, rangi kabila, dini na hali zao kiuchumi.

Amesema kuwa watumishi wa serikali ni watumishi wa wananchi hivyo wanapaswa kujituma bila ya kujali vyeo vyao kwani vyeo hivyo havitakuwa na maana ikiwa wananchi hawapati huduma wanayoitarajia kutoka katika serikali waliyoiweka madarakani.

“Sisi viongozi wa Serikali lazima tufanye kazi kwa kujituma na kujitoa na tukumbuke kuwa sisi ni watumishi tu, sio watu wa kujivuna ama wabinafsi na kujinadi kwa vyeo vyetu kwamba mimi meneja, daktari sijui nani, vyeo vyetu vitakuwa na maana pale tu tunapokwenda kwa wananchi na kuwapa huduma” Alieleza.

Na kuongeza kuwa serikali ya awamu ya tano ipo kuhakikisha kuwa kila kiongozi anayehudumia wananchi anakuwa mtumishi wa wananchi na kuhakikisha kuwa haki inatendeka na kuonya vikali watumishi wanaowahudumia wananchi kwa kutumia lugha chafu.   

Ameyasema hayo kwenye kikao cha muda mfupi kilichowajumuisha viongozi kutoka katika mashirika ya umma, wakala na mamlaka mbalimbali za serikali zilizomo Mkoani humo ili kufahamu matatizo wanayokumbana nayo pindi wanapotimiza wajibu wao wa kuwahudumia wananchi.

Sambamba na hayo Mh. Wangabo amewataka watumishi wote Mkoani humo kuzingatia muda na kutekeleza kwa wakati mipango waliyojiwekea ili kazi zizae matunda na kutoa taarifa sehemu husika bila ya kusubiri kusukumwa.

MWANAMKE ACHARANGWA MAPANGA, ACHINJWA

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399. 
 Imeandikwa na Peti Siyame, Nkasi
MWANAMKE mkazi wa Kijiji cha China Kata ya Kate, Nkasi, Rukwa, Telestina Silanda (45) ameuawa kwa kuchinjwa na mwili kucharangwa na watu wasiojulikana akiwa amelala nyumbani kwake usiku wa kuamkia jana.
Ndugu wa marehemu, Charles Silanda alidai tukio hilo lilitokea saa mbili usiku watu wasiojulikana waliovalia “kininja” walipovamia nyumba yake (shangazi) na kumshambulia kwa panga na kumchinja.
Alisema hadi wao wanajulishwa tukio hilo na kukimbilia eneo la tukio walikuta shangazi ameuawa na wauaji hao wametoweka katika eneo la tukio. Ofisa Mtendaji wa kijiji hicho, Konrad Kauzeni alisema mwanamke huyo aliuawa kinyama, kwa kukatwa miguu yake yote miwili na kuitenganisha na mwili, kichwa na shingo.
Alisema mume wa mwanamke huyo alikuwa amekwenda porini kurina asali kwenye mizinga yake na aliporejea nyumbani alikuta mkewe kauawa kikatili na waliofanya tukio hilo hawajafahamika.
Mkuu wa Wilaya ya Nkasi, Said Mtanda ambaye ni Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama amethibitisha kutokea kwa mauaji hayo akisema ataenda kijiji hicho wananchi wapige kura za maoni ili kuwabaini wauaji hao.
Alisema ni jambo lisilokubalika watu kufanya uhalifu mkubwa kiasi hicho na wakaachwa, hivyo kura za maoni zitasaidia kuwanasa wauaji hao ili sheria ichukue mkondo wake. Aliwataka wakazi wa eneo hilo kwenda ofisini kwake kutoa taarifa za siri kwa wale wanaowafahamu.
CHANZO HABARI LEO

RC RUKWA AAHIDI KUIMARISHA UTENDAJI KAZI WA WATUMISHI WA RUKWA KATIKA SEKTA ZOTE

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.

 Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Mh. Joackim Leonard Wangabo (kushoto) na Mh. Zelote Stephen (Waliokaa) katika picha ya pamoja na Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa, Wakuu wa Wilaya pamoja na baadhi ya Wakurugenzi wa Halmashauri na Mwenyekiti wa CCM Mkoa.
 Mkuu nwa Mkoa wa Rukwa, Mh. Joachim Leonard Wangabo akisalimiana na Meneja wa PS3 Mkoa wa Rukwa Bi. Rose wakati wa kumkaribisha Mh. Wangabo katika Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Rukwa tayari kwaajili ya Kuanza kazi.
Aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Rukwa, Kamishna Mstaafu Zelote Stephen (kushoto) akimkabidhi nyaraka za ofisi Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Mh. Joackim Wangabo. katika makabidhiano ya ofisi hiyo yaliyofanyika katika ukumbi wa ofisi ya Mkuu wa Mkoa. 

 Aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Rukwa, Kamishna Mstaafu Zelote Stephen (kushoto) akisaini nyaraka za ofisi Mkuu wa Mkoa kwaajili ya Kumkabidhi ofisi hiyo Rukwa Mh. Joackim Wangabo. 

​Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Mh. Joackim Wangabo amewatahadharisha watumishi kutobweteka baada ya aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Kamishna Mstaafu Zelote Stephen kustaafu na kumkabidhi yeye kijiti cha utekelezaji wa shughuli za maendeleo ya mkoa.

Amesema kuwa hatomwangusha Rais Dk. John Pombe Magufuli kwa kumuamini na kumkabidhi madaraka hayo na kuahidi kuwa ataimarisha elimu inayoonekana bado ipo chini kwa ufaulu lakini pia kuendeleza kasi ya uzalishaji katika kilimo.

“Baada ya kusoma kabrasha hili la kukabidhiana ofisi kuna mambo mengi ya kuyazingatia ikiwemo, elimu, kilimo, ulinzi na usalama, utunzaji wa mazingira, uvuvi na uwekezaji katika viwanda. Hasa katika elimu maana mimba ni nyingi, kuna upungufu wa madawati, upungufu wa vyumba vya madarasa lakini pia kiwango cha ufaulu hakijafikia kile kilichopo katika ilani ya Chama cha Mapinduzi ambayo ni asilimia 80 kwa darasa la saba,” Alisisitiza.

Mh. Wangabo ameyasema hayo katika makabidhiano ya ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Rukwa mapema leo hii tarehe 31/10/2017 katika ukumbi wa ofisi hiyo, jambo lililoshuhudiwa na watumishi wa sekretariet ya Mkoa pamoja na baadha ya Halamashauri.

Katika kuhakikisha utendaji kazi unakuwa wa ufanisi Mh. Wangabo amesema kuwa hupemda kusikiliza mipango ya watendaji inayotekelezeka ili waweze kuitekeleza kama walivyoipanga nay eye ataisimamia na kutoa ushauri wa kuongeza kasi ya utekelezaji pale inapobidi ili kuyafikia malengo waliyojiwekea kwa wakati.

Kwa upande wake aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Kamishna Mstaafu Zelote Stephen amewashukuru watumishi wote wa serikali katika Mkoa wa Rukwa pamoja na wananchi wa mkoa kwa kumpa ushirikiano katika kipindi chote alichokuwepo na kuwaomba waendeleze kumpa ushirikiano huo huo Mkuu wa Mkoa mpya ili naye aweze kufanya majukumu yake kwa ufanisi.

SERIKALI YADHAMIRIA KUFUNGUA UTALII WA KANDA YA KUSINI, YAPO MAPOROMOKO YA PILI KWA KUWA NA KINA KIREFU ZAIDI BARANI AFRIKA

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Japhet Hasunga (kulia) akiteta jambo na Mkurugenzi Mwendeshaji wa kampuni ya Greens Construction Limited, Hamimu Bakari wakati akishuka kwenye ngazi maalum zinazojengwa na mkandarasi huyo kwa ajili ya kuwawezesha watalii kushuka hadi kwenye kina cha Maporomoko ya Mto Kalambo wakati wa ziara yake mkoani Rukwa. Maporomoko hayo ambayo ni ya pili kwa kina kirefu barani Afrika baada ya TUGELA yaliyopo Afrika ya Kusini yana kina cha mita 235 na upana kati ya mita 3.6 hadi 18. 

Na Hamza Temba - WMU
...............................................................
SERIKALI imesema imedhamiria kufungua utalii wa Kanda ya Kusini ili kupanua wigo wa vivutio vya utalii nchini na hatimaye kuongeza idadi ya watalii na kipato kwa Serikali na jamii kwa ujumla.

Hayo yamesemwa na Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Japhet Hasunga katika kijiji cha Kapozwa Wilaya ya Kalambo Mkoani Rukwa wakati wa ziara yake ya siku moja ya kutembelea Maporomoko ya Mto Kalambo ambayo ni ya pili kwa kina kirefu barani Afrika baada ya Maporomoko ya Tugela yaiyopo nchini Afrika ya Kusini.

Alisema kwa sasa vivutio vingi vinavyotumika kwa utalii nchini ni vile vya ukanda wa Kaskazini hususan vya wanyamapori ambavyo vimeanza kuelemewa kutokana na watalii wengi kutembelea ukanda huo zaidi kuliko Kanda ya Kusini ambayo pia ina vivutio mbalimbali vya asili.

Alisema Serikali kwa kushirikiana na wadau mbalimbali wa maendeleo ikiwemo benki ya Dunia kupitia mradi wa REGROW imepanga kuboresha miundombinu ya vivutio vya utalii vya Kanda ya Kusini na kuvitangaza ili kuimarisha sekta hiyo muhimu ambayo inachangia asilimia 25 ya mapato yote ya kigeni na asilimia 17.5 ya pato la taifa.

Katika ziara yake hiyo Mkoani Rukwa, alitembelea eneo la Hifadhi ya Msitu ya Mto Kalambo na kukagua ujenzi unaoendelea wa ngazi maalum zitakazowawezesha watalii kushuka hadi kwenye kina cha Maporomoko ya Mto Kalambo ambacho ni mita 235 na upana kati ya mita 3.6 hadi 18. 

Alisema Serikali kupitia Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania inajenga ngazi hizo ili kuongeza thamani ya maporomoko hayo huku akiagiza Wakala hiyo kwa kushirikiana na wadau wengine kuongeza juhudi za uwekezaji ili kuimarisha utalii wa kivutio hicho na kupanua kanda yote ya kusini.

"Tumekusudia kupanua wigo wa vivutio vyetu vya utalii kwa kufungua Kanda hii ya Kusini ambayo ina vivutio vingi ambavyo havijachangia ipasavyo kwenye uchumi wetu, maporomoko haya ni moja ya kivutio adimu katika ukanda huu. 

"Ni wakati muafaka sasa tushirikiane kuhamasisha wawekezaji kujenga mahoteli ya kisasa katika eneo hili, tuone uwezekano wa kuanzisha utalii wa 'cable cars' kuwezesha watalii kuona maporomoko kiurahisi, tujenge maeneo ya kupumzikia ili kuweka mazingira rafiki ya kupata watalii wengi na mapato yaongezeke" alisema Hasunga.

Aidha, alitoa wito kwa wananchi wa kijiji cha Kapozwa ambao wanaishi jirani na hifadhi hiyo kushirikiana na Serikali katika uhifadhi wa uoto wa asili wa hifadhi hiyo pamoja na kudumisha tamaduni zao kwa kusajili vikundi vya ngoma na kutunga nyimbo za kabila lao kwa ajili ya kutumbuiza watalii watakaofika kuona maporomoko hayo na hivyo kujitengenezea kipato kupitia utalii wa Kiutamaduni.

Pamoja na Maporomoko hayo kivutio vingine kinachopatikana ukanda wa kusini ni Hifadhi ya Taifa ya Ruaha ambayo ni ya pili kwa ukubwa nchini baada ya hifadhi ya Taifa ya Serengeti, hifadhi hii inasifika kwa kuwa na tembo wengi kuliko hifadhi nyingine nchini.

Hifadhi ya Taifa ya Kitulo ni kivutio kingine katika ukanda huu ambacho sifa yake kubwa ni uwepo wa aina nyingi za maua ndwele ya asili ambayo hayapatikani kwingineko duniani, sifa hiyo imesababisha wenyeji kuita hifadhi hiyo 'Bustani ya Mungu'. Wataalamu wa uhifadhi wanasema endapo maua yaliyopo Kitulo yangekuwa ni wanyamapori basi hifadhi hiyo ingeizidi wanyama waliopo Serengeti.

Vivutio vingine ni pamoja na Hifadhi ya Taifa ya Katavi ambayo ni ya tatu kwa ukubwa nchini, Hifadhi ya Taifa ya Udzungwa, Mikumi, Mahale, Gombe, Pori la Akiba la Selous, Hifadhi ya Mazingira Asilia ya Mlima Rugwe na Kimondo cha Mbozi.
Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Japhet Hasunga (kushoto) akiteta jambo na Katibu Tawala Wilaya ya Kalambo Frank Schalwe wakati akishuka kwenye ngazi maalum zinazojengwa kwa ajili ya kuwawezesha watalii kushuka hadi kwenye kina cha Maporomoko ya Mto Kalambo wakati wa ziara yake mkoani Rukwa. Maporomoko hayo ambayo ni ya pili kwa kina kirefu barani Afrika baada ya TUGELA yaliyopo Afrika ya Kusini yana kina cha mita 235 na upana kati ya mita 3.6 hadi 18. 
Meneja wa TFS Wilaya ya Kalambo, Joseph Chezue (kushoto) akimuonyesha Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Japhet Hasunga (kulia) ngazi maalum zinazojengwa kwa ajili ya kuwawezesha watalii kushuka hadi kwenye kina cha Maporomoko ya Mto Kalambo wakati wa ziara yake mkoani Rukwa. Maporomoko hayo ambayo ni ya pili kwa kina kirefu barani Afrika baada ya TUGELA yaliyopo Afrika ya Kusini yana kina cha mita 235 na upana kati ya mita 3.6 hadi 18.
 Muonekano wa ngazi hizo kuelekea kwenye Maporomoko ya Mto Kalambo.
Muonekano wa ngazi hizo.

Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Japhet Hasunga (katikati) akizungumza na waandishi wa habari muda mfupi baada ya kukagua ujenzi wa ngazi maalum zinazojengwa kwa ajili ya kuwawezesha watalii kushuka hadi kwenye kina cha Maporomoko ya Mto Kalambo wakati wa ziara yake mkoani Rukwa. Maporomoko hayo ambayo ni ya pili kwa kina kirefu barani Afrika baada ya TUGELA yaliyopo Afrika ya Kusini yana kina cha mita 235 na upana kati ya mita 3.6 hadi 18. Kushoto ni Mkuu wa Wilaya ya Kalambo, Julieth Binyura. 
Baadhi ya washiriki wa ziara hiyo wakishuka kwenye ngazi ambazo ujenzi wake bado unaendelea. Ujenzi huo ukikamilika ngazi hizo zitakuwa na urefu wa mita 227.
Ngazi hizo zimejengwa kwenye ukingo wa korongo la Mto Kalambo.
Sehemu ya juu ya Maporomoko ya Mto Kalambo.
 Muonekano wa mto Kalambo ambao unaotengeneza Maporomoko ya Mto Kalambo (Kalambo Falls)
Taswira ya maporomoko ya mto Kalambo kutokea angani (Picha hii ni kwa hisani ya Mtandao)

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Rukwa Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa