Beda Mapengo (40), makazi wa kijiji cha Majomoto katika mkoa wa Katavi juzi akisaidiwa kutolewa kwenye basi la Mbeya Express T844 ARZ na wapiga debe na mawakala katika Kituo Kiuu cha mabasi mjini Sumbawanga mara baada ya kusafirishwa kutoka Mbeya hadi mjini hapa, baada ya kutelekezwa kituoni hapo na ndugu zake kutokana na kushindwa kumuhudumia katika Hospitali ya Rufaa mjini humo ambako alilazwa zaidi ya mwaka na nusu baada ya kuooza kiwili wili kufuatia ajali ya gari. Picha na Mussa Mwangoka.
Beda Mapengo (40),makazi wa kijiji cha Majomoto katika mkoa wa Katavi akiwa amelezwa katika Hospitali ya Mkoa wa Rukwa mjini Sumbawanga jana baada ya kutelekezwa na ndugu zake katika Stendi kuu ya mabasi mjini Mbeya baada ya kushindwa kumuhudumia katika Hospitali ya Rufaa mjini humo ambako alikolazwa zaidi ya mwaka na nusu baada ya kupooza kiwiliwili kufuatia ajali ya gari. Picha na Mussa Mwangoka.
******************
Mussa Mwangoka, Sumbawanga. Rukwa yetu
Mkazi mmoja wa kijiji cha Majimoto Wilayani Mlele, Mkoa wa Katavi, Beda Mapengo (40) amedai kutoroshwa hospitalini na ndugu zake kumtelekeza katika kituo cha mabasi cha Mbeya mjini kwa madai kuwa hawana uwezo wa kifedha wa kuendelea kumuuguza ugonjwa wake alioupata baada ya kugongwa na gari.
Akizungumza na mwandishi wa habari hizi jana katika hospitali ya Mkoa mjini Sumbawanga ambako amelazwa katika wodi namba tatu Mapengo alisema kuwa awali alilazwa kwa zaidi ya mwaka mmoja na nusu katika Hospitali ya Rufaa Mkoani Mbeya.
Hadi juzi alipochukuliwa na ndugu zake ambao hakuwa tayari kuwataja majina yao na kumtorosha hospitalini hapo kisha kumtelekeza bila msaada wowote katika Kituo Kikuu cha mabasi mjini Mbeya.
Mapengo ambaye ni baba mzazi wa watoto wanne aligongwa na gari wakati akitembea kwa miguu mwaka mmoja na nusu uliopita kijijini Majimoto na sasa hawezi kukaa wala kutembea kutokana na kiwiliwili na miguu yake kupooza.
“ Mie mwenyewe nimeshachoka kuendelea kuishi hospitalini sasa ninachohitaji ni kupewa msaada ili niweze kurejeshwa kijijini kwangu Majimoto kwani hata ndugu zangu hawana tena uwezo wa kunihudumia kifedha kwani wameniachia sh.10,00 za kujikimu” alisema
Kufuatia kadhia hiyo yakutelekezwa na ndugu zake hapo Kituo Kikuu cha mabasi mjini Mbeya , wapiga debe , mawakala wa mabasi wakiwemo na baadhi ya wafanyabiashara ndogo kituoni hapo waliguswa na kuhamasika na kufanya harambee katika jitihada kuhakikisha anasafirishwa hadi mjini Sumbawanga ambako angeweza kukutana na ndugu zake kutoka kijijini kwake Majimoto .
“ Sisi kwa umoja wetu tuliguswa sana hiyo tukatangaza harambee na kufanikiwa kukusanya Sh.256,000 ambapo tulitumia kiasi cha fedha hiyo kumnunulia godoro , shuka mpya na dishi kwa ajili ya kujisaidia haja ndogo” alisema Joseph Saibaba kiongozi wa wapiga debe na kuongeza:
“Tumemkatia tiketi ya viti vinne katika basi hili la Mbeya Express, unajua kwa siku nne tulikuwa naye hapa stendi tukimpatia huduma zote muhimu ikiwemo chakula na maji kiasi hiki cha Sh.190,000 kilichosalia tumemkabidhi yeye ili zimsaidie huko aendako”.
Mapengo alifanikiwa kusafirishwa na basi la Mbeya Express T 844 ARZ kutoka mjini Mbeya hadi Sumbawanga, baada ya wasamaria wema kumkatia tiketi za viti sita nyuma va gari hilo ambapo alilazwa katika viti hivyo.
Aidha kutokana ubovu wa barabara na gari hilo walilazimika kufika mjini hapa nyakati za saa 4 usiku ambapo baada ya kuwasili stendi kuu ya mabasi mjini Sumbawanga hakukuta ndugu yake yoyote aliyejitokeza kumlaki.
Mwenyekiti wa chama cha waandishi wa habari mkoa wa Rukwa, Peti Siyame alilazimika kuwasiliana na uongozi wa polisi Mkoa wa Rukwa ili uweze kutoa msaada kwa mtu huyo.
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Rukwa , Jacob Mwaruanda alifika mara moja kituoni hapo na kuamuru basi hilo alilosafiri nalo limfikishe hadi katika Hospitali ya Mkoa wa Rukwa mjini Sumbawanga ambapo alipokelewa na amelazwa kwa matibabu zaidi.
Hata hivyo, akizungumza hospitali hapo Mapengo anasisitiza kuwa anachotaka yeye ni kurudi nyumbani kwake majimoto umbali wa kilometa zaidi 180 kwa kuwa ugonjwa anaoumwa hawezi kupona na hana ndugu yoyote mjini Sumbawanga ambaye angeweza kumuhudumia sasa kulazwa hospitalini ni kuendelea kupata mateso.
0 comments:
Post a Comment