DC CHANG'A KUZIKWA IRINGA KESHO

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399. 

Waombolezaji katika msiba wa aliyekuwa Mkuu wa Wilaya ya Kalambo, Moshi Chang’a aliyefariki dunia juzi wakimpa pole mtoto wa marehemu, Chiku (katikati) nyumbani kwake, Mbagala-Kibonde Maji, Dar es Salaam.

Mkuu wa Wilaya ya Kalambo mkoani Rukwa, Moshi Chang’a aliyefariki dunia juzi atazikwa kesho Kihesa mkoani Iringa.
Chang’a alifariki juzi saa 10.15 jioni katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) alikokuwa amelazwa tangu Machi 29, mwaka huu kwa ugonjwa wa shinikizo la damu.
Mdogo wa marehemu, Faustine Kikove alisema jana kwamba mwili wa marehemu utasafirishwa leo saa 10.00 jioni kwa gari kwenda Iringa.
Alisema kabla ya kusafirishwa, mwili wa Chang’a utaagwa nyumbani kwake Mbagala Kibondemaji kuanzia saa 8.00 mchana na utazikwa kesho baada ya swala ya adhuhuri.
Akimzungumzia marehemu, alisema wakati akiwa Kalambo, alimpigia simu akimweleza kuwa hajisikii vizuri na kwamba alikuwa anakwenda Muhimbili kwa ajili ya kuchunguza afya yake.
“Hatukujua kwamba hali yake ingebadilika ghafla, tulijua anakwenda kuchunguzwa afya na angerejea salama kuendelea na majukumu ya kitaifa lakini haikuwa hivyo,” alisema .
Akizungumzia kifo hicho, Mkuu wa Mkoa wa Rukwa, Stella Manyanya alisema ni pigo kwa Wanakalambo na mkoa mzima kwa jumla.
“Tumepoteza kiongozi ambaye alikuwa mwongoza njia ambaye wananchi aliowaongoza walimpenda kwa ucheshi wake na uchapakazi,” alisema.
Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, Jordan Rugimbana alisema katika vikao vya wakuu wa wilaya, Chang’a alikuwa mwalimu kutokana na uzoefu wake wa kutumikia nyadhifa mbalimbali za Serikali.
“Alitufundisha mambo mengi kutokana na uzoefu wake, pia kwa sababu ni mwalimu kitaaluma na kiongozi wa muda mrefu CCM,” alisema Rugimbana.
Nyumbani kwa marehemu viongozi walifika kutoa pole kwa wafiwa, wakiwamo Manyanya na Rugimbana ni Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Saidi Meck Sadiki, Mkuu wa Wilaya ya Temeke, Sophia Mjema na Mkuu wa Wilaya ya Bahi, Betty Mkwasa.
Chanzo;Mwananchi

TAARIFA RASMI YA MSIBA WA ALIYEKUWA MKUU WA WILAYA YA KALAMBO MH.MOSHI MUSSA CHANG'A

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
 IMG_3959

Kifo cha DC: Rais Kikwete amtumia salamu Waziri Mkuu

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399. 

IMG_3959
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete amemtumia salamu za rambirambi Waziri Mkuu Mheshimiwa Mizengo Peter Pinda kuomboleza kifo cha Mkuu wa Wilaya ya Kalambo, Mkoa wa Rukwa, Ndugu Moshi Chang’a(pichani).
“Ni kifo cha kusikitisha kwa sababu kimepunguza safu ya uongozi wetu na kimelinyang’anya taifa letu mhamasishaji hodari na mtetezi wa kuaminika wa maendeleo ya wananchi,” Rais Kikwete amesema katika salamu hizo.
Amesema Rais Kikwete katika salamu zake za rambirambi: “Nilimjua Ndugu Chang’a kwa miaka mingi tokea mwaka 1979 alipojiunga na utumishi wa Chama cha Mapinduzi ambacho pia alikitumia kwa uaminifu mkubwa hadi alipoteuliwa kuwa Mkuu wa Wilaya mwaka 2003. Alikuwa kiongozi wa kweli kweli wa maendeleo na kifo chake kimetuachia pengo la uongozi.”
“Nakutumia salamu zangu za dhati kuomboleza msiba huu. Aidha, kupitia kwako, naitumia familia wa Ndugu Chang’a pole za dhati ya moyo wangu kwa kuondokewa na mzazi na mhimili wa familia. Nakuomba uwajulishe kuwa naelewa machungu yao katika kipindi hiki na nawaombea subira na uvumilivu kwa sababu yote ni mapenzi ya Mungu. Aidha, naungana nao katika kumwomba Mwenyezi Mungu, Mwingi wa Rehema, aiweke peponi roho ya marehemu. Amen,” amesema Rais katika salamu hizo.
Ndugu Moshi Chang’a ambaye aliaga dunia jioni ya, Jumapili, Aprili 20, 2014  katika Hospitali ya Taifa, Muhimbili, Dar Es Salaam amekuwa mkuu wa wilaya katika Mikoa ya Mbeya, Tabora na Rukwa.

MKUU WA WILAYA YA KALAMBO, MOSHI CHAN'GA AFARIKI DUNIA

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399. 
Mkuu wa Wilaya ya Kalambo, mkoani Rukwa, Moshi Chang’a enzi za uhai wake akifafanua jambo

Mkuu wa Wilaya ya Kalambo, mkoani Rukwa, Moshi Chang’a amefariki dunia. Kiongozi huyo alifariki dunia jana saa 10: 15 jioni katika Hospitali ya Taifa Muhimbili, alikokuwa amelazwa kwa zaidi ya siku 20.
Ofisa Habari wa hospitali hiyo, Aminieli Aligaesha alisema DC Chang’a alifika hospitalini hapo Machi 29, mwaka huu akiwa anaumwa na kulazwa.
Alisema madaktari wamekuwa wakimpatia matibabu, lakini ilipofika jana saa 9:30 alasiri hali yake ilibadilika ghafla.
“Walijitahidi kuokoa uhai wake bila mafanikio na ilipofika saa 10: 15 alikata roho, alisema Aligaesha huku akikataa kueleza tatizo lililokuwa linamsibu.
“Huyu ni kiongozi wa Serikali, bila shaka wakubwa huko serikalini wataeleza zaidi kuhusu kifo hicho,” alisema.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Tamisemi), Hawa Ghasia alithibitisha kutokea kwa kifo hicho mchana wa jana, baada ya kiongozi huyo kusumbuliwa na ugonjwa wa shinikizo la damu.
Alisema amemwagiza katibu wake (wa waziri) na Mkuu wa Mkoa wa Rukwa, Stella Manyanya kufuatilia na kushughulikia msiba huo na taarifa zaidi kuhusu utaratibu zitapatikana leo baada ya kuzungumza na familia.
Chang’a kabla ya kuhamishiwa katika Wilaya ya Kalambo alikuwa DC wa Wilaya Mpya ya Mkalama.
Chanzo;Mwananchi

MAGAZETI YA LEO JUMATATU APRIL 21, 2014

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.JELA KWA KUSHINDWA KUBAKI NJIA KUU

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.

MWALIMU wa Shule ya Msingi Misunkumilo, Kata ya Namanyere, wilayani Nkasi, mkoani Rukwa, Oswald Kapota (33) amehukumiwa kwenda jela miezi sita kwa kosa la kutelekeza familia yake na kwenda kuishi kwa kimada.
Mwalimu huyo ambaye ameshindwa kubaki njia kuu na kuendeleza michepuko, amepata hukumu hiyo jana baada ya Mahakama ya Mwanzo Namanyere, kumtia hatiani.
Akitoa hukumu hiyo, Hakimu wa Mahakama ya Mwanzo Namanyere, Baraka Stanley, alisema kuwa mahakama hiyo imeridhika na ushahidi uliotolewa na upande wa mashitaka ambao unaonyesha kuwa Mwalimu huyo alifanya kitendo hicho kwa kukusudia.
Mwalimu huyo alidaiwa kuitelekeza familia yake ya watoto wawili na mke, kisha kuhamia nyumbani kwa  mwanamke mwingine na kuifanya familia hiyo kuishi katika mazingira magumu kwa kipindi cha zaidi ya miezi sita, hali iliyomlazimu mkewe kufungua kesi polisi ya kudai huduma ya malezi ya familia hiyo.
 Licha ya hukumu hiyo mahakama imeamuru mwalimu huyo atakapomaliza adhabu yake ya kifungo jela atalazimika kuitunza familia yake kama wajibu unanavyomtaka kama mzazi.
Awali upande wa mashitaka uliieleza mahakama hiyo kuwa mwalimu huyo alimtelekeza  mke wake, Lucy Malambugi, ambaye amezaa naye watoto wawili kiasi cha kuifanya iishi maisha magumu huku mkewe akihangaika kuomba omba ilhali yeye akiponda raha na nyumba ndogo.
Kabla ya kutolewa kwa hukumu hiyo, mshitakiwa alitakiwa kujitetea ambapo alikataa kutoa utetezi wake kwa madai kuwa hawezi kujitetea mbele ya mwanamke huyo, akimtuhumu kuwa  si mwaminifu kwenye ndoa na ndiyo chanzo cha yeye kuamua kuhamia kwa nyumba ndogo.
Kutokana na kosa hilo, mahakama imemtia hatiani mtuhumiwa huyo chini ya kifungu cha sheria namba 167, sura ya 16, ambayo imefanyiwa marekebisho mwaka 2002.
Chanzo:Tanzania Daima

MKUU WA MKOA WA RUKWA ASHIRIKI NA UVCCM KATIKA MBIO ZA UZALENDO TANZANIA KUADHIMISHA MIAKA 50 YA MUUNGANO WA TANZANIA

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399. 

Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Injinia Stella Manyanya akipokea msafara wa pikipiki wa vijana wa CCM (UVCCM) ambao wanaendesha mbio za Uzalendo Tanzania zikiwa na lengo la kuadhimisha Miaka 50 ya Uhuru wa Tanzania Bara na Tanzania Zanzibar jana tarehe 07-04-2014. Mbio hizo za kitaifa zinahusisha msafara wa pikipiki tano zinazoongozwa na viongozi watatu wa UVCCM ambao wanakuwa kwenye gari, aidha zinashirikisha wadau mbalimbali wa UVCCM katika kuzifanikisha. Mbio hizo  zinahimiza vijana kudumisha muungano, kuweka utaifa mbele na kutumia fursa zilizopo kwa maendeleo yao. Mbio hizo zitakuwa Mkoani Rukwa tarehe 07 na 08 April 2014 na kuelekea Mkoani Mbeya. 
Ujumbe wa mbio hizo za Uzalendo Tanzania ambazo zinaendeshwa na UVCCM.
Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Injinia Stella Manyanya (kati) akiendesha duwa rasmi ya kuwaombea viongozi waasisi wa Muungano ambao wametangulia mbele za haki kama wanavyonekana kwenye picha Hayati Mwalim Julius K. Nyerere na Hayati Abeid Amani Karume muda mfupi baada ya kupokea msafara wa mbio hizi ofisini kwake jana tarehe 07-04-2014.
Msafara wa Mbio za Uzalendo Tanzania ukiondoka katika Ofisi ya Mkuu ya Mkoa wa Rukwa mara baada ya kupata baraka za kiongozi huyo na kusaini kitabu tayari kwa zoezi la mbio hizo katika Manispaa ya Sumbawanga na baadae kuelekea katika Mji Mdogo wa Laela.
Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Injinia Stella Manyanya akiondoka na pikipiki iliyokuwa ikiendeshwa na Katibu wa UVCCM Mkoa wa Rukwa Ndugu Philipo Elieza ambapo alishiriki mbio hizo hadi kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika nje ya uwanja wa Nelson Mandela katikati ya Manispaa ya Sumbawanga.
Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Injinia Stella Manyanya akiongoza mbio hizo na vijana wa UVCCM kuelekea kwenye mkutano wa hadhara.
Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Injinia Stella Manyanya (Mb) akizungumza katika Mkutano wa hadhara ambapo alisema tunu ya muungano ni lazma ilindwe na kila moja wetu na kuwa sio jambo la hiari. Aliongeza kuwa madai ya uwepo wa Serikali tatu ni hatua za kuhatarisha Muungano uliopo wa Tanzania Bara na Tanzania Zanzibar hivyo hakuna budi kuimarisha Muungano wa Serikali mbili kwa maslahi watanzania wote. Aliuotelea mfano muungano wa Serikali tatu kuwa hauna tofauti na kuchukua kisu na kugawana mtoto ambapo kila mzazi atachukua kipande ambacho sio mtoto kamili.
Mkuu wa Mkoa wa Rukwa akizungumza kwenye mkutano wa hadhara.
Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Injinia Stella Manyanya akimkabidhi Katibu wa UVCCM Mkoa wa Rukwa Ndugu Philipo Elieza cheti cha pongezi kwa ushiriki wa Mbio za Uzalendo Tanzania na kingine kwa UVCCM Mkoa na Taifa kwa kuandaa na kufanikisha mbio hizo. Mkuu huyo wa Mkoa aliandaa vyeti vya pongezi kwa washiriki wote wa mbio hizo.
Mwenyekiti wa UVCCM Mkoa wa Rukwa Ndugu Agustino Mzurikwao akitoa salam za vijana wa CCM katika mkutano huo wa hadhara ambapo alisisitiza juu ya vijana kutumia fursa zilizopo katika kujiendeleza kiuchumi na kudumisha Muungano wa Tanzania Bara na Tanzania Zanzibar. Kulia ni Katibu Muenezi wa CCM Mkoa wa Rukwa Ndugu Clemence Bakuli.
(Na Hamza Temba - Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Rukwa

CCM:TUTAREJESHA MAJIMBO YOTE YA UPINZANI

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.

CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) kimesema hivi sasa kipo makini kuhakikisha kinaweka udhibiti wa kutosha wa makundi majimboni. Pia chama hicho, kimesisitiza kuwa, kutokana na kukithiri kwa makundi hayo, viongozi wake wa kitaifa wamekuwa hawalali kwa kuangalia namna ya kurejesha majimbo yote ya wapinzani mikononi mwa chama hicho.
Hayo yalisema mwishoni mwa wiki na Katibu Mkuu wa CCM, Abdulrahman Kinana, alipozungumza kwa nyakati tofauti na wajumbe wa Halmashauri Kuu za Wilaya ya Nkasi, Kalambo na Sumbawanga ambako amehitimisha ziara yake ya kukagua Ilani na kuimarisha chama hicho, mkoani Rukwa.
Akizungumza na wajumbe wa halmashauri hizo, Kinana aliweka msisitizo na kuwataka wana CCM nchini kote kuhakikisha wanakuwa kitu kimoja na kuepuka makundi ya uchaguzi.
Alisema umoja ndio ushindi na iwapo kila mwanachama wa chama hicho, atalitambua hilo na kulitekeleza kwa vitendo, chama hicho katika uchaguzi ujao, kitakuwa salama na kuibuka na ushindi wa kishindo.
"Kutokana na hali hii, Kamati Kuu na NEC ipo macho kuhakikisha tunarejesha majimbo yote yaliyokuwa katika mikono ya wapinzani, na nikiwa kama mtendaji wa chama ninazo taarifa za kuanza kwa vurugu hasa katika majimbo yanaongozwa na wapinzani," alisema Kinana.
Alisema iwapo wanachama wa chama hicho watashindwa kushikamana na hata kuwa na mipango ni wazi kuwa chama hicho kitashindwa kuyarejesha majimbo hayo.
"Hili siko tayari kuliona na kila mwana CCM atambue hivyo." Kinana alisema kutokana na hali hiyo, wananchi wengi walikata tamaa na kutafuta njia mbadala na kuunga mkono upinzani.
"Najua wengi walichagua upinzani kutokana na kukata tamaa, hili tulibadilishe, tuwajibike."
Chanzo;Habari Leo

Madiwani Kalambo waridhia uanzishwaji CHF

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399. 
BARAZA la Madiwani la Halmashauri ya Wilaya ya Kalambo, mkoani Rukwa, limeridhia kupitisha sheria itakayoruhusu kuanzishwa kwa Mfuko wa Afya ya Jamii (CHF).
Wakipitisha sheria hiyo ndogo, wajumbe wa baraza hilo walisema walikuwa wakisubiri kwa hamu kupelekwa kwa mswada huo ambao utawasaidia wapiga kura wao kuondokana na adha ya kupata matibabu pindi wanapougua na hawana hela za matibabu.
Diwani wa Kisumba, Paul Kasitu, alisema kutokana na kupitishwa sheria hiyo, wananchi wa Kalambo watakuwa na uhakika wa kutibiwa hata kama hawana hela.
Alisema wakazi hao wamekuwa wakipata shida pindi wanapougua, na hasa ikizingatiwa wananchi wengi hawana utaratibu wa kuweka akiba ya hela katika taasisi za kifedha.
Diwani wa Viti Maalumu, Crisensia Nyembela, alisema kuanzishwa kwa mfuko huo kutasaidia wajawazito na watoto ambao ndio wanakuwa waathirika wakubwa, kwani ni kundi ambalo linahitaji huduma za afya kwa umakini wa hali ya juu.
Chanzo:Mwananchi

ZIARA YA KATIBU MKUU WA CCM,NDUGU KINANA YAKUMBANA NA CHANGAMOTO ZA BARABARA WILAYANI NKASI MKOANI RUKWA

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
 Katibu Mkuu wa CCM,Ndugu Abdulrahman Kinana akimueleza jambo Mbunge wa jimbo la Nkasi Kaskazini,Mh.Ali Mohammed Kessy,walipokuwa wakitembea kwa miguu kufuatia msafara huo kukumbana na changamoto ya barabara mapema jana jioni katikati ya Msitu wa hifadhi ya wilaya ya Nkasi.Ndugu Kinana na Msafara wake ulikuwa umetoka kijiji cha Namanyere kuelekea kijiji cha Mwampemba kusikiliza matatizo ya Wananchi na kukagua miradi mbalimbali ya maendeleo iliyopangwa kutekelezwa kwenye Ilani ya uchaguzi ya mwaka 2010.

Barabara hiyo yenye urefu wa kilometa 100,lakini iliwachukua zaidi ya masaa 12 kwenda na kurudi kutokana na ubovu wa barabara.Ndugu Kinana yuko Mkoani Rukwa,Katavi na Kigoma kwa ziara ya siku 21 ya kuimarisha Chama cha CCM,kukagua miradi mbalimbali ya maendeleo kiwemo na kuzisikiliza kero mbalimbali za wananchi
 Ndugu Kinana akishiriki kuweka mawe sehemu korofi,angalau kusaidia Lori hilo pichani lililolala ndani ya msitu huo kwa siku mbili,wapite nae msafara wake uweze kuendelea na safari.
 Sehemu korofi ya Barabara ikiwekwa sawa ili lori lipite na kisha msafara nao uweze kupita,lakini hata hivyo zilitumika juhudi kubwa kuvusha msafara wa Kinana na hatimae kuendelea na safari ya kuelekea kijiji kingine.
 Ndugu Kinana akizungumza na baadhi ya Wanahabari aliokuwa ameambatana nao kwenye msafara wake,baada ya magari kunasa kutokana tatizo la barabara
 Wanahabari waliokuwa kwenye msafara wa Katibu Mkuu wa CCM,Ndugu Kinana wakiwa hoi kabisa,wakisubiri kudra za Mwenyezi Mungu,msafara wa magari yao yanasuliwe na kuendelea na safari.Picha hii imepigwa na Katibu Mkuu,Ndugu Kinana.
 Hali ilikuwa tete mnoo,kipande cha kilometa mia kinapitika kwa zaidi ya masaa sita,kutoka kijiji kimoja kwenda kingine.
 Ilikuwa ni shughuli nzito katika msafara wa Ndugu Kinana,barabara ni mbovu kupita maelezo
 Kila mmoja akipumua kivyake,baada ya kuvuka salama sehemu korofi ya barabara.
 Katibu Mkuu wa CCM,Ndugu Kinana (alinaerusha jiwe) akishiriki kuziba sehemu korofi kwa mawe,ili msafara uweze kupita
 Pichani kulia ni Katibu Mkuu wa CCM,Ndug Kinana akiongoza kuvuka sehemu korofi ya barabara kwa miguu,huku madera wakipiga hesabu zao namna ya kupita.
Mchuma ukipita sehemu korofi ya barabara kwa mbinde.PICHA NA MICHUZIJR-MICHUZI MEDIA GROUP-NKASI RUKWA.
SIKILIZA TONE RADIO HAPA

Sikiliza Tone Radio Live Hapa, na Tembelea Website yetu www.toneradiotz.com
 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Rukwa Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa