Imeandikwa na Peti Siyame, Sumbawanga
MKUU wa Mkoa wa Rukwa, Zelothe Steven amesema ili aendane na kasi ya
falsafa ya Rais John Magufuli ya “Hapa Kazi Tu”, atakuwa akilala kwa saa
nne kila siku zilizobakia, saa 20 atakuwa kazini akisaka majibu sahihi
ya kero zinazowakabili wananchi wa mkoani humo.
Zelothe alibainisha hayo jana katika kikao maalumu cha kufahamiana
kilichojumuisha wazee, viongozi wa dini, watendaji wa umma na wajumbe wa
Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa huo kilichofanyika mjini hapa. Kwa
kawaida binadamu anatakiwa kulala saa nane na kufanya kazi si zaidi ya
saa 12 kwa siku.
Alisema aliamua kutumia fursa ya mapumziko ya madhimisho ya Siku ya
Karume kuzungumza nao ili kufahamiana na kuelewa vipaumbele vya mkoa huo
ambavyo atavisimamia kwa makini, ukaribu na uadilifu.
“Piga ua naahidi nitawasimamia watendaji wa Serikali Kuu na wale wa
Serikali za Mitaa ili nihakikishe wanaendana na kazi na juhudi za Rais
Magufuli kwa kauli mbinu yake ya ‘Hapa Kazi Tu’. “Msidhani napiga porojo
la nitakuwa nalala kwa saa nne tu, muda mwingine uliobakia (saa 20)
kwangu ni ‘Hapa Kazi Tu’, isitoshe kazini ninaripoti saa 1:30 asubuhi
kila siku za kazi,” alisisitiza Kamishna huyo mstaafu wa Jeshi la
Polisi.
Alionya kuwa kwa kila saa atakayokuwa kazini atakuwa na jukumu la
kupata majibu sahihi ya maswali sita ambayo ni “nini, wapi, lini, kwa
nini, nani na vipi lazima ninapowauliza watendaji maswali hayo nijibiwe
tena kwa usahihi mkubwa.” Alisisitiza kuwa lazima watendaji serikalini
wamjibu maswali hayo. “Niwahakikishie kuwa katika kupata majibu hayo
hakuna jiwe litakaloachwa bila kugeuzwageuzwa ... Lazima libinuliwe kwa
kuwa sababu ya kufanya hivyo ipo , uwezo upo pia nia ipo”.
Akisisitiza kuwa maofisa tarafa, kata na vijiji wamegeuka kuwa
“miungu watu’ akiwafananisha na ‘kutu ya chuma’ , wameacha kuwatumikia
wananchi badala yake wamegeuza kazi zao kuwa mitaji yao ya kujitajirisha
wakiwakera na kuwakatisha tamaa wananchi.
Awali akimkaribisha Msaidizi Katibu Tawala Mkoa wa Rukwa (Tamisemi),
Albinus Mgonya alieleza kuwa RC ameonesha njia na dira ya kufuata katika
utendaji wa kila siku wa watumishi wa umma. Wazee walieleza kuwa
watampatia ushirikiano wa kutosha ili asimamie vyema nidhamu na
uwajibikaji serikalini.
CHANZO: HABARI LEO.
0 comments:
Post a Comment