SEKTA ya afya mkoa wa Rukwa inakabiliwa na changamoto kadhaa ikiwemo
upungufu mkubwa wa kada za kitaalamu ambapo uwiano uliopo daktari mmoja
analazimika kuhudumia wagonjwa 200,000 kwa mwaka.
Kaimu Mganga Mkuu wa mkoa wa Rukwa, Dk Hans Ulaya alisema idadi hiyo
ya wagonjwa ni zaidi ya mara nane ya uwiano wa Kitaifa, ambapo daktari
mmoja anahudumia wagonjwa 25,000 kwa mwaka.
Dk Ulaya alibainisha hayo wakati wa kikao cha Ushauri wa mkoa wa
Rukwa (RCC) kilichofanyika juzi mjini hapa chini ya uenyekiti wa Mkuu wa
Mkoa wa Rukwa, Magalula Said.
Aliongeza kuwa uhaba wa kada za kitaalamu pia umewakumba wauguzi
ambapo muuguzi mmoja mkoani humo analazimika kuhudumia wagonjwa 30,000
kwa mwaka, ikiwa ni mara sita zaidi ya uwiano wa kitaifa ambapo muuguzi
anahudumia wagonjwa 5,000 tu kwa mwaka.
Dk Ulaya alisema sekta hiyo pia inakabiliwa na upungufu mkubwa wa
vituo vya afya vya kutolea huduma ya afya vipatavyo 188 ukilinganisha na
idadi ya kata na vijiji vilivyopo.
Akifafanua alieleza kuwa changamoto nyingine kubwa ni halmashauri ya
Sumbawanga na Kalambo hazina hospitali hivyo hutumia hospitali ya mkoa
kama ya wilaya na kwamba kata zipatazo 77 hazina vituo vya afya na
vijiji 153 havina zahanati.
Takwimu za hivi karibuni zinaonesha kuwa mkoa wa Rukwa una idadi ya
kata zipatazo 97 na vijiji 341, ambapo idadi ya vituo vya afya ni 20 tu
na zahanati zikiwa 179. Kwa mujibu wa Magalula ili kukabiliana na tatizo
la upungufu wa watumishi wenye taaluma mkoa unajitahidi kuwaendeleza
kitaalamu watumishi wachache waliopo na kuomba vibali vya kuajiri
watumishi wapya.
Chanzo: Habari Leo
0 comments:
Post a Comment