Mussa Mwangoka, Sumbawanga-Rukwa yetu
MIKOPO yenye riba nafuu inayotolewa na baadhi ya wafanyabiashara wakubwa waliopo nchini Zambia imekuwa kivutio cha kuwafanya wafanyabiashara wadogo wa samaki wa Tanzania kushawishika kupeleka kuuza bidhaa hiyo nchini humo.
MIKOPO yenye riba nafuu inayotolewa na baadhi ya wafanyabiashara wakubwa waliopo nchini Zambia imekuwa kivutio cha kuwafanya wafanyabiashara wadogo wa samaki wa Tanzania kushawishika kupeleka kuuza bidhaa hiyo nchini humo.
Baadhi ya wafanyabiashara hao wakizungumza kwa nyakati tofauti kwa njia ya simu walisema kuwa, kinachowavuti wao kuuza bidhaa hiyo nchini humo ni mikopo ambayo imekuwa ikisaidia kukuza mitaji yao ya kibiashara.
"Tunalazimika kwenda kuuza samaki nchini humo kwa sababu kuna soko ni la uhakika la bidhaa yao lakini kikubwa ni mikopo ya fedha kwa mfano mimi nilikopeshwa zaidi ya Sh milioni 12, pasipo riba ya aina yoyote ile" alisema Jofrey Simtenda.
Simtenda ambaye huwa anavua kati ya tani 4 hadi 5 kwa usiku mmoja kwa kutegemeana na hali ya ziwa kwa siku hiyo, alisema kuwa pia wanakopeshwa vitendea kazi kama vile mashine za uvuvi na vinginevyo ambapo kitu cha msingi ni kutokiuka mkataba ambao unaelekeza kwamba wanapovua samaki wanalazimika kuwauzia wale waliowakopesha na si tofauti na hivyo.
Mfanyabiashara mwingine aitwaye Geofrey Juma alisema kuwa licha ya hali hiyo pia bei ya samaki ni nzuri ukilinganisha na maeneo mengine hivyo wanashawishika kupeleka bidhaa hiyo nchini humo.
Aliongeza kuwa wanunuzi wa ndani hawana uwezo wa kununua tani nyingi za samaki na hata soko lililojengwa la kimataifa lililopo kijiji cha Kasanga halina ufanisi kwa kuwa linataka samaki wa kukausha ambao soko lake halina tija kwao.
Habari zinadai kuwa wafanyabiashara hao wamewekeza mjini Mpulungu nchini Zambia kwa kujenga viwanda vikubwa vya kuhifadhi samaki wabichi ambapo wamekuwa wakiwategemea wafanyabiashara wadogo kutoka nchini hususani wale wanaofanya shughuli za uvuvi kwenye Ziwa Tanganyika upande wa Mkoa wa Rukwa.
Kwa upande wake, afisa maendeleo ya jamii wa halmashauri ya wilaya ya Sumbawanga, Luckness Chiragwile alikiri wafanyabiashara hao kuvutiwa kuuza bidhaa hiyo nchini humo kutokana na ushawishi huo wa mikopo kutoka kwa wafanyabiashara hao wakubwa ambapo kwa mwaka zaidi ya tani 5200 huuzwa nchini humo.
Blogzamikoa
0 comments:
Post a Comment