Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
Wengi hukaa kimya bila kutoa taarifa pale wanapokutana na kadhia
licha ya kwamba wananyanyaswa na kutumikishwa na watu wao wa karibu,
wanaowaamini na kuwategemea.
Siyo kwa sababu hawaumii au kuathirika, bali ni
kutokana na woga wa yale watakayokumbana nayo baada ya ‘kuchoma utambi’
kwa vyombo vya usalama, ili kupata msaada zaidi.
Licha ya hao wanaojitambua, kuna kundi la wale
wasiojua kinachoendelea duniani, ambao hujikuta wakiishia katika madampo
kwa sababu tu wazazi wao walishindwa kuwalea baada ya kupata mimba
katika mazingira tatanishi.
Hii ndiyo hali halisi wanayokumbana nayo watoto wa
sehemu mbalimbali nchini katika maisha yao ya kila siku, ya kufanyiwa
vitendo vya kikatili. Jamii hiyo imejikuta ikiwa pweke na isiyo na
matumaini ya furaha.
Kwa mujibu wa Ripoti ya Haki za Binadamu ya mwaka
2013 iliyotolewa na Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) hivi
karibuni, anasema matukio ya unyanyasaji kwa watoto yameongezeka nchini
licha ya jitihada lukuki za kupambana nayo.
Ripoti hiyo inabainisha kuwa kuna kesi 863 za watoto kulawitiwa na ndugu wa karibu wakiwamo baba, kaka, binamu na wajomba.
Mbali na hao waliolawitiwa, ripoti hiyo inaongeza
kuwa wapo watoto zaidi ya 250 ambao walitupwa au kutelekezwa na walezi
au wazazi wao.
“Vitendo vya utelekezaji watoto vimekuwa
vikiripotiwa kutoka katika hospitali na vituo ya afya. Watoto wachanga
huachwa na mama zao saa chache baada ya kuzaliwa,” inasema sehemu ya
taarifa hiyo.
Kwa mujibu wa ripoti hiyo ya 11 tangu zilipoanza
kutolewa mwaka 2002, wazazi wa watoto hao hufanya vitendo hivyo kwa
madai ya kutokuwa tayari kulea viumbe hivyo, kutokana na ugumu wa
maisha.
Kutokana na kushamiri vitendo hivyo, mkurugenzi
mtendaji wa kituo hicho, Dk Hellen Kijo-Bisimba anapendekeza kuanzishwa
kwa vituo vitakavyotoa elimu ya malezi kwa wazazi na walezi, ili
kupunguza ukatili kwa watoto.
Hatua hiyo pia inaungwa mkono na Sia Malamsha,
mwanafunzi wa Chuo Kikuu cha Mtakatifu Agustino, ambaye anasema
wasichana wengi hujikuta wanapata mimba wakati hawajajiandaa kuwa mama,
hivyo hutafuta njia ya kukwepa majukumu.
“Unajua wengi huwa hawapo tayari kubeba majukumu
ya ulezi, hivyo huishia kumtupa au kumtelekeza mara tu baada ya
kujifungua,” anabainisha Sia anayesomea sheria.
Anaongeza kuwa tatizo hilo linaweza kuepukika iwapo serikali na
wadau wengine watafanya jitihada za kutoa elimu ya afya ya uzazi bila
kuchoka, ili wazazi wafahamu taratibu za kujiandaa kabla kupata
ujauzito.
Hata hivyo, binti huyo anatoa njia mbadala ambayo
inaweza pia kupunguza idadi ya watoto waliotelekezwa mitaani akisema ni
kuasili.
Sia anasema kuwa serikali ijaribu kupitia upya
sheria zake na kuzifanyia mabadiliko kwa ajili ya kurahisisha watu
wanaotaka kuasili watoto, waweze kuwapata kirahisi bila usumbufu.
Mbali na kurahisisha taratibu za kuasili, pia
anaongeza kuwa elimu itolewe kwa jamii kujua namna ya kuasili watoto na
taarifa zinazohusu masuala hayo ziwe wazi.
“Unajua kuna watu hawana watoto na wana shida ya
kupata watoto wa kuasili ili kuziba pengo walilonalo. Lakini wanashindwa
kujua watapata wapi watoto kutokana na kukosa taarifa sahihi juu ya
namna ya kuwapata na namna ya kuwaomba,” anasema Sia.
Ripoti hiyo pia inasema kuna kesi nyingi za
vipigo kwa watoto, ukilinganisha na aina nyingine ya unyanyasaji ambao
iliripotiwa mwaka jana kutoka katika shule na ndani ya familia
mbalimbali.
Inabainisha kuwa baadhi ya kauli za viongozi pia
zilichochea unyanyasaji wa watoto, ikiwemo ile ya aliyekuwa naibu waziri
wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Phillipo Mlugo ya kutangaza kuwa
serikali ina mpango wa kurudisha viboko shuleni kama njia ya kuhamasisha
uelewa kwa wanafunzi.
Msemaji wa Jeshi la Polisi nchini, Advera Senso
anasema matukio mengi ya unyanyasaji watoto hayaripotiwi katika vyombo
husika kwa ajili ya hatua zaidi, kutokana na watu wengi kuyapuuza kuwa
siyo uvunjifu wa haki za watoto.
Senso anaunga mkono ripoti ya LHRC na kuongeza
kuwa, wazazi na walezi wengi ndio wamekuwa mstari wa mbele kutekeleza
matukio hayo kutokana na ulevi au ushirikina.
Anaongeza kuwa ili kukabiliana na hali hiyo, Jeshi
la Polisi kwa kushirikiana na wadau wengine, lilianzisha madawati
maalumu ya kushughulikia matukio yote ya unyanyasaji kwa wanawake na
watoto katika mikoa yote nchini.
“Tangu tulipoanzisha madawati hayo idadi ya watu
wanaoripoti uvunjifu wa haki za watoto imeongezeka ukilinganisha na
kipindi cha nyuma,” anasema.
Hapo awali, kulikuwa na makabila mengi ambayo
yalikuwa hayajui vitendo wanavyofanya kuwa ni ukatili kwa wanawake na
watoto,” anasema Senso akiongeza kuwa mafanikio hayo ni matokeo ya
ushirikiano na wadau kama Wizara ya Jinsia, Wanawake na Watoto na
taasisi za kijami (NGOs).
Anabainisha kuwa kwa sasa wana utaratibu wa kuwahoji faragha
watoto, na kwamba hutoa siri nyingi juu ya ukatili unaofanywa dhidi yao.
“Tunaendelea kufanya maboresho ya vituo vya
kufanyia mahojiano katika vituo vya polisi mbalimbali nchini ili
kuhakikisha tunapunguza vitendo hivi. Lazima watu wajue kuwa awe mzazi
au mlezi; tukimkamata tutamfikisha mahakamani,” anaonya Senso.
Matokeo ya ripoti ya LHRC yameendeleza tu takwimu
za utafiti wa awali uliofanywa na Wizara ya Maendeleo ya Wanawake,
Jinsia na Watoto kwa kushirikiana na Shirika la Umoja wa Mataifa
linaloshughulia watoto (UNICEF) na Kituo cha Kudhibiti Magonjwa (CDC).
Iliongeza kuwa watoto wengi hapa nchini
walifanyiwa ukatili wa kingono, kimwili na kunyanyaswa kisaikolojia
kabla ya kufikisha miaka 18. Zaidi ya asilimia 70 ya watoto wote
walifanyiwa ukatili wa kimwili na kisaikolojia.
Hata wakati ukatili kwa watoto ukiendelea,
serikali nayo imekuwa ikifanya jitihada kupambana wa suala hilo, ikiwemo
kuwatoa watoto katika mazingira magumu.
Katika hotuba yake ya bajeti ya mwaka wa fedha
unaoishia, Waziri wa Maendeleo ya Wanawake, Jinsia na Watoto, Sophia
Simba alisema Serikali iliwatambua watoto 849,051 wakiwemo wasichana
407,544 sawa na asilimia 48 na wavulana 441,507 sawa na asilimia 52.
“Watoto hao kwa sasa wanapatiwa huduma za elimu,
afya, chakula na msaada wa kisheria na kisaikolojia kupitia wadau
mbalimbali,” alisema Simba akionyesha mafanikio ya mwaka 2012/13.
Pia serikali kwa kushirikiana na wadau waliandaa
mpangokazi wa miaka mitatu (2013–2016) wa kutokomeza ukatili kwa watoto,
uliozinduliwa mwaka jana.
Pamoja na jitihada hizo za serikali na wadau, bado
umma una wajibu wa kuhakikisha unalinda haki za watoto kwa kusimamia
kikamilifu Sheria ya Mtoto namba 21 ya mwaka 2009 na sera yake ya mwaka
2008.
Chanzo;Mwananchi
Chanzo;Mwananchi
0 comments:
Post a Comment