WAZIRI wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Profesa Makame Mbawara
ameagiza ujenzi wa barabara ya Sumbawanga –Matai hadi Bandari ndogo ya
Kasanga wilayani Kalambo mkoani Rukwa, inayojengwa kwa kiwango cha lami,
uwe umekamilika ifikapo Julai mwakani.
Amesema hakuna sababu ya ujenzi wa barabara hiyo ya urefu wa kilometa
112 unaogharimu zaidi ya Sh bilioni 133.2 kuendelea kusuasua wakati
fedha zipo.
Alimwagiza mkandarasi anayejenga barabara hiyo kwa kiwango cha lami
kukamilisha ujenzi wa mizani, nyumba za watumishi watakaofanya kazi
kwenye mizani hiyo na ujenzi wa daraja kufikia Desemba mwaka huu.
Alitoa maagizo hayo baada ya kutembelea na kukagua ujenzi wa barabara
hiyo unaotekelezwa na mkandarasi wa Kampuni ya China Railway 15, Bereau
Group Corporation (CR15G) na Henan Provincial Newcentry Road na Bridge
Consultants Limited JV.
Katika hatua nyingine, Mbarawa alisema Serikali imetenga zaidi ya Sh
bilioni 11.6 kwa ajili ya ujenzi wa barabara inayounganisha miji ya
Matai na Kasesya wilayani Kalambo mkoani Rukwa kwa mwaka wa fedha
2016/17. Alisema mchakato wa kumpata mkandarasi wa kujenga kipande hicho
cha barabara chenye urefu wa kilometa 50 unaendelea.
Alisisitiza kuwa kukamilika kwa ujenzi huo kunafungua na kukuza wigo wa biashara kati ya mkoa wa Rukwa na nchi jirani ya Zambia.
“Pia itapunguza kwa kiasi kikubwa mlundikano wa magari makubwa katika
Mji mdogo wa Tuduma yanayosafiri kati ya Tanzania na nchi jirani za
Kongo DRC na Zambia,” alieleza Profesa Mbawara.
Kwa upande wake, Meneja wa Wakala wa Barabara (Tanrods) mkoani Rukwa,
Masuka Mkina alisema kazi za usanifu wa kina wa mradi huo zinafanywa na
Mhandisi Mshauri , M/s Inter Consult Limited na G –PES Limited kwa
gharama ya Sh milioni 400 na usanifu ulianza Januari Mosi, 2014 na
kukamilika Januari 31, 2015.
HABARI LEO
HABARI LEO
0 comments:
Post a Comment