SIKU
zote tunaamini Polisi wako kwa ajili ya kulinda na kuhakikisha usalama
wa raia. Hata hivyo dhana hiyo huenda ikaanza kuleta utata hasa kutokana
na matukio ya ukatili yanayohusisha polisi kuongezeka kila wakati.
Matukio
mengi ya polisi kunyanyasa raia ikiwemo mahabusu yamekuwa yakiripotiwa
katika vyombo vya habari, jambo ambalo linasikitisha na kutia huzuni
sana, hasa ukizingatia kuwa watu wengi wamekuwa wakiamini kuwa polisi
ndio kimbilio lao, sehemu ambayo haki na usalama vinaweza kupatikana.
Hata
habari za polisi kunyanyasa mahabusu zimekuwa zikiandikwa ama
kuripotiwa katika vyombo vya habari jambo ambalo kimsingi linatia doa
jeshi hilo, zaidi kuleta woga kwa watu wanaojikuta wamevunja ama kukiuka
Sheria na kujikuta mikononi mwa Polisi.
Kilichonisukuma
hasa kuzungumzia hili ni tukio lililoripotiwa na vyombo vya habari
kutoka Sumbawanga ambapo polisi wanane akiwemo mmoja wa kike kutuhumiwa
kumtesa mahabusu mwanamke kwa kumvua nguo na kumuingizia chupa ya bia
katika sehemu za siri.
Ukisoma
habari hii, kama una moyo mwepesi sana unaweza usimalize kuisoma kwani
inaogofya na kusikitisha kuona binadamu anavyoweza kubadilika na kuwa
katili kwa binadamu mwingine kwa kiwango cha namna hii.
Lakini
cha kuogofya zaidi ni vitendo hivyo kufanywa na polisi ambao wamepewa
jukumu la kulinda na kuhakikisha usalama wa raia wake haijalishi mtu
huyo ni mkosaji kiasi gani, kwani ndio maana kuna Mahakama ambazo
zinajukumu la kusikiliza kesi na mwisho kutoa hukumu kwa mtuhumiwa.
Kitendo
cha mshtakiwa aliyetajwa kwa jina la Clara God kufanyiwa unyama huo na
polisi ni kitendo cha unyanyasaji na ukatili wa kutisha ambao naamini
hakipaswi kufumbiwa macho. Mtuhumiwa huyo na wenzake watatu wa kiume
wanakabiliwa na kesi ya unyang’anyi wa kutumia silaha na wako rumande
kwa kuwa kesi yao haina dhamana.
Akizungumza
mbele ya Hakimu Mkazi wa mjini Sumbawanga, Rosalia Mugissa, mshitakiwa
Clara akibubujikwa na machozi alieleza namna askari Polisi walipofika
nyumbani kwake katika Kitongoji cha Chanji na kumtaka aeleze alipomficha
mumewe na kisha kumchukua kwa nguvu na kumbambikia kesi hiyo ya
unyang’anyi wa kutumia silaha.
Kisha
mtuhumiwa huyo ndipo alipoeleza unyanyasaji na kitendo cha ukatili
alichofanyiwa na askari hao, kwa kudhalilishwa kwa kuvuliwa nguo na
kisha kulazimishwa kukalia chuma na machungu aliyopitia mwanamke huyo.
Ninachoamini
polisi wana njia nyingi za kulazimisha mtuhumiwa kusema ukweli au
kukiri makosa lakini vitendo vya namna hii havipo katika taratibu hizo,
huu ni ukatili ambao viongozi wa Jeshi la Polisi wanapaswa kuvifuatilia,
kuvikemea na kuvikomesha kabisa.
Vile
vile bado ninaamini hawa ni baadhi ya polisi ambao hawana ubinadamu,
utu na maadili na ndio wanaochafua Jeshi la Polisi na kufanya watu waone
kama polisi ni watu waliojaa ukatili wakati wako polisi wengi
wanofahamu wajibu wao wa kulinda raia na haki zao.
Ninachojiuliza
unapomfanyia mtu ukatili wa namna hii, halafu baadaye ikabainika kuwa
hana kosa lolote, unajisikiaje? Najikuta nikijiuliza, hivi kwenye Jeshi
letu la Polisi watu wanaoajiriwa wengine ni majambazi au ni wauaji,
nashindwa kupata jibu la haraka maana kwa akili za kawaida unashindwa
kuamini polisi mwenye maadili na aliyesomea wajibu wake vizuri anaweza
kuwa katili kiasi hiki.
Ninachoelewa
hata mahabusu au mfungwa ana haki yake kama binadamu mwingine yoyote na
hastahili wala hapaswi kufanyiwa ukatili wa namna hii hata kama
amefanya kosa kubwa kiasi gani.
Kuna
haja sasa ya viongozi wa Polisi kufuatilia polisi wake kwa umakini ili
wale watakaobainika kuwa na mambo yasioeleweka waondolewe mapema, badala
ya kuacha waendelee kuwanyanya na kutesa watu kwa kiwango cha namna hii
na kuchafua jeshi hilo kwani inasikitisha na inahuzunisha.
Chanzo;Mwananchi
0 comments:
Post a Comment