Home » » MZINDAKAYA,ASEMA JINO KWA JINO MBELE YA PINDA

MZINDAKAYA,ASEMA JINO KWA JINO MBELE YA PINDA

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399. 
  Juhudi za RC kuwasuluhisha zakwama
  Mzindakaya asema hawezi kuwa juha
Waziri Mkuu,Mizengo Pinda.
 
Vita yenye mwonekano wa kisiasa inazidi kushamiri kati ya Mbunge wa Sumbawanga Mjini (CCM), Aeshi Hilaly na mtangulizi wake, Dk Chrisant Mzindakaya, safari hii ikiwa mbele ya Waziri Mkuu, Mizengo Pinda.
Mzindakaya ametamka hadharani kwamba hatamsamehe `kirahisi’ Hilaly ambaye ni miongoni mwa wanasiasa vijana mkoani Rukwa, ikiwa ni baada ya vita ya maneno iliyodumu kwa zaidi ya miaka miwili kati yao.

Wakati Hilaly amekuwa akitumia fursa ya kuwapo bungeni, kumshughulikia Mzindakaya, mwanasiasa huyo mkongwe anaelezwa kutumia uzoefu na kukubalika kwake `kujibu mapigo’ jimboni humo.

Jana, Dk. Mzindakaya, alikataa mbele ya hadhara ya waumini wa dini ya kikristo wakiongozwa na Pinda, kumsamehe Hilaly, ikiwa ni sehemu ya jitihada za kuzika tofauti zao za kisiasa.

Wanasiasa hao walikutaka jana kwenye ibada ya kusimikwa kwa Askofu wa  Kanisa la Moravian, Jimbo la Rukwa, Cornad Nguvumali, iliyofanyika kwenye uwanja wa michezo wa Nelson Mandela uliopo mjini hapa.

Ibada hiyo iliwajumuisha viongozi mbalimbali wa kitaifa akiwemo viongozi wa madhehebu ya dini ya kikristo nchini.

Dk. Mzindakaya, alifikia hatua hiyo ya kugoma kumsamehe Hilaly baada ya Mkuu wa Mkoa wa Rukwa, Stella Manyanya, kuwaita jukwaani akitaka washikane mikono ikiwa ni hatua ya kuzika tofauti zao zinakadiriwa kuanza mwaka 2010.

Baada ya ombi la Manyanya, Dk. Mzindakaya alisema kuwa alipoombwa na Waziri Mkuu kutoa msamaha kwa Mbunge huyo, alitoa utaratibu wa kutumika kupitia vikao vya ki-chama ikiwa pamoja kuitishwa vikao kwa maeneo yote ambayo mbunge huyo  alifanya mikutano na kuchafua heshima mwanasiasa huyo mkongwe nchini.

"Sasa miye ni mtu mzima, nafsi ya msamaha inahitaji kuandaliwa miye sijaandaliwa kiroho kwa ajili ya jambo hili...tayari nilitoa utaratibu kwa wazee wa Chama cha Mapinduzi (CCM) watuite mimi na kijana wangu, nipo tayari kumsamehe,” alisema na kuongeza:

“Lakini hapa siyo mahali pake hapa ni sehemu ya kidini, siyo kuleta siasa hapa na nikisema hapa nitakuwa juha," alisema Dk. Mzindakaya.

Awali, Manyanya akiri kutowashirikisha wanasiasa hao kwenye jambo hilo alidai kutoridhishwa na jinsi ambavyo hawaelewani, kitu ambacho kinatia doa uhusiano wa watu hao, na jinsi ambavyo hawawezi kushirikiana kwenye mambo ya maendeleo mkoani humo.

Manyanya alianza kwa kumsimamisha Aeshi kwenye hadhara hiyo ambapo mwanasiasa huyo alikiri kuwapo kwa misuguano baina yake na Dk. Mzindakaya.

Alisema tofauti hiyo imekuwapo kwa kipindi kirefu sasa na kusababisha kuibuka makundi ndani ya CCM, hali anayoiona ni kosa hivyo kuomba Dk Mzindakaya amsamehe mbele ya hadhara hiyo.

"Siku zote tunatofautia miye na mzee wangu, lakini hakuna mrefu yasiyo…mzee wangu Mzindakaya najua nilikukosea au inawezekana wewe ulinikosea, lakini ya kale si ndwele tugange yajao, naomba unisamehe....miye nimetamka hapa mbele ya Mungu kuna viongozi wa dini," alisema Aeshi

CHANZO CHA MGOGORO
Mgogoro baina ya Hilaly na Dk. Mzindakaya, ulianza wakati wa kura za maoni mwaka 2010 ndani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM),baada ya Hilaly kushinda ilidaiwa Mzindakaya aligoma kumuunga mkono.

Hata hivyo, inaelezwa baadaye alijitokeza mwanachama wa CCM, Nobert Yamsebo, ambaye alihamia Chama cha Demakorasia na Maendeleo (Chadema), na kugombea kwenye jimbo hilo huku wazee maaruifu wa CCM wakikimbilia Chadema na kumpigia kampeni mgombea wa Chadema.

Aidha, baada ya Hilaly kushinda, inadaiwa alitumia mikutano ya hadhara kumzungumzia Dk. Mzindakaya kuwa ni fisadi kutokana na kupangisha nyumba ya serikali kwa Sh. 50,000 kwa mwezi kisha kuipangisha kwa kampuni ya ujenzi wa barabara ya Tunduma hadi Sumbawanga Mjini kwa Dola 400 za Marekani.

Aidha, mara kwa mara Hilaly amenukuliwa akiwaeleza wananchi kuwa yuko tayari kwenda mahakamani kusaidia nyumba hizo kurudi serikalini, ili zipangishwe na kuiingizia serikali mapato.

CCM YASHANGAZWA
Hata hivyo, uamuzi wa Manyanya, kuwapatanishwa wahasimu hao hadharani kwenye ibada, kuliwashangaza viongozi wa CCM.

 Mwenyekiti wa CCM mkoa wa Rukwa, Hypotrius Matete, alisema ndani ya chama hicho wameitisha vikao mara mbili kwa lengo la kufanya suluhu, na vyote Dk. Mzindakaya anahudhuria Mbunge Hilaly haudhurii .

“Nimeshangazwa na uamuzi wa RC kuwaita mbele ya ibada ili awapatanishe, kama ni suluhu suluhu ilipaswa kufanyika ndani ya vikao vya chama na tulishaanza,” alisema.

PINDA: WAPENI UHURU WAUMINI WENU
Kwa upande wake, Pinda ambaye alimwakilisha, Rais Jakaya Kikwete, aliwataka viongozi wa kidini kuwapa uhuru waumini wao kuwa na mapenzi na vyama vya kisiasa wanavyotaka lakini wasifuate misimamo ya nyumba zao za ibada.

"Kuna viongozi wanawanyima waumini wao uhuru wa kupenda chama cha siasa anachotaka...kila muumini awe na uhuru wa kuchagua chama anachotaka siyo kulazimishwa kufuata msimamo wa kanisa," alisema Pinda.
CHANZO: NIPASHE
Jika Anda menyukai Artikel di blog ini, Silahkan klik disini untuk berlangganan gratis via email, dengan begitu Anda akan mendapat kiriman artikel setiap ada artikel yang terbit di Creating Website

0 comments:

Post a Comment

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Rukwa Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa