Mussa Mwangoka, Sumbawanga-Rukwa yetu
TAHARUKI ilitanda katika Kambi ya Kampuni ya Ujenzi ya Kichina ya kijijini Matai Wilaya ya Kalambo Mkoani wa Rukwa baada ya mafundi na vibarua 50 walipovamia kambi hiyo na kuwafungia ndani “ matajiri wao” hao wa Kichina wakishinikiza kulipwa posho na mapunjo yao ya mishahara.
Vibarua hao wanafanya kazi za ujenzi katika Kampuni ya Kichina iitwayo China Railway Construction Ltd ambayo inajenga barabara kutoka Sumbawanga mjini kupitia kijijini Matai hadi Bandari ya Kasanga katika mwambao mwa Ziwa Tanganyika yenye urefu wa kilomita 112 kwa kiwango cha lami.
Kufuatia vurugu hiyo iliyodumu kwa zaidi ya saa nne iliwalazimu viongozi wa kampuni hiyo ya ujenzi kutoa taarifa Kituo cha Polisi cha mjini Matai ambao walilazimika kufika kambini hapo na kutuliza ghasia hiyo.
Tukio hilo lilitokea jana saa sita mchana pale vibarua hao wenye hasira wapatao 53 walipovamia kambi hiyo na kuwafungia ndani ‘mabosi’ wao wa Kichina huku wakiwapiga marufuku kwenda kujipatia chakula cha mchana.
Kwa mujibu wa taarifa hizo zilizothibitishwa na Msimamizi wa Kampuni hiyo Salim Juma zinaeleza kuwa ghasia hizo zinafuatia madai ya vibarua hao yanayotokana na kupunjwa posho zao ambapo wanadai kuwa wamekuwa wakilipwa tofauti na makataba wao wa kazi.
Kwa mujibu wa madai ya vibarua hao wamedai kuwa wamekuwa wakilipwa Sh 10,000- kwa siku badala ya Sh 12,000- kwa mafundi ilihali vibarua wakilipwa Sh 3,500- kwa siku badala ya Sh 5,000- ambapo waliaamua kufunga lango kuu la kambi hiyo na kuwazuia wachina hao kwenda kula chakula chao cha mchana hadi watakapowalipa posho na mapunjo yao .
Mkuu wa Polisi wa Wilaya ya Kalambo Hosea Setieli alithibitisha kutokea kwa tukio hilo ambapo aliongeza kuwa tayari askari polisi walikuwa wamepelekwa katika eneo la tukio ili kutuliza ghasia hizo na kuhakikisha usalama wa raia na mali zao .
Hata hivyo hakuwa tayari kueleza kwa kina mkasa huo kwa kuwa yeye alidai si msemaji wa Jeshi la Polisi .
Hata hivyo kwa kujibu wa Salim hakuna mtu yeyote aliyeumia wala uhalibifu wowote wa mali uliotokea kufuatia ghasia hizo ambapo aliongeza kusema kuwa Kampuni ilifikia makubaliano ya kuwalipa wafanyakazi hao leo asubuhi ili kunusuru ghasia zaidi zinazoweza kutokea na kuzorotesha utendaji wa kazi wa kampuni hiyo .
0 comments:
Post a Comment