Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
DARAJA la mto Koga lililopo mpakani mwa mikoa ya Katavi na Tabora,
limefurika maji ya mvua na kusababisha vifo vya watu sita, ambao
wamesombwa na maji.
Pia mafuriko hayo yamesababisha foleni ndefu ya magari katika eneo la mto huo.
Akizungumza na gazeti hili kwa njia ya simu kutoka mjini Mpanda jana
jioni, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Katavi, Dhahri Kidavashari alisema watu
hao waliosombwa na maji na miili yao haijaonekana, hadi sasa ni
wanawake wawili na watoto wanne.
Alisema watu hao wamefikwa na umauti baada ya gari aina ya Toyota
Pick Up yenye namba za usajili T597 BTC, kusombwa na maji wakati
likijaribu kuvuka Mto Koga uliokuwa umefurika maji.
Kufurika maji kwa daraja la Mto Koga, kumesababisha kukatika kwa
mawasiliano ya barabara kati ya miji ya Mpanda mkoani Katavi na Sikonge
mkoani Tabora, na kusababisha kero kubwa kwa mamia ya abiria.
Inadaiwa kuanzia juzi zaidi ya 100 yalikuwa yamekwama huku idadi kubwa ya abiria wakikwama pia katika eneo hilo.
Walieleza kuwa wamesubiri kwa muda muda mrefu maji yapungue.
Miongoni mwa waathirika hao ni wanawake na watoto, wanaotumia
miundombinu kwa ajili ya kwenda kliniki na shuleni, wamelazimika kulala
eneo la mto huo kusubiri maji yapungue.
Kwa mujibu wa Kamanda Kidavashari, ajali hiyo ilitokea juzi saa 12
jioni baada ya gari hilo lililokuwa likitokea Tabora kwenda mjini Mpanda
kufika katika eneo hilo la Mto Koga na kukuta foleni ya magari
yakisubiri kuvuka.
CHANZO ; HABARI LEO.
0 comments:
Post a Comment