
Ofisa Ustawi wa Jamii wa Halmashauri wa Wilaya ya Nkasi, Oscar Mdenye
======= ======== ========
Aowa
Wanafunzi Mtu na Dada Yake
JESHI la
Polisi Wilaya ya Nkasi kupitia dawati la Jinsia na Watoto, linamshikilia
Pius Jacob Mkazi wa Kijiji cha Chala kwa kosa la kuoa mtu na dada yake, ambapo
mdogo mtu alikuwa ni mwanafunzi wa darasa la tano katika Shule ya Msingi Kabwe
wilayani Nkasi.
Jacob alikamatwa na Polisi wa Dawati la Jinsia na watoto Kituo
cha Nkasi ikiwa ni wiki moja tangu amchukue kwa nguvu binti huyo wa darasa la
tano (umri miaka 12) na kuja kuishi naye kama mke na mume huku akiwa tayari
amemuoa binti mwingine wa kwanza mwenye umri wa miaka 16 ambaye pia ni dada wa
binti wa pili.
Akizungumzia tukio hilo, Mkuu wa Dawati la Jinsia Nkasi,
CPL-Anna Kisimba alisema walimfuatilia Jacob na kumkamata baada ya wao kupewa
taarifa na mmoja wa majirani wa mtuhumiwa kuwa alikuwa akiishi kinyumba na
wanafunzi hao.
“…Tulikuwa katika ziara zetu za kawaida zilizoambatana na
siku 16 za kupinga ukatili tukizunguka baadhi ya vijiji vya wilaya yetu, ndipo
raia wema walituarifu kuwepo kwa tukio hilo na kuanza kufuatilia hatimaye
kumkamata mtuhumiwa,” alisema Kisimba.
Tayari mtuhumiwa huyo amefikishwa mahakamani kwa mara ya
kwanza Desenba 10, 2013 kwa kosa la kumuoa mwanafunzi na kubaka katika Mahakama
ya Wilaya ya Nkasi, Mkoa wa Rukwa kujibu mashtaka ya tuhuma zake.
Akizungumzia tukio hilo, Ofisa Ustawi wa Jamii wa
Halmashauri wa Wilaya ya Nkasi, Oscar Mdenye alisema baada ya kufuatilia zaidi
wamebaini hata binti (16) aliyemuoa wa kwanza alikuwa ni mwanafunzi haijulikani
alitumia mbinu gani za kumpata na kuanza kuishi naye kama mke na mume.
Aidha ameongeza kuwa kwa mujibu wa tarifa ambazo
walizipata kutoka kwa majirani inadaiwa binti wa pili alimpata kwa kutumia
nguvu na vitisho, kwani alimfuata nyumbani kwao na kudai anakuja kuwasalimia
lakini baada ya kufika kwake alimjulisha binti huyo kuanzia sasa wewe ni mke
wangu na kuanza kuishi naye.
“…Hadi Polisi na Ofisi ya Ustawi wa Jamii tunafikiwa na
taarifa hizo inadaiwa mtuhumiwa huyu alikuwa tayari ameishi na binti huyu wa
pili kwa wiki nzima nyumbani kwake, na majirani walijua baada ya binti wa pili
(12) kuanza kulalamika kwao kuwa alikuwa amechukuliwa kwa nguvu na kulazimishwa
kuolewa,” alisema Mdenye.
Juhudi za kumpata mtuhumiwa kuzungumzia tuhuma zake
hazikuweza kuzaa matunda baada ya kuwa mahabusu akisubiri mwenendo wa kesi yake
inayomkabili.
Hata hivyo matukio ya ukatili yanayoripotiwa polisi kupitia
Dawati la Jinsia na Watoto Wilaya ya Nkasi yamekuwa yakipungua kutoka mwaka
hadi mwaka, kwani kwa mujibu wa takwimu za dawati hilo kwa mwaka 2012 kulikuwa
na kesi 224 za ukatili zilizoripotiwa, ilhali kwa mwaka 2013 jumla ya kesi 143
zimeripotiwa wilayani hapo.
*Imeandaliwa na www.thehabari.com
kwa ushirikiano na TAMWA.
0 comments:
Post a Comment