Mussa Mwangoka, Sumbawanga.
IMEELEZWA kuwa maisha ya wakazi wa mwambao mwa Ziwa Tanganyika wilayani Nkasi mkoani Rukwa yako hatarini kwa kukumbwa na matukio ya mara kwa mara ya kuvamiwa na Majambazi toka nchi jirani kutokana na kukosekana kwa mawasiliana na vituo vya polisi vilivyo katika maeneo hayo.
Mkuu wa wa wilaya ya Nkasi, Iddy Kimanta, alisema hayo juzi wakati akizungumza na uongozi wa Chama cha Mapinduzi mkoa wa Rukwa waliofanya ziara ya siku mbili kukagua shughuli za maendeleo kwenye wilaya hiyo.
Kimanta alisema kuwa kutokana na kukosekana kwa mawasiliano, majambazi hao kutoka nchi jirani wamekuwa wakipata mwanya wa kufanya vitendo vya kihalifu huku wakifahamu kuwa itachukua muda mrefu vyombo vya usalama kufika kwenye maeneo hayo.
Alisema kuwa hali hiyo imewafanya wakazi wa maeneo hayo kuishi kwa hofu kubwa kwa kudhani kuwa wanaweza kuvamiwa wakati wowote hali inayochangia kudumua kwa uchumi wa wananchi hao.
Mkuu huyo wa wilaya alisema katika kukabiliana na hali hiyo wilaya imeanza kuwahamasisha wakazi wa maeneo hayo kujenga vituo vya polisi, lakini pia kuzishawishi kampuni za simu za mikononni kufikiria kujenga minara ya mawasiliano kwenye maeneo hayo ambayo yana mwingiliano mkubwa watu na shughuli nyingi za kiuchumi.
Maeneo ya mwambao mwa Ziwa Tanganyika hususani kwenye kata za Kala na Wampembe wilayani Nkasi yamekuwa yakikumbwa na uvamizi wa mara kwa mara ambapo Majambazi toka nchi jirani kwa kushirikana na baadhi ya wenyeji wamekuwa wakivamia na kuwapora wavuvi na baadhi ya Wafanyabiashara kisha kutoroka kwa mitumbwi kwenda nchi jirani.
0 comments:
Post a Comment