Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
Imekuwa ni kawaida kwa watu hapa nchini kufanya biashara bila kufuata taratibu na kanuni za kisheria.
Ni kutokana na kutojali sheria na kanuni, wapo
watu ambao hujikuta katika wakati mgumu ikiwa ni pamoja na kufilisiwa
biashara zao.
Sababu ya kufilisiwa inaweza kuwa ni kutokana na
kuingia mikataba bila kujua taratibu za sheria za kibiashara. Wapo ambao
kwa sababu ya kutojua sheria na kanuni za biashara wamekuwa wakiingia
kwenye migogoro na Serikali au watu binafsi kimakosa.
Ninachotaka kusema katika safu hii ni kwamba kabla
ya kuanzisha biashara yoyote, penda kuifahamu biashara hiyo kisheria;
kwa mfano unataka kufanya biashara ya kuuza ngozi ya ng’ombe, kuuza dawa
za wanyama au binadamu, sheria zinasemaje hasa?
Ni mambo muhimu sana kuyafahamu. Wapo watu wengi
wamekuwa wakisumbuliwa na sheria, sababu kubwa ni wao wenyewe kuanzisha
biashara pasipo kuangalia hasa sheria zinasemaje.
Biashara ni nini? Ni shughuli yoyote inayohusisha
uuzaji na ununuzi wa vitu au huduma yoyote, kwa lengo la kupata faida.
Biashara inaweza kufanywa na mtu binafsi (sole proprietorship), kampuni
au kwa kuingia kwenye ubia.
Mfanyabiashara binafsi ni nani? Ni mtu yeyote
aliyeamua kuanzisha biashara yoyote akiwa mmiliki pekee ambaye atakuwa
ametoa mtaji wake mwenyewe, faida na hasara zote zinakuwa kwake.
Sheria za biashara nchini; Sheria zinazosimamia
uanzishaji wa biashara ni zikiwamo zile za usajili wa majina ya biashara
(Business names Registration Act Cap 213) na Sheria ya Kodi ya Mapato (
The Income Tax Act). Pia sheria ya Leseni za Biashara Sura ya 208 (The
Business Licence Act Cap 208).
Sheria nyingine zinategemeana na aina ya biashara
yako mfano, kama ni biashara ya dawa utahitaji kibali cha Taasisi ya
Chakula na Dawa (Tanzania Food and Drugs Authority;TFDA).
Nimelazimika kuyatumia haya maneno ya kiingereza
kutokana na ukweli kuwa ndiyo tunayokutana nayo tunapokwenda kusajili,
kwani Kiingereza kinafahamika nchini kama lugha ya kiofisi.
Utaratibu wa kufuata ili kuanzisha biashara
Ukishakuwa na mtaji pamoja na nia ya kuanzisha
biashara, hatua ya kwanza ni kusajili jina la biashara kwa Wakala wa
Usajili wa Biashara (BRERA; Business Regulatory and License Agency).
Pili, unatakiwa kuwa na leseni ya biashara ambayo hupatikana
katika ofisi za manispaa husika chini ya Sheria ya Leseni ya Biashara
Sura ya 208 kifungu cha 3 ambacho kinasema ni marufuku kufanya biashara
bila kuwa na leseni halali katika eneo halali.
Tatu unatakiwa kwenda TRA na kupata namba ya mlipa kodi au kwa lugha ya Kiingereza Tax Identification Number (TIN).
Vibali vingine vitatolewa kulingana na shughuli
unayotaka kuifanya, kwa mfano kuna biashara zinalazimisha uwe na vibali
kutoka Shirika la Viwango la Taifa (TBS), TFDA, Baraza la Taifa la
Usimamizi wa Mazingira (NEMC), Baraza la Wakala wa Usalama na Afya
mahala pakazi (OSHA) na vinginevyo.
Faida za kuwa mfanyabiashara binafsi
Mfanyabiashara binafsi ana faida nyingi ikiwa ni
pamoja na ukweli kwamba hata uanzishaji wake ni rahisi, faida zinakuja
moja kwa moja kwa mfanyabishara, kuingiza mshirika mwingine ni rahisi,
uanzishaji wake hauna gharama sana, ni rahisi kuibadili na kufuata aina
nyingine ya kufanya biashara.
Itaendelea Alhamisi
Jebra Kambole ni mtaalamu wa sheria kutoka Kampuni ya Law Guards Advocates ya Jijini Dar es Salaam.
Chanzo:Mwananchi
Chanzo:Mwananchi
0 comments:
Post a Comment