Home » » MWIGULU: WANANIITA NYERERE

MWIGULU: WANANIITA NYERERE

 Ni juu ya mbio za urais.
Naibu Waziri wa Fedha, Mwigulu Nchemba.
Naibu Waziri wa Fedha, Mwigulu Nchemba, ameibuka na mpya baada ya kujifananisha kwamba yeye ni sawa na Baba wa Taifa, hayati Mwalimu Julius Nyerere na aliyekuwa Waziri Mkuu, hayati Edward Sokoine, kwa madai ya kuwa na misimamo isiyoyumba katika masuala yenye maslahi kwa taifa.

Mwigulu, ambaye pia ni Naibu Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Tanzania Bara, aliyasema hayo juzi wakati akizungumza katika kipindi cha dakika 45 kinachorushwa na kituo cha televisheni cha ITV, ambapo alizungumza mambo mbalimbali, likiwamo suala la uchotwaji wa zaidi ya Sh. bilioni 300 katika akaunti ya Tegeta Escrow, iliyokuwa Benki Kuu ya Tanzania (BoT).

Alisema suala la yeye kuitwa Sokoine, halijaanza leo, kwani hata alipokuwa anasoma, alikuwa akiitwa mara Nyerere au Sokoine, hasa kutokana na misimamo yake isiyoyumba, hususan katika masuala yenye maslahi kwa taifa.

“Ukicheza kama (Christian) Ronaldo ukapiga chenga kama Ronaldo, watakwita Ronaldo. Majina wanayoniita ni ya watu maarufu waliokuwa wakisimama katika haki ili kutetea haki za wanyonge,” alisema.

Alisema viongozi waliopewa uongozi wana wajibu mkubwa wa kutetea haki za wanyonge, kwani wapo watu, ambao hawana fursa ya kusema na jambo hilo likiachwa kuna siku mawe yatasema na haijulikani nini kitakachotokea.

URAIS 2015
Akijibu swali lini atatangaza kugombea urais katika uchaguzi mkuu wa mwaka huu, Mwigulu, ambaye pia ni Mbunge wa Iramba Magharibi (CCM), alisema yupo katika Chama kwa ajili ya kusimamia misingi na miiko ya Chama, hivyo hawezi kuwa miongoni mwa wanaoivunja.

“Mimi nipo kwenye Chama. Nimepewa jukumu la kusimamia  miiko na misingi ya Chama. Hivyo, nisingependa niwe miongoni mwa wanaovunja miiko. Tutavuka mto. Tukishavuka, tutaangalia,” alisema Mwigulu.

Kuhusu maagizo yanayotolewa na Katibu Mkuu wa CCM kwa watendaji wa serikali, alisema kwa utaratibu wa uendeshaji wa serikali ndani ya mfumo wa vyama vingi, Chama ndicho kinachoisimamia serikali.

“Sasa hivi tunakwenda kwenye uchaguzi. Watakaokwenda kuomba kura kwa wananchi ni wana-CCM siyo wataalam ama katibu mkuu wa wizara ndiyo atakwenda kufanya kampeni, hapana, ni chama,” alisema Mwigulu.

WALA RUSHWA WAFILISIWE
Alisema kuna haja kwa watumishi wa serikali au viongozi wanaobainika kula rushwa wawe wanafilisiwa mali zao, kupelekwa mahakamani na wasiwe wanapewa dhamana hadi siku ya hukumu.

“Inatakiwa ijulikane mtu akila rushwa na kugundulika kwanza fedha hiyo airudishe, afilisiwe na kufikishwa mahakamani na kusiwe na dhamana mpaka siku hukumu itakapotolewa,” alisema Mwigulu.

Alisema kama utaratibu huo utawekwa, watu wataogopa kuiba au kula rushwa, lakini inapokuwapo sheria na haki zaidi kumlinda mtu, ambaye anaibia wenzake, inakuwa ni tatizo.

“Siyo mtu amepoteza au amesababisha hasara ya Sh. milioni tatu halafu mnashusha nguvu mnatumia Sh. milioni moja kumshughulikia, halafu aliyefuja Sh. milioni 20 anashushwa cheo tu kwa kigezo cha utawala bora ama utawala wa sheria, hapana,” alisema Mwigulu.

Alisema ni jambo la kushukuru kwa serikali ya awamu ya nne chini ya Rais Jakaya Kikwete, kuanzisha taasisi kama ile ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), ambayo ina jukumu la kushughulikia vitendo vya rushwa.

Mwigulu alisema Tanzania ijayo inatakiwa ijengwe kwenye misingi ili kila mtu ajipime kama anatosha kwa uadilifu, kwani hata nchi zilizoendelea zimefanikiwa kutokana na kujiwekea misingi yake.

Alisema haiwezekani kuwa na utawala bora au haki za binadamu zinazolinda raia wanaonewa walio wengi na kulinda wanaoibia wengine.

Mwigulu alisema Watanzania lazima watambue kuwa mtu akiiba au kupoteza fedha za umma, anakuwa amesababisha watu wengine kufa kwa kukosa dawa hospitalini au akina mama wajawazito kukosa huduma.

Alisema mazingira haya yanakuwa yametengezwa na mtu, ambaye hakutimiza wajibu wake.

“Huwezi ukawa na haki ya binadamu ama utawala bora bila kuchuckua hatua. Ni lazima kuwalinda na wanaoonewa. Haiwezekani kwa mfano, mtu anapoteza Sh. bilioni 20 halafu adhabu kubwa anayopata anaondolewa cheo tu au kuhamishwa kituo cha kazi. Hii ni sawa na kumpa likizo akatumie fedha alizochukua,” alisema Mwigulu.

Alisema awamu ya nne imefanikiwa kuweka uwazi katika suala la hesabu kwenye mapato na matumizi ya fedha za umma na hivyo, awamu ya tano ijayo inapaswa kuanza kuwashughulikia watu wanaofuja fedha ili kujenga nidhamu katika matumizi ya fedha za umma.

“Siyo tu kwamba, ni fedha za wahisani kwamba, ndiyo tutumie vizuri. Huko tunakokwenda fedha yoyote inatakiwa itumike kwa uadilifu ili kuwafanya walipakodi waone kodi wanayoitoa inatumika kwa malengo yaliyokusudiwa,” alisema Mwigulu.

Alisema mtu akilipa kodi ya umeme aone umeme, atakuwa na moyo wa kulipa na hakutakuwa na suala la kukimbizana kuhusu kulipa kodi.

“Lakini mtu akilipa kodi akaona yeye anaendelea kuwa maskini na kuna ngazi au viongozi waliopo madarakani wananeemeka na familia zao, inavunja moyo wa kulipa kodi,” alisema Mwigulu.

KASHFA YA ESCROW
Alisema Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) imeshawafanyia mahesabu ya kodi wanayopaswa kulipa kwa serikali wote waliopata mgawo wa fedha za akaunti ya Tegeta Escrow na kwamba, ni lazima italipwa na siyo jambo la mjadala.

“Lazima tajiri alipe kodi ili tuweze kusomesha maskini. Hatuwezi kusamehe kodi kubwa namna ile halafu tukakimbizana na mama mjane anayeuza mchicha,” alisema Mwigulu.

Alisema katika dhamana ya utumishi, kila mmoja anabeba yake kwa sababu amesomeshwa na kodi ya serikali na kuaminiwa  na taifa, hivyo haiwezekani afanye kosa halafu adhabu aibebe balozi wa CCM.
CHANZO: NIPASHE
Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
Jika Anda menyukai Artikel di blog ini, Silahkan klik disini untuk berlangganan gratis via email, dengan begitu Anda akan mendapat kiriman artikel setiap ada artikel yang terbit di Creating Website

0 comments:

Post a Comment

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Rukwa Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa