Home » » BEI YA PETROL HAIKAMATIKI RUKWA, LITA MOJA YAUZWA SH.10, 000

BEI YA PETROL HAIKAMATIKI RUKWA, LITA MOJA YAUZWA SH.10, 000


Mussa Mwangoka, Sumbawanga-Rukwa Yetu

TATIZO la kuadimika kwa nishati ya mafuta ya petroli mara kwa mara limeendelea kuwa sugu Mkoani Rukwa baada ya bidhaa hiyo muhimu kuadimika tena katika miji ya Namanyere wilayani Nkasi na Manispaa ya Sumbawanga hivyo kumesababisha bei yake kupanda maradufu.

Katika maeneo mawili bei ya nishati hiyo imepanda kwa kasi kutoka 2,500 hadi Sh 8,000 na Sh 10,000 kwa lita moja, ikiwa ni ndani ya kipindi cha siku tano tangu kuadimika kwa bidhaa hiyo kwenye vituo mbalimbali vya mafuta.

Pamoja na  kadhia  hiyo,  pia imebainika kuwa  nishati ya mafuta ya taa  imeadimika  kwa  zaidi ya mwezi mmoja sasa katika wilaya ya Nkasi huku wakazi wa  mjini  humo  wakidai  kuwa  wameshasahau kabisa kuwepo  kwa  nishati hiyo.

Uchunguzi uliofanywa na Rukwa yetu umebaini kuwa hivi sasa watu binafsi "walanguzi" ndio wamekuwa wakifanya biashara mitaani ambapo huuza mafuta hayo kwa bei hiyo kitu ambacho kimekuwa kikilalamikiwa na baadhi ya watumiaji wa bidhaa hiyo.

"Ndugu yangu 'kufa kufaana' kuna jamaa zangu huwa wananunua kiasi kikubwa cha mafuta na kuhifadhi ndio wamenipa 'dili' niuze kwa lita Sh 7,000 na mie  naamua kupandisha  bei  hadi kufikia Sh  10,000-wananunua asiyetaka shauri yake na aache kwani  wengine wako tayari "  alisema mmoja wa wauzaji wa mafuta hayo Michael Kipara mkazi wa Jangwani.

Kutokana na hali hiyo vyombo vya usafiri vinvyotoa huduma ya usafiri ikiwa ni pamoja na daladala, teksi na pikipiki ‘bodaboda’ katika mji huo vimeadimika na kusimamisha huduma huku vingine vikipandisha bei ya usafiri huo mara tatu zaidi.

Mafuta ya petroli yamekuwa na soko kubwa mwambao wa Ziwa Tanganyika na nchi jirani ya Kongo (DRC) ambapo wafanyabiashara wakubwa wa mjini humo wanalazimika kuelekeza nguvu zao huko katika kutafuta soko la uhakika.

Hata hivyo baadhi ya wananchi wameeleza kusikitishwa kwao juu ya kukosekana kwa mafuta katika miji  hiyo mara kwa mara, huku wakieleza kuwa mara nyingi hali hiyo inajitokeza mara Ewura inapotangaza kushusha bei ya nishati hiyo kitu ambacho hakipaswi kufumbiwa macho.
Blogzamikoa
Jika Anda menyukai Artikel di blog ini, Silahkan klik disini untuk berlangganan gratis via email, dengan begitu Anda akan mendapat kiriman artikel setiap ada artikel yang terbit di Creating Website

0 comments:

Post a Comment

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Rukwa Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa