Home » » KAMA HUKITAKI, KUNA WANAOKITAKA

KAMA HUKITAKI, KUNA WANAOKITAKA

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.


“CHAKO ni chako, cha mwenzio si chako.” Kitu unachokiita chako ni kizuri na huweza kukufaa na una uhuru nacho kuliko cha mtu mwingine. Methali hii yatufunza kuvithamini na kuvitegemea vitu vyetu wala si vya watu wengine.

Umaarufu wa lugha ya Kiswahili umezifanya baadhi ya nchi mbalimbali duniani kuomba walimu kutoka Tanzania ili wananchi wao wafundishwe Kiswahili. Nchi za hivi karibuni kuomba walimu wetu ni Rwanda na Sudan.
Ingawa ni jambo la kujivunia kuwa Kiswahili kinakuwa cha kimataifa, sisi twang’ang’ania Kiingereza wakati lugha yetu yatushinda kuitumia itakiwavyo!
“Watake wasitake … Hiki ni kikosi cha karne Simba SC. Kikosi cha Simba cha msimu ujao kinaweza kuwa cha karne iwapo Wekundu wa Msimbazi hao watafanikiwa kumalizana na nyota kadhaa wanaodaiwa kusainishwa mikataba na timu hiyo.”
‘Karne’ ni kipindi cha miaka mia moja. Hakuna timu yoyote ya Tanzania yenye umri huo. Yanga ilianzishwa mwaka 1935 na Simba mwaka 1936. Aidha sentensi ya mwandishi haikuandikwa kwa mtiririko mzuri.
“Watake wasitake …” Wanaoambiwa hivyo ni watu gani? Ni wasomaji, au mwandishi anakiuka maadili na kuwa shabiki wa Simba ili kuwakejeli (maneno ya kukebehi; utani) mashabiki wa Yanga?
“…Wekundu hao wa Msimbazi watafanikiwa …” Neno ‘hao’ halina umuhimu ingawa hutumiwa sana na waandishi kwa sababu wanazozijua wenyewe. Kadhalika maneno “Watake wasitake”nisingeyatumia kwani ni kuwalazimisha hao wanaosemwa na mwandishi.
Ingeandikwa: “Iwapo Simba itafanikiwa kuwasajili wachezaji mahiri wanaotakiwa na klabu hiyo, hapana shaka itakuwa timu bora ya msimu.”
Mwandishi kajitambulisha anaowalenga aliporudia kulazimisha kwamba: “Wapinzani wa Simba watake wasitake, kikosi cha Msimbazi msimu ujao kitakuwa ni balaa na huenda kikavifunika vyote vilivyopita kwa miaka ya hivi karibuni, lakini tu iwapo Kocha Mkuu wa Simba, Joseph Omog, atatuliza akili yake na kuwatumia ipasavyo wachezaji hao.”
Sentensi ya mwandishi ina maneno 40 yasiyo na umuhimu. Ingeandikwa: “Huenda msimu ujao Simba ikaweka rekodi ya kuwa na kikosi bora zaidi ya misimu iliyopita endapo kocha Omog atawatumia wachezaji hao ipasavyo.”
Sielewi ni kwa nini waandishi wetu hutumia ‘balaa’ kwa lengo la kusifu tofauti kabisa na maudhui (wazo linaloelezwa katika maandishi) yake. Kwa ufasaha wa lugha, neno ‘balaa’ au ‘baa’ ni janga lililoenea katika jamii au kwa mtu binafsi.
Ajabu! Wakati Tanzania yasifiwa kwa lugha ya Kiswahili, baadhi ya waandishi wanajibidiisha kukichafua. Ukurasa wa mbele wa gazeti hilo ulikuwa na kichwa kilichoandikwa kwa herufi kubwa nyeusi ti (neno la kushadidia kukoza kwa weusi; nyeusi sana)
“YANGA YANASA KIBERENGE KIPYA.”
Tuone maana ya ‘kiberenge.’ (i) garimoshi dogo la kukagua reli kabla ya treni kupita; gari moshi dogo linalotumiwa katika mashamba ya mkonge; toroli. (ii) mwanamke malaya; kibiritingoma, kahaba.
Anayeitwa ‘kiberenge’ si mwanamke bali ni mwanamume, mcheza kandanda Issa Yahya aliyesajiliwa na Yanga kuziba nafasi ya Msuva. Issa Yahya ametajwa mara tatu kuwa ‘kiberenge!’ Si vizuri kuwapa binadamu wenzetu majina ya kuwadhalilisha.
Gazeti hilohilo lilikuwa na habari iliyopewa kichwa: “Eeh Mchungaji Msigwa kumbe Simba!” Kilichomshangaza mwandishi Mchungaji Msigwa kuwa shabiki au mwanachama wa Simba ni nini?
Kama hiyo haitoshi, soma lugha iliyofuatia kichwa hicho. “Mbunge wa Iringa Mjini, Mchungaji Peter Msigwa, kumbe Simba buana.” Neno la mwisho (buana) latumiwa mara kwa mara na waandishi wa habari za michezo. Wakati mwingine huandika ‘bhana’ eti kwa maana ya ‘bwana!’
“Msigwa aliwataka wachezaji waliotua Msimbazi kutuliza akili ili kuiletea mafanikio chama lao ambalo lina misimu mitano mfululizo halijatwaa taji la ligi.”
“Chama lao ambalo …” ni lugha gani? Uandishi wa ‘chama lao’ umeenea sana siku hizi. Ndio ukuaji wa lugha? Hapana ni uchafuzi na upotoshaji.
“Salaam! Hao walengwa wanautazama ukurasa huu? Kama wanautazama kwa nini hawabadiliki? Hiyo ‘no’ ni saratani katika lugha ya Kiswahili.
“Rupia ni sarafu ya India mpaka sasa na ilitumika Zanzibar wakati wa ukoloni. Thamani yake ilikuwa shilingi nne za Afrika Mashariki. Ndio shilingi ikaitwa ‘roboo’ (robo rupia) senti 50 ikaitwa thumni. Wa Dar es Salaam wakaiita nusu shilingi.
“Tatizo ni waandishi wetu kuwa na mamlaka ya kila kitu: lugha, siasa, uchumi, utawala n.k. Yote hayo si kwa kuyasomea bali kwa kuwa mwandishi na kupewa ukurasa na gazeti. Si mchumi, azungumzia uchumi. Si mwanasheria azungumzia mahakama.
“Kwenye michezo usiseme. Huko ndio wakipitia kwenye mitandao huja na lugha za ajabu ajabu. Mwandishi mmoja aliandika: ‘Dr. Williamson, alianzisha sailing club ya kwanza Mwadui.’ Akatolea ufafanuzi ‘sailing club’ kuwa ni ‘club inayoelea!’ Mambo ni kama hayo. Hao ni wale wajionao ‘walijualo hakuna alijuaye.’”
Huu ni ujumbe wa msomaji ambaye hataki ajulikane nami natii maagizo yake.
Methali: Usiache mbachao kwa msala upitao.
[email protected]
0715/0784 33 40 96
Jika Anda menyukai Artikel di blog ini, Silahkan klik disini untuk berlangganan gratis via email, dengan begitu Anda akan mendapat kiriman artikel setiap ada artikel yang terbit di Creating Website

0 comments:

Post a Comment

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Rukwa Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa