SAKATA la ndoa iliyovunjwa na Mahakama ya Mwanzo Wilaya ya Nkasi,
Rukwa limeingia katika sura mpya baada ya kubainika kuwa mume aliyeomba
kuvunjwa kwa ndoa yake, Ndebile Kazuri, alimkatisha masomo mkewe baada
ya kumtia mimba akiwa darasa la sita.
Kwa mujibu wa vyanzo vya habari ambavyo mwandishi wa habari hii
amevipata, Kazuri ambaye hivi karibuni ameiomba mahakama hiyo kuvunja
ndoa yake na Maria Tarafa kwa madai ana kiburi na mdokozi wa vitu ndani
ya nyumba yao, alimkatisha masomo na baadaye kumuoa mwaka 2004.
Taarifa zinaeleza kuwa Kazuri alikatisha masomo ya Maria akiwa Shule
ya Msingi Isale wilayani Nkasi wakati huo akiwa na miaka 15 na
alijifungua mtoto akiwa na miaka 16.
Ilidaiwa kwamba baada ya kupata ujauzito, wazazi wa pande zote mbili
walizungumza kifamilia na kukubaliana wasimshtaki Kazuri kwa kuwa
atafungwa jela huku Maria na mtoto wake watakosa huduma, hivyo
walikubaliana waoane ndipo mwanaume huyo alipolipa mahari na kufunga
ndoa.
Akizungumza na gazeti hili, Maria alikiri kukatishwa masomo na Kazuri
mwaka 2003 akiwa darasa la sita, lakini kwa kuwa baba zao walikuwa
marafiki walikubaliana waoane.
Alisema aliunganishwa na mumewe Kazuri mwaka 2004 akiwa na umri wa
miaka 16 baada ya kulipa mahari ya ng’ombe kwa familia yao.
“Inaniuma kwa kitendo ambacho ananifanyia kwa sasa kwani alinikatisha
masomo, kanipotezea muda wangu na kaniongezea mzigo wa watoto wanne na
anataka niende kuishi nao peke yangu baada ya kwenda kuongopa
mahakamani,” alisema Maria.
Alisema sababu alizozitoa mahakamani si za kweli kwani amekuwa
akimpiga na kumnyanyasa ndani ya ndoa yake na kumtaka aondoke kwake na
kwenda kuishi kwao.
Maria alisema kuna kipindi mtalaka wake huyo aliwahi kumfukuza akiwa
na watoto wawili na kurudi nyumbani kwao, lakini baadaye alikuja kuomba
radhi na kutaka apewe mke wake aende kuishi naye.
Kazuri alifungua kesi namba katika Mahakama ya Mwanzo, Namanyere
Oktoba 28, 2013 iliyosikilizwa na Hakimu B. Stanley na Novemba 18, 2013
hakimu huyo aliamuru ndoa ivunjwe.
Mahakama ilivunja ndoa hiyo na kuamuru Maria aondoke na watoto wawili
kati ya wanne aliozaa na mumewe bila kueleza namna watakavyopata
huduma toka kwa baba yao.
Katika hukumu yake, mahakama iliamuru watoto wa miaka saba na tisa
watabaki kwa baba yao na wenye miaka chini ya saba kubaki na mama yao.
Mahakama hiyo ya mwanzo pia iliamuru mke apewe magunia tisa ya
mahindi kati ya 10 ambayo walizalisha wote na mabati saba yaliyokuwa
nyumbani kwao.
Hata hivyo, alipotafutwa Kazuri kuzungumzia madai hayo kwa njia ya
simu hakuweza kupatikana kwani taarifa ambazo zimetufikia ni kwamba,
kwa sasa anashikiliwa na Jeshi la Polisi Wilaya ya Nkasi kwa kitendo
cha kuvunja nyumba ya mtalaka wake na kumtishia kumdhuru huku akimtaka
aondoke kwake.
Chanzo;Tanzania Daima
0 comments:
Post a Comment