UONGOZI wa Chama cha Wafanyabiashara, Viwanda na Kilimo (TCCIA)
mkoani Rukwa, umeilaumu serikali kwamba inachangia kuua sekta ya kilimo
nchini.
Shutuma hizo zinatokana na serikali kupitia Wakala wa Hifadhi ya
Chakula nchini (NFRA) mkoani Rukwa kushindwa kuwalipa wakulima
waliowakopesha mahindi kuanzia Agosti hadi sasa na kuishia kutoa ahadi.
Akizungumza na waandishi wa habari mkoani hapa jana, Mwenyekiti wa
TCCIA Rukwa, Sadrick Malila ‘Ikuwo’, alisema kitendo cha serikali
kushindwa kuwalipa wakulima hao kinazidi kuwaongezea umasikini miongoni
mwao.
“Hivi sasa tayari msimu wa kilimo umeshaanza, unadhani mkulima huyo
atalimaje ikiwa hana fedha za kununulia pembejeo? Wengi huko vijijini
wamebaki kuitazama mvua kwa sababu hawana jeuri ya kuingia shambani,”
alisema Ikuwo.
Wakati TCCIA ikisema hivyo, baadhi ya vyama vya siasa mkoani hapa
navyo vimelalamikia kitendo cha wakulima kutolipwa fedha wanazodai
kutokana na kuuza mahindi NFRA.
Katibu Mwenezi wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Rukwa, Clemence Bakuli,
alisema chama hicho kinaitaka serikali kuwalipa haraka wakulima hao
ambao wengi wao wanategemea fedha hizo kwa ajili ya shughuli
mbalimbali.
Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) mkoani
Rukwa, Zeno Nkoswe, alisema kwa hali hiyo mafanikio katika kilimo
hayatapatikana kwa kuwa serikali inavunja moyo wakulima.
Wakulima mkoani Rukwa wanaidai NFRA zaidi ya sh bilioni 10 kutokana na mahindi waliyokopesha mwaka huu.
Chanzo;Tanzania Daima
0 comments:
Post a Comment