KULINDWA
kwa vyanzo vya maji na misitu ya asili katika maeneo mbalimbali ya kata
ya Sintali wilayani Nkasi mkoani Rukwa kumetajwa kuwa sehemu ya matokeo
chanya ya elimu ya utunzaji mazingira iliyotolewa mwanzoni mwa mwaka
huu kwa wakazi wa kata hiyo.
Mtandao
wa asasi zisizo za kiserikali wilayani Nkasi (Nkango) ndiyo ulitoa
elimu hiyo kupitia mdahalo uliofanyika kijijini Sintali kwa ufadhili wa
The Foundation for Civil Society. Viongozi na wakazi wa kata hiyo
wanakiri kuwa elimu waliyoipata kupitia mdahalo huo miezi kadhaa
iliyopita imekuwa na manufaa makubwa kwani imewaongezea uelewa kwenye
masuala ya utunzaji wa mazingira na kukabiliana na mabadiliko ya
tabianchi.
Kaimu
ofisa mtendaji wa kata ya Sintali, Halle Siame, anasema baada ya kupata
elimu serikali za vijiji vya katahizo zimekuwa na mikakati endelevu ya
kutunza mazingira ikiwemo kuweka doria za kushtukiza kwenye maeneo ya
misitu ya asili kwa ajili ya kuwabaini watu wanaokata miti hovyo na
kuingiza mifugo kiholela kwenye misitu hiyo.
“Kwa
kata hii tuna vijiji vya Sintali, Nkana, Mkomanchindo na Kasapa na hivi
vyote vimekuwa na mikakati ya kuhakikisha misitu ya asili iliyotengwa
inalindwa. Uongozi wa kijiji husika unaweza kufanya doria ya mara kwa
mara kwenye misitu na kubaini waharibifu wa misitu hiyo,” anasema Halle
Siame.
“Lakini
pia kumekuwa na hamasa kubwa ya taasisi mbalimbali kujishughulisha na
uoteshaji wa miche ya miti kwa ajili ya kuigawa kwa wananchi tayari kwa
kuipanda kwenye maeneo yao. Lakini pia utaona kasi ya kuchoma mapori
yetu imepungua ikilinganishwa na awali. Viongozi wa vijiji pia mara kwa
mara wanaandaa mikutano ambayo wanaitumia kutoa elimu juu ya utunzaji wa
mazingira,” ameongeza Siame.
“Ni
dhahiri kuwa wakazi wengi sasa katika kata yetu wametambua umuhimu wa
kuyatunza mazingira. Wametambua pia juu ya athari zinazoikumba dunia
kutokana na kuharibiwa kwa mazingira kwa kuwa tayari zimetukumba hata
sisi. Moja kati ya athari hizo ni kutokuwa na misimu ya mvua
inayoeleweka kama ilivyokuwa miaka ya nyuma,” anasema kaimu ofisa
mtendaji wa kata hiyo.
Anasema
wanaokamatwa na kubainika wanakata miti hovyo na kuchoma mkaa bila kuwa
na kibali wanaadhibiwa sawa na wanaochoma moto mapori ambapo hutakiwa
kulipa faini ya kati ya Sh 20,000 hadi Sh 50,000. Naye Ofisa Mtendaji wa
kijiji cha Sintali, Crisense Silanga, anasema kwa kijijini hapo kamati
ya huduma za jamii ndiyo yenye jukumu la kutembelea msitu wa asili
uliopo kilomita chache kutoka eneo la makazi ya kijiji hicho.
Kwa
mujibu wa Silanga utendaji wa kamati hiyo kwenye kuilinda misitu na
vyanzo vya maji vilivyopo kijijini hapo umekuwa na ufanisi mkubwa katika
siku za hivi karibuni. Anasema bila shaka ni kutokana na wakazi kuanza
kupata uelewa juu ya nini madhumuni ya vijiji kulinda rasilimali hizo
muhimu kwa kizazi kilichopo na kijacho.
“Ukiangalia
ugumu uliokuwa ukizikumba kamati hizi kwa miaka ya nyuma
zilizopotembelea msitu na vyanzo vya maji ni tofauti na sasa. Kumekuwa
na ushirikiano mkubwa wa wananchi. Wapo baadhi ya wananchi wanaothubutu
hata kutoa taarifa pale wanapoona mtu akifanya uharibifu kwenye vyanzo
vya maji au akikata miti kwenye msitu wa kijiji,” amesema Crisense
Silanga.
“Zamani
haikuwa hivyo. Hata tulipochukua hatua dhidi ya wahusika wapo wananchi
walioonekana kutulaumu na kujenga chuki kwa wajumbe wa kamati na uongozi
wa kijiji kwa ujumla. Wao walijua ni uonezi na kila mtu ana haki ya
kuingia kwenye misitu tuliyotenga na kufanya kile atakacho hata bila
kibali,” amefafanua Silanga.
Alisema
pia kwa sasa zoezi la kupunguza mifugo ili iendane na eneo lililotengwa
kwa ajili ya malisho ya mifugo halisumbui sana. Wakazi ambao miaka ya
nyuma walikuwa wakiwapokea kiholela wafugaji na kuwapa hifadhi sasa ni
wachache waanaoendelea na tabia hiyo. Lakini pia wafugaji wanakubali
kuhamisha mifugo yao kupunguza idadi ambayo awali ulikuwa mzigo mkubwa
kwa kijiji.
Hata
hivyo, mwalimu mkuu wa shule ya msingi Sintali, Sezari Katelema,
anasema elimu zaidi bado inahitajika. Anasema bado wapo wakazi katika
kijiji hicho wanaopingana na mikakati inayofanywa na wadau wa utunzaaji
wa mazingira. “Wapo wafugaji ambao hawataki kuona miti ikipandwa
wakiamini watakosa maeneo ya kulishia mifugo yao.
Unapopanda
wao hung’oa miche hiyo. Mfano mzuri ni miti tuliyopanda katika eneo
moja la shule, kuna watu walipita usiku na kuing’oa. Wanataka maeneo
yawe wazi ili mifugo yao izurure hovyo. Nadhani elimu bado inahitajika
zaidi, hatuwezi kubadilika wote kwa pamoja,” amesema Sezari Katelema
akiwa ofisini kwake.
Mwalimu
Katelema anakitaja kijiji cha Sintali kuwa kati ya vijiji vilivyovyo na
bahati kubwa ya kuwa na vyanzo vya maji vya asili vingi. Mfano ni kile
kilichopo jirani na shule ambacho hutiririsha maji kwa mwaka mzima.
“Kijiji
hiki kinaweza kuongoza kwa mkoa mzima wa Rukwa kwa kuwa na maji mengi.
Serikali na wadau wanapaswa kuwekeza huku kwa kuhakikisha wanashirikiana
na wananchi kuweka mikakati madhubuti ya kuvilinda vyanzo hivi ili viwe
endelevu. Naamini uelewa mdogo huu uliopo si tatizo la wanakijiji,
tatizo ni wasimamizi hawajatoa elimu ya kutosha,” anaongeza Katelema.
Chanzo;Habari Leo
0 comments:
Post a Comment