Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
HALMASHAURI ya Manispaa ya Sumbawanga imezidiwa na mzigo wa uzoaji
wa taka ngumu kutoka eneo lililotengwa kwa ajili ya kukusanyia kutokana
na uzalishaji wake kuwa mkubwa kuliko ilivyotarajiwa.
Hali hiyo imesababisha wakazi wa Kitongoji cha Sabato, eneo ambalo
limetengwa kwa ajili ya kukusanyia taka hizo, kuulalamikia uongozi wa
manispaa kwa kile walichodai kugeuzwa eneo hilo kama dampo la kudumu,
hivyo kuhatarisha afya zao.
Mmoja wa wakazi hao, Agness Chobalika, alisema pamoja na kufanya
jitihada za kuwaeleza viongozi wa manispaa hiyo na mkoa juu ya kero
hiyo ili kuliondoa dampo hilo, lakini hakuna aliyewajali.
“Tumeandamana hadi kwa Mkuu wa Mkoa wa Rukwa tukitaka waondoe dampo
kwenye eneo hili, lakini hakuna aliyetujali zaidi ya kutupuuza,”
alisema Agness.
Mkurugenzi Mtendaji wa Manispaa ya Sumbawanga, William Shimwela,
alikiri kuzidiwa na uwezo wa kuzoa taka, kwani katika taka tani 70
zinazozalishwa, tani 28 ndizo zinazoweza kuzolewa na kwenda kutupwa
kwenye dampo husika lililo nje kidogo ya mji huo.
Alisema sababu kubwa ya kushindwa kufanya hivyo ni ukosefu wa magari,
kwani lililopo ni moja na limekuwa likishindwa kumudu wingi wa taka.
Chanzo:Tanzania Daima
0 comments:
Post a Comment