Imeandikwa na Pety Siyame, Sumbawanga
MAHAKAMA Kuu ya Tanzania Kanda ya Sumbawanga imewahukumu wakazi
wawili wa Kijiji cha Kaengesa wilayani Sumbawanga, kifo kwa kunyongwa
baada ya kutiwa hatiani kwa kumuua Magreth Lazaro kwa kukusudia baada ya
kumbaka kwa zamu.
Washitakiwa hao wawili ni Maurus Simwanza na Edward Chikwema maarufu
Jeshi. Walitiwa hatiani kwa kumvamia na kumbaka Magreth kisha
wakamshindilia kwa nguvu kitu chenye ncha kali ukeni hadi utumbo wake
ukatoka nje na kumsababishia umauti.
Akisoma hukumu hiyo, Jaji wa mahakama hiyo, Dk Adam Mambi alisema
wawili hao walitenda kosa hilo kinyume cha Kifungu 199 cha Sheria ya
Makosa ya Jinai Sura ya 16, kama ilivyofanyiwa marekebisho 2002.
Alieleza mahakamani hapo marehemu kabla ya kukata roho akiwa
anapatiwa matibabu katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Rukwa, aliwataja
washtakiwa hao wawili kwa majina kuwa ndio waliomshambulia na kumuumiza
vibaya.
Katika shauri hilo, upande wa mashtaka uliita mashahidi wanne ili
kuthibitisha ushahidi wao dhidi ya makosa hayo yaliyokuwa yakiwakabili
washtakiwa hao. Awali, Mwendesha Mashtaka , Njoloyota Mwasubira
akisaidiana na Safi Kashinde, alidai mahakamani hapo kuwa washtakiwa hao
kwa pamoja walitenda uhalifu huo Juni 10 , 2012 saa nne usiku kijiji
Kaengesa.
Ilidaiwa kuwa usiku huo wa tukio wawili hao walimvamia binti huyo,
aliyekuwa akinywa pombe ya kienyeji katika klabu moja iliyokuwa ikiuza
kilevi hicho kijijini humo, ambapo baada ya kutoka nje na kumbaka kwa
zamu, walimuingizia kitu chenye ncha kali kwenye sehemu zake za siri
hadi utumbo ukatoka nje.
Kwa mujibu wa Njoloyota, mtu huyo kwanza alikimbizwa katika Kituo cha
Afya cha Kaengesa kwa matibabu, lakini baadae alipelekwa katika
Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Rukwa mjini hapa ambapo alikufa akiwa
anapatiwa matibabu.
Upande wa utetezi uliongozwa na Wakili wa Kujitegemea, Peter
Kamyalile. Wakati huo huo, mahakama hiyo imemhukumu kifo mkazi wa Kijiji
cha Singiwe wilayani Kalambo, Augustino Nandi kwa kunyongwa baada ya
kupatikana na hatia ya kumuua kwa makusudi binti yake, Oliveta Nandi
(12) kwa wivu wa kimapenzi.
CHANZO HABARI LEO
0 comments:
Post a Comment