Mussa Mwangoka, Sumbawanga. Rukwa yetu Blog
MAHAKAMA ya wilaya ya Sumbawanga imemuhukumu Nkinga Majeki (35) kutumikia kifungo cha miaka 30 jela baada ya kumtia hatiani kwa kosa la unyang’anyi wa kutumia silaha ya moto.
Hakimu wa Mahakama hiyo , Adamu Mwanjokolo akisoma hukumu hiyo mahakamani hapo juzi alisema kuwa mahakama amemtia hatiani Majeki ambaye ni mkazi wa kijiji cha Mheza wilayani Chunya mkoani Mbeya baada ya kuridhishwa na ushahidi wa upande wa mashtaka pasipo kutia shaka yeyote kuwa mshtakiwa alitenda kosa hilo .
Kwa mujibu wa hati za mashtaka zilizowasilishwa mahakamani hapo zinaonesha kuwa upande wa mashtaka ukiongozwa na Mkaguzi Msaidizi wa Polisi , Emanueli Shani uliwaleta mashahidi watano kutoa ushahidi katika shauri hilo.
“Hakika upande wa mashtaka umethibitisha pasipo kuacha shaka yeyote kuwa mshtakiwa alitenda kosa hilo hivyo natoa adhabu kali, ambapo nakuhukumu kutumikia kifungo cha miaka 30 jela adhabu ambayo itakuwa fundisho sio tu kwako mshtakiwa bali pia kwa wengine wote wenye tabia kama yako ambayo inarudisha nyuma maendeleo ya mtu binafsi na nchi kwa ujumla “alisema akitoa hukumu hiyo .
Awali, Upande a mashtaka ulidai mahakamani hapo kuwa mshtakiwa huyo alitenda kosa hilo Novemba 08 mwaka jana nyakati za usiku katika kijiji cha Kipeta wilayani Sumbawanga akiwa na mwenzake ambaye hajakamatwa walipovamia nyumbani kwa Ronald Lwenje (61) kijijini humo na kumnyang’anya fedha taslimu Sh 5,000,000- baada ya kumtishia kumpiga risasi kwa bunduki waliyokuwa nayo ambayo haijafahamika ni aina gani pia haijapatikana.
Kwa mujibu wa hati ya mashtaka inaonesha kuwa Lwenje alikuwa amepokea mafao yake siku chache kabla ya kuvamiwa baada ya kustaafu kazi ya ualimu .
Shani alidai mahakamani hapo kuwa mshatakiwa alikamatwa na polisi Novemba , 15 mwaka jana kijijini Klyamatundu wilayani Sumbawanga ambapo alikiri kutenda kosa hilo alipohojiwa pia aliweza kutambuliwa na mlalamikaji wa shauri hilo.
Mwisho
0 comments:
Post a Comment