Na Walter Mguluchuma-Blogs za mikoa
Mpanda
MTOTO wa kiume mwenye ulemavu wa ngozi ‘albino” Mwigulu Matomange Magessa mwenye umri wa miaka saba ameshambuliwa na vijana watatu walivaa kininja na kuunyofoa mkono wake mmoja na kutokomea na kusikojulikana .
Kwa mujibu wa Diwani wa Kata ya Milepa , Apolinari Macheta tukio hilo lilitokea saa kumi na moja jioni wakati Mwigulu ambaye anasoma Darasa la Kwanza katika Shule ya Msingi Msia katika Kata ya Milepa, Bonde la Ziwa Rukwa wilayani Sumbawanga akirejea nyumbani Msia mashambani akiwa ameongozana na kundi la wanafunzi wenzake.
Kwa mujibu wa Diwani , Macheta , mtoto Mwigulu amelazwa katika zahanati ya Mtowisa katika Bonde la Ziwa Rukwa wilayani Sumbawanga kwa matibabu ambapo hali yake inaelezwa kuwa bado ni tete kwani alifikishwa kwenye zahanati hiyo akiwa amepoteza fahamu .
Akisimulia kisa hicho cha kusikitisha , Diwani Macheta amedai kuwa kijiji cha Msia kimegawanyika sehemu mbili “Msia Center” na “Msia mashambani’ ambapo mtoto Mwigulu akiwa ameongozana na kundi la wanafunzi wenzie wakirejea nyumbani ‘Msia Mashambani’ baada ya masomo ghafla vijana watatu wanaodaiwa kuvaa kininja waliwagutusha ambapo mmoja wao anadaiwa kumkimbiza Mwingulu huku wengine wawili wakiwafukuza wanafunzi wengine.
“Licha ya wanafunzi hao kupiga kelele zao haziweza kusikika kijijini kwani walikuwa mbali na makazi ya watu …… ndipo yule kijanammoja aliyekuwa akimfukuza mtoto ‘albino’ akiwa na panga aliukata mkono wake mmoja na kutokomea nao kusikojulikana “ alisema .
Kwa mujibu wake watoto walipofika kwa wazazi wa kule Msia mashambani waliwasimulia mkasa uliowakuta ndipo ulipoanza msako mkali wa kumtafuta mtoto Mwigulu na kumkuta akiwa mashamba ni huku mkono wake mmoja ukiwa umenyofolewa na kumkimbiza katika zahanati ya kijiji cha jirani cha Mtowisa ambapo amelazwa kwa matibabu.
Jitihada za gazeti hili kumpata Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Rukwa,Peter Ngusa kupitia simu yake ya mkononi kwa majaribio kadhaa hakuwa na mafanikio kwani ilikuwa ikiita bila kupokelewa.
Hata hivyo habari za ndani za kipolisi zinathibitisha kutokea kwa tukio hilo ambapo hadi sasa hakuna yeyote aliyekamatwa .
0 comments:
Post a Comment