Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
WAKALA wa Akiba ya Chakula wa Taifa (NFRA), ameshindwa kulipa deni
la zaidi ya sh. milioni 600 zinazodaiwa na Halmashauri ya Wilaya ya
Nkasi mkoani Rukwa kutoka kwenye ushuru wa mahindi ya wakulima kwa
misimu mitatu mfululizo.
Hali hiyo imeiweka katika kipindi kigumu halmashauri ya Nkasi kwa
kuikosesha mapato ya ndani yanayofikia asilimia 30 kutoka kwenye zao la
mahindi na hivyo kukwamishwa utekelezaji wa maendeleo ya jamii.
Mkurugenzi Mtendaji wa halmashauri hiyo, Kimulika Galikunga alieleza
hayo juzi wakati akihojiwa na Tanzania Daima kuhusu madai yanayotolewa
na wananchi juu ya mkwamo wa utekelezaji wa miradi.
Alisema kuwa licha ya kuwepo kwa changamoto nyingi za ukusanyaji wa
mapato ya ndani bado mdai wao mkubwa ni NFRA, anayedaiwa sh.
629,561,077.
Galikunga alisema kuwa miaka mitatu mfululizo wakala huyo amekuwa
akinunua mazao ya wakulima lakini hajalipa ushuru wa mazao aliyonunua na
kusababisha deni hilo kuongezeka zaidi.
Akifafanua juu ya deni hilo, alisema katika msimu wa 2010/2011, NFRA
ilikuwa na deni la sh.103,668,990 na mwaka 2011/2012 deni lilikuwa sh.
410,333087, ambapo alilipa sh. milioni 200 akabakiza deni la sh.
210,333,087.
Alisema kuwa deni hilo liliongezeka tena msimu wa kilimo mwaka
2012/2013 na kuwa sh. 315,559,000, hivyo kufanya jumla kwa misimu yote
mitatu kufikia sh. 629,561,077.
Kwa mujibu wa mkurugenzi, jitihada mbalimbali za ufuatiliaji wa madai
ya hayo zimekuwa zikifanywa pia na Katibu Tawala wa mkoa wa Rukwa na
timu ya maafisa wa halmashauri hiyo kwenda jijini Dar es Salaam lakini
hakuna matunda yaliyoonekana zaidi ya kuendelea kupigwa danadana.
Chanzo;Tanzania Daima
0 comments:
Post a Comment