MKUU wa Mkoa wa Rukwa, Zelothe Steven amemwagiza Kamanda wa Polisi
mkoa huo, Jacob Mwaruanda kuwasaka na kuwakamata watumishi hewa 18
waliobainika katika uhakiki uliofanyika katika halmashauri zote mkoani
humo hivi karibuni.
Pia ameagiza fedha hizo zilizolipwa kwa watumishi hao hewa na kuiingizia hasara kubwa Serikali zirudishwe mara moja.
Akifafanua alisema katika uhakiki huo, watumishi hewa tisa
walibainika katika wilaya ya Nkasi, wanane katika Manispaa ya Sumbawanga
na mmoja wilaya ya Sumbawanga wakati Kalambo ikiwa haina mtumishi hewa.
Uhakiki huo unatokana na maagizo aliyotoa Rais John Magufuli baada ya
kuwaapisha wakuu wa mikoa aliowateua, aliwaambia wakafanye kazi ya
kutatua kero za wananchi na sio kwenda kufanya siasa.
Pia Rais Magufuli aliwapa wakurugenzi wa halmashauri siku 15 wawatoe
katika orodha ya malipo ya mshahara wafanyakazi hewa wote katika
halmashauri zote nchini.
Zelothe alitoa agizo hilo jana katika kikao maalumu cha kufahamiana
kilichojumuisha wazee , viongozi wa dini , watendaji wa umma na wajumbe
wa kamati ya ulinzi na usalama ya mkoa huo kilichofanyika mjini hapa.
Akisisitiza kuwa hajaridhishwa na uhakiki huo, hivyo akaagiza halmashuri
zote kurudia upya uhakiki wa watumishi.
“Siku ile ile nilipoapishwa kabla sijavuka geti kutoka nje ya Ikulu
nilipiga simu na kuagiza halmashauri zote (Manispaa, Nkasi, Kalambo na
Sumbawanga) kuanza uhakiki mara moja wasinisubiri hadi niripoti mkoani
hapa,” alieleza.
Aliongeza kuwa aliporudi mkoani humo na kuripoti kazini katika siku
yake ya kwanza ofisini alikabidhiwa kitabu chenye orodha ya watumishi wa
umma wa halmashauri zote akielezwa kuwa hakuna mtumishi hewa katika
mkoa wa Rukwa.
“Sikukubaliana nao nilikataa, nikaagiza ufanyike uhakiki mara moja
ndipo wamepatikana watumishi hewa 18 na watumishi wengine 137 wapowapo
tu wakiwa na taarifa zinazotia mashaka. Wote wamebainika kwenye hicho
kitabu nilichokabidhiwa kikionesha hakuna mtumishi hewa,” alisisitiza.
CHANZO: HABARI LEO.
0 comments:
Post a Comment