SERIKALI imesema imeamua kuwekeza kwenye mikoa ya pembezoni
kuhakikisha usikivu wa Shirika la Utangazaji la Taifa (TBC) unakuwa
mkubwa na wa kutosha kwa maeneo yote nchini.
Rai hiyo ilitolewa na Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo,
Nape Nnauye alipofanya ziara jana katika Mkoa wa Rukwa na kukagua
mitambo ya kurushia matangazo ya shirika hilo pamoja na kukutana na
wadau wa sekta anazozisimamia.
“Mkoa wa Rukwa ni kati ya mikoa ya pembezoni ambayo usikivu wa
Shirika la Utangazaji la Taifa ni mdogo hivyo kufanya mikoa hii
kusikiliza matangazo ya redio kutoka nchi jirani badala ya kusikiliza
taarifa za nchi yetu,” alisema Nape.
Alisema lengo la serikali ni kuwa na vyombo vyenye nguvu ya kusikika
mikoa ya pembezoni na ikiwezekana vivuke mipaka na kusikika katika mikoa
ya jirani, badala ya wananchi kusikiliza matangazo kutoka vyombo vya
nje.
Ili kutimiza lengo hilo, Nape aliahidi kufanya maamuzi magumu kwa
kusimamia ubadilishaji wa baadhi ya vifaa, kuhamishia mitambo maeneo ya
milimani pamoja na kuweka busta zenye nguvu zitakazoweza kufikisha
matangazo ya redio (TBC Taifa) na Televisheni ya taifa (TBC 1) nchi
nzima.
Akitoa taarifa kuhusu usikivu wa TBC, mkoa wa Rukwa, Kaimu Mkuu wa
Kanda TBC, Nyanda za Juu Kusini, Hosea Cheyo, alisema usikivu wa shirika
hilo upo kwa asilimia 75, hivyo kuiomba serikali kuhamisha mtambo wa
shirika hilo katika mlima wa King’ombe ili wananchi wa mkoa huo wapate
fursa ya kusikiliza redio ya taifa.
Naye Meneja wa TCRA Kanda ya Nyanda za Juu Kusini, Lilian Mwangoka
aliipongeza Halmashauri ya Nkasi iliyopo katika mkoa wa Rukwa kuwa na
redio ya wilaya ijulikanayo kama Nkasi FM inayosaidia kufikisha taarifa
kwa jamii.
CHANZO: HABARI LEO
0 comments:
Post a Comment