Home »
» Auawa kwa kukatwa na shoka shingoni
Auawa kwa kukatwa na shoka shingoni
|
|
MTU mmoja aliyefahamika kwa jina la Ruswetura Mahongo (40)
mkazi wa Kijiji cha Kambuzi Halt, Wilaya ya Mlele, Mkoa wa Katavi
ameuawa kwa kukatwa na shoka kichwani na shingoni na sehemu ya bega
la kulia na watu wawili waliokuwa wakifanya kazi ya kibarua nyumbani
kwake ya kujenga uzio wa zizi la ng’ombe.
Kwa mujibu wa Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Katavi, Dhahiri
Kidavashari, alisema tukio hilo la mauaji ya kutisha lilitokea jana
majira ya saa kumi na moja jioni nyumbani kwa marehemu.
Alisema siku moja kabla ya mauaji hayo alifika mtu mmoja nyumbani
kwa marehemu na kuomba kibarua cha kutengeneza zizi la ng’ombe na
ndipo alipokubaliwa na kuanza kazi ambayo hakuimaliza siku hiyo.
Kidavashari alieleza siku iliyofuata kibarua huyo alifika nyumbani
kwa marehemu akiwa na kijana mwingine ambaye alionekana kumsaidia
kazi hiyo hata marehemu alielewa hivyo.
Alisema ilipofika majira ya saa kumi na moja jioni marehemu akiwa
amelala kwenye jamvi pembeni ya nyumba yake mke wake mdogo aitwaye
Tatu Shiranga alimuaga marehemu kuwa anakwenda mtoni kuteka maji na
alimuacha marehemu akiwa na vibarua hao pamoja na mtoto wake mdogo
mwenye umri wa miaka saba.
Baada ya mke wake kuondoka vibarua hao walimfuata mahali alipokuwa
amelala marehemu na kuanza kumkatakata kwa shoka kichwani, shingoni
na kwenye bega, hali ambayo ilisababisha mwanae huyo mdogo akimbie
mbio na kujificha kichakani huku akiwa akishuhudia wanavyomshambulia
baba yake na alishindwa kuomba msaada kwa majirani kutokana na wao
kuishi mbali na majirani.
Kamanda Kidavashari alieleza mke wa huyo wa marehemu alirejea kutoka
mtoni kuteka maji ndipo alipokaribia kufika kwake mtoto wake
alimkimbilia na kumweleza kuwa wale watu wawili waliokuwa wakifanya
kazi ya kibarua wamemkata baba yake kwa shoka na kisha wamekimbilia
porini.
Alisema mke wa marehemu alilazimika kwenda kuangalia pale ambapo
alikuwa amemuacha mumewe amelala na ndipo alipomkuta akiwa
amegalagala chini huku mwili wake ukiwa na majeraha makubwa na damu
zikiwa zimetapakaa huku akiwa amefariki dunia.
Alifafanua kuwa uchunguzi uliofanywa na Jeshi la Polisi baada ya
kumhoji mke mdogo wa marehemu na ndugu zake kifo hicho kimesababishwa
na sababu mbambali zilizotokana na tabia ya ukorofi na ubabe wa
marehemu kwa majirani na ndugu zake.
Marehemu wakati akiishi katika Kijiji cha Mtowisa Mkoa wa Rukwa hapo
mwaka 2012 aliwahi kuvamiwa na watu wasiojulikana na kushambuliwa kwa
mapanga na kuponea chupuchupu na nyumba yake kuchomwa moto na ndipo
baada ya hapo marehemu aliamua huhamia katika kijiji hicho mkoani
Katavi.
Kamanda Kidavashari alisema mpaka sasa hakuna mtu aliyekamatwa na
jitihada za kuwasaka watu waliohusika katika mauaji ili
wafikishwe kwenye vyombo vya sheria zinaendelea.
Chanzo;Tanzania Daima
|
|
0 comments:
Post a Comment