Home » » Majambazi wamvamia jirani na wazazi wa Pinda wilaya ya mpanda Mkoani Rukwa

Majambazi wamvamia jirani na wazazi wa Pinda wilaya ya mpanda Mkoani Rukwa

MAJAMBAZI wanne wakiwa na marungu na silaha isiyojulikana, wamevamia nyumba ya Ofisa Mtendaji wa Kijiji cha Kibaoni jirani na nyumbani kwa wazazi wa Waziri Mkuu Mizengo Pinda, 

katika Kata ya Usevya, Tarafa ya Mpibwe wilayani Mpanda, na kupora fedha taslimu. 

Kwa mujibu wa Polisi wa Mkoa wa Rukwa, majambazi hao wamevamia nyumbani kwa Ofisa Mtendaji huyo, Ladislaus Munguwajua (37), saa tatu usiku Jumamosi wakiwa na bunduki 
isiyojulikana na marungu, na walimshambulia mtendaji huyo kichwani kwa kutumia marungu 
wakimlazimisha awapatie fedha. 

Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Rukwa, Jacob Mwaruanda, alisema majambazi hao walipora fedha taslimu Sh milioni moja ya mtendaji huyo ambaye anajishughulisha na biashara, huku wakimlazimisha kuwapatia funguo za kasiki walilolikuta nyumbani kwa 
Mtendaji ambalo hulitumia kuweka fedha. 

Fedha hizo ni zile zinazotokana na biashara ya kuuza mabati kwa bei ya punguzo ambayo yanasadikiwa ni ya Kampeni ya Ondoa Nyasi Mkoa wa Rukwa na Katavi inayojulikana kwa jina la ONYARU; mradi ambao unaelezwa kwamba unaungwa mkono na Waziri Mkuu Pinda. 

Kwa mujibu wa Polisi, licha ya kubanwa na kupigwa, mtendaji huyo alikana kuwa na funguo za kasiki hiyo kwa sababu zilikuwa zimepotea siku tatu kabla ya kuvamiwa; hivyo majambazi hao wakajaribu kulifungua kwa kutumia silaha zao na kushindwa na kuamua kuondoka na fedha 
walizompora mtendaji huyo. 

Kaimu Kamanda Mwaruanda alisema katika tukio hilo, majambazi hao pia walimjeruhi Mwenyekiti wa Kijiji hicho, Gaston Kamina (52), ambaye alikuwa akitazama video na kujeruhiwa mkononi kwa marungu ambapo alitibiwa katika Zahanati ya Kijiji cha Kibaoni na kuruhusiwa. 

Mtendaji huyo alipelekwa Hospitali ya Wilaya ya Mpanda ambako alitibiwa na kuruhusiwa kurejea nyumbani. 

Aidha, Polisi walifika eneo la tukio usiku huo na kuendesha msako ambao walifanikiwa 
kuwakamata watuhumiwa wawili, Wilembo Salum (35) na Kheri Obeid (30), wote wakulima 
wa kijiji jirani cha Usevya. 

Mwaruanda alisema eneo la tukio kuliokotwa maganda mawili ya risasi za SMG/SAR, na watuhumiwa hao wanahojiwa na watafikishwa mahakamani baada ya uchunguzi wa 
awali utakapokamilika; huku Polisi ikiendelea kuwasaka watuhumiwa wengine waliohusika na uvamizi huo. 

Katika hatua nyingine, Mkuu wa Mkoa wa Rukwa, Stella Manyanya amemwagiza Kaimu Kamanda huyo kuhakikisha anashiriki katika kuwasaka wote walioshiriki kuvamia kijiji hicho kwao Waziri Mkuu. 

Manyanya alisema ni lazima watuhumiwa hao wafikishwe katika sheria na kutoa onyo kwa wengine wanaodhani mikoa hiyo ni kimbilio la wahalifu. 
Habari kwa hisani ya Habari leo
Jika Anda menyukai Artikel di blog ini, Silahkan klik disini untuk berlangganan gratis via email, dengan begitu Anda akan mendapat kiriman artikel setiap ada artikel yang terbit di Creating Website

0 comments:

Post a Comment

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Rukwa Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa