Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
Kwa miaka 50 sasa, taifa letu limeshuhudia ufisadi wa kutisha,
huku baadhi ya viongozi wakijilimbikizia mali kwa upande mmoja na
Watanzania wakiendelea kuishi katika lindi la umaskini kwa upande
mwingine.
Hivi sasa tunashuhudia kiongozi wa umma anapewa
ofisi, lakini ndani ya kipindi kifupi anakuwa na utajiri wa kutisha,
watoto wao wanakuwa na utajiri wa kutisha bila kuainisha vyanzo vyao vya
mapato.
Lakini ibara 10 za Rasimu ya Pili ya Katiba
zilizopendekezwa na wananchi kama zitapita zilivyo, zitakuwa ndio
mwarobaini wa ufisadi kwa viongozi wa umma.
Pamoja na umuhimu wa ibara hizi kwa mustakabali wa
nchi yetu, bado Watanzania hawajazipa umuhimu unaostahili na badala
yake mjadala umejikita zaidi katika muundo wa muungano.
Ibara hizo 10 ambazo kwa hakika zitaongeza
uwajibikaji zipo katika sura ya tatu ya Rasimu ya Pili ya Katiba
zikihusu Maadili na Miiko ya uongozi na utumishi wa umma, zimeanzia
ibara ya 13 hadi ya 22.
Kwa mujibu wa ibara ya 13, madaraka atakayopewa
kiongozi wa umma ni dhamana na atatumia madaraka hayo kutekeleza wajibu
wake kwa kuheshimu wananchi na atateuliwa kwa misingi ya haki.
Kwamba kiongozi wa umma atazingatia uwezo, pasipo
upendeleo katika kufanya uamuzi na kuhakikisha uamuzi wake haufuati
udugu, ukabila, udini, upendeleo, rushwa na ubaguzi.
Sote ni mashahidi namna watoto wa vigogo
walivyoajiriwa katika taasisi nyeti, huku usaili wao ukidaiwa kugubikwa
na upendeleo. Baadhi ya ofisi zimejaa watumishi kutoka eneo moja.
Ibara ya 14 ya Rasimu ya Katiba inambana kiongozi
wa umma kwamba anapokuwa katika kazi za ofisi au binafsi atahakikisha
haruhusu kutokea kwa mgongano wa masilahi kati ya binafsi na ya umma.
Mbali na ibara hiyo, ibara ya 16 inambana kiongozi
wa umma kutofungua au kumiliki akaunti nje ya nchi isipokuwa kwa namba
ambayo sheria za nchi zinaruhusu.
Sharti hili ni muhimu hasa ikizingatiwa kuwa zaidi
ya Sh2 trilioni zinatoroshwa kila mwaka kwenda nje ya nchi, huku
viongozi wa umma na vigogo wengine wakimiliki akaunti za kigeni nje.
Mbali na utoroshwaji huo wa fedha, kuna mabilioni
ya Dola za Marekani, yanadaiwa kuhifadhiwa nchini Uswisi licha ya sheria
kutaka wapate kibali cha Benki Kuu ya Tanzania (BoT).
Ibara ya 16(b) inasema kiongozi wa umma “Hataomba au kupokea
mkopo au faida yeyote kwa namna au mazingira ambayo yanashusha hadhi au
heshima ya utumishi wa umma.
Ibara ya 17 ambayo ni muhimu mno kwa mazingira
tuliyonayo sasa ya viongozi wa umma kujilimbikizia mali. Inamtaka
kiongozi kutangaza mali zake anapoingia na kuacha uongozi wa umma.
“Kiongozi wa umma atalazimika kutangaza na
kuwasilisha mali zake, ndani ya siku 30 baada ya kupata uongozi na baada
ya kuacha uongozi, mali na thamani yake na madeni yake Tume ya
Maadili,” inasomeka.
Ibara hiyo fasili ndogo ya 2 (1) inambana kiongozi
wa umma kutangaza mali na madeni yake binafsi, ya mweza wake na ya
watoto wake waliochini ya umri wa miaka 18 mara moja kila mwaka. Ibara
ya 18, imeweka wazi kuwa kiongozi wa umma hatashiriki katika kufanya
uamuzi wa jambo au shughuli yoyote ambayo ana masilahi nayo yeye
binafsi, mwenza wake, watoto wake ama jamaa zake.
Hali ilivyo sasa katika nchi yetu inatisha. Baadhi
ya mawaziri wanafanya biashara na Serikali, wabunge wanafanya biashara
na Serikali, madiwani wanafanya biashara na Halmashauri.
Huu ni mgongano mkubwa wa masilahi. Ni mgongano
mkubwa kwa sababu wabunge ndio wanaopaswa kuisimamia Serikali.
Wataisimamiaje wakati inawapa mkate?
Vivyohivyo kwa madiwani, wapo baadhi sio wote,
wamesajili kampuni hasa za ukandarasi ambazo zimesimama kidete na
kuhakikisha halmashauri wanazozisimamia, zinazipa zabuni.
Ibara ya 21, imeweka bayana kuwa kiongozi wa umma
atapaswa kuheshimu na kutii maadili ya viongozi wa umma ikiwamo miiko ya
uongozi ambayo ni pamoja na kutotoa au kupokea rushwa.
Miiko hiyo ya uongozi ni pamoja na
kutojilimbikizia mali kinyume cha sheria kama ambavyo nimetangulia
kusema hapo juu kuwa “Utajiri wa viongozi wetu una maswali mengi kuliko
majibu”. Ibara hiyo ya 21 fasili ndogo ya 2(a) (vi), inamzuia kabisa
kiongozi wa umma kutumia wadhifa, nafasi au cheo chake kwa manufaa yake
binafsi, familia yake, ndugu, jamaa na marafiki zake.
Kiongozi wa umma kulingana na ibara hiyo ya 21
ambaye atatuhumiwa kwa makosa ya kimaadili, udhalilishaji wa mtu au wizi
au ubadhirifu wa mali za umma atakuwa amevunja katiba ya nchi.
Ibara hiyo imeweka wazi kuwa kiongozi wa aina hiyo
atasimamishwa kazi hadi suala lake litakapoamuliwa kwa mujibu wa sheria
za nchi au taratibu zinazohusu viongozi wa umma.
Sharti hilo ni muhimu sana, kwani kwa miaka mingi
tumeshuhudia viongozi wakishitakiwa kwa matumizi mabaya ya ofisi na bado
wakaendelea kuhudumia wananchi. Mifano hii ipo.
Ibara ya 22 inawazuia watumishi wa umma
kugombea, kuchaguliwa au kuteuliwa kushika nafasi ya madaraka katika
chama cha siasa au nafasi ya madaraka ya kisiasa ya aina yoyote chini ya
katiba hii.
“Mtumishi huyo atachukuliwa kuwa utumishi wake
umekoma tangu siku ya kuteuliwa kuwa mgombea, kuchaguliwa au kuteuliwa
kushika nafasi ya madaraka ya kisiasa au katika chama cha siasa.
Kuwapo kwa ibara hii kutasaidia kutatua kero ya
muda mrefu ya viongozi wetu kuwa na kofia mbili. Ni Rais wa nchi na hapo
hapo ni mwenyekiti wa taifa wa chama cha siasa. Hii haikubaliki.
Chanzo:Mwananchi
0 comments:
Post a Comment