Imeandikwa na Peti Siyame, Tanganyika
MWALIMU wa dini wa Kanisa Katoliki Jimbo la Mpanda, Noel Sitemele
amefariki dunia muda mfupi baada ya kumaliza kuongoza ibada ya mazishi
ya muumini wake yaliyofanyika katika makaburi ya Mchakamchaka Kijiji cha
Majalila wilayani Tanganyika mkoani Katavi.
Katekista huyo alikuwa akitoa huduma ya kiroho katika Kigango cha
Mchakamchaka kilichopo katika Parokia ya Mpanda Ndogo katika Wilaya ya
Tanganyika mkoani Katavi. Akizungumzia mkasa huyo, Diwani wa Kata ya
Mpanda Ndogo, Hamad Mapengo alisema licha ya Sitemele kuwa mwalimu wa
dini, katika uhai wake alikuwa pia Mwenyekiti wa Kijiji cha Majalila
kilichopo katika Halmashauri ya Mpanda wilayani Tanganyika.
Mapengo ambaye pia ni Mwenyekiti wa Halmashauri ya Mpanda, alisema
Katekista alifariki dunia juzi saa 11 jioni muda mfupi baada ya
kufikishwa zahati ya kijijini Majalila kutibiwa.Alisema kabla ya kukutwa
na umauti, Katekista huyo alikuwa mwenye siha njema na aliongoza ibada
ya mazishi ya muumini wake hadi mwisho katika makaburi ya Kigango cha
Mchakamchaka kilichopo katika Kijiji cha Majalila ambapo alianza
kujisikia vibaya.
“Baada ya kumaliza ibada hiyo ya mazishi, alianza kujisikia vibaya
hivyo akalazimika kurejea nyumbani kwake na kuwaacha waombolezaji
makaburini,” alieleza Mpaengo. Alisema, baada kufika nyumbani kwake,
hali yake iliendelea kuwa mbaya na aliomba msaada kutoka kwa majirani
zake wamkimbize kwenye kituo cha afya kwa matibabu.
Inaelezwa zahanati hiyo haiko mbali kutoka alikokuwa akiishi mwalimu
huyo wa dini. Mwenyekiti alisema, taarifa za kifo cha Katekista huyo
zilizagaa haraka kijijini humo na kuwafikia waombolezaji waliokuwa
nyumbani kwa marehemu aliyeongozewa ibada ya mazishi na Katekista huyo
waliopata simanzi kubwa wengine wakiwa hawaamini jambo hilo.
Maziko yake yalifanyika jana makaburi ya kigango cha Mchakamchaka
Kijiji cha Majalila. Padri Paschal Kipenye wa Parokia ya Mpanda Ndogo
aliongoza ibada ya mazishi yaliyohudhuriwa na mamia ya waombolezaji
akiwemo Mbunge wa Mpanda Vijijini, Selemani Kakoso.
CHANZO HABARI LEO
0 comments:
Post a Comment