WAKAZI wa Kata ya Mtowisa wilayani Sumbawanga, Rukwa wamewakatalia
madiwani sita wakiongozwa na Mwenyekiti wa halmashauri ya wilaya hiyo
kufanya mkutano wa hadhara kwenye eneo lao wakishinikiza gari la
wagonjwa lirejeshwe kwenye kituo chao cha afya.
Inadaiwa kuwa mkutano huo ulilenga kuzungumzia matumizi ya gari la
kubebea wagonjwa lililotolewa msaada kwa kituo cha afya Mtowisa na
mashirika ya Africare, Jhpego na Plan International kupitia mradi
wanaotekeleza wa wazazi na mwana.
Mmoja wa wananchi hao, George Edwin alisema waliwakatalia madiwani
hao wasifanye mkutano wa hadhara eneo hilo kwani haukuwa na tija kwao
na walichokuwa wakikihitaji na kuona gari hilo la wagonjwa.
“Hawa jamaa wanaleta siasa kwenye mambo ya msingi, gari lilitolewa
msaada kwa kituo cha afya Mtowisa, lakini linafanya shughuli nyingine
mjini… hatujaliona kwa zaidi ya miezi miwili na nusu, wajawazito watatu
wamekufa kwa kukosekana gari hilo, sasa wanakuja na siasa, sisi
tumewaeleza mkutano haufanyiki ila tunataka gari lirudishwe kituoni,”
alisema.
Alisema baadaye madiwani hao walielewa na kupiga simu ofisi ya
mkurugenzi, ambapo aliamuru gari hilo lirejeshwe kituoni hapo na
kupokelewa kwa shangwe na wananchi hao.
Edwin akizungumzia jaribio la kulichoma moto gari hilo, alisema
zilikuwa hasira tu za vijana, lakini baadae walikaa na kutafakari kuona
umuhimu wa gari hilo kurudi kituoni kuendelea kutumika kwa malengo
yaliyokusudiwa na si kutumiwa na mkurugenzi kwa shughuli nyingine.
Mwenyekiti wa halmashauri hiyo, Edes Maembe alikiri wao kupata wakati
mgumu baada ya kugomewa na wananchi hao, lakini alisisitiza kwamba
mkutano huo ulilenga kueleza hatua ambazo madiwani wamepanga kuchukua
baada ya uchunguzi kukamilika kuhusu tuhuma zisizo sahihi za gari hilo
kwani sehemu kubwa lilikuwa likionekana wilayani Mpanda, Katavi.
Mwenyekiti Maembe aliongeza kuwa utaratibu uliowekwa hivi sasa ni
kuhakikisha gari hilo linakaa muda wote kituoni hapo ili litumike kwa
walengwa waliokusudiwa kwenye mradi huo ambao ni wakazi wa bonde la
ziwa Rukwa na si vinginevyo.
Hivi karibuni kulitokea tafrani baada ya mjamzito kufariki dunia
wakati akisubiri gari litoke mjini ili limpeleke hospitali ya mkoa
mjini Sumbawanga kwa upasuaji baada kushindwa kujifungua kwa njia ya
kawaida, lakini lilichelewa kwa zaidi ya saa saba hivyo wananchi
kukasirika na kuvunja vioo vya gari huku likinusurika kuchomwa moto.
Chanzo:Tanzania daima
0 comments:
Post a Comment