Umuhimu wa elimu na mafunzo ya ufundi unaonekana kutokana na
ukweli kwamba rasilimali watu ni suala la muhimu katika mchakato wa
maendeleo.
Bila ya rasilimali watu, vigezo vingine kama mtaji, ardhi na rasilimali nyingine haviwezi kuwa na manufaa yoyote.
Hata hivyo, rasilimali watu itakuwa na tija kama
tu itapewa nyenzo na ujuzi ili kuboresha utendaji na ufanisi. Hiki
ndicho hasa elimu na mafunzo ya ufundi inalenga kukifanya.
Tangu baada ya mapinduzi ya viwanda katika nchi za
Ulaya Magharibi katika karne ya 18 na 19, maendeleo na mafanikio ya
elimu ya ufundi, vimenasibishwa kwa karibu na maendeleo ya kiuchumi. Na
maendeleo yoyote ya kiuchumi ya nchi husika hutokana na ubora wa
rasilimali watu wa nchi husika.
Ubora huu wa rasilimali watu hutokana na ubora wa
mfumo wa elimu wa nchi husika. Elimu na mafunzo ya ufundi inachukuliwa
kama ni mojawapo ya vigezo muhimu katika kukuza uzalishaji na uchumi kwa
jumla.
Katika kufanikisha hili, shule na vyuo vina jukumu
la kuandaa na kuzalisha nguvukazi yenye ujuzi wa kutosha ili kuongeza
ufanisi kazini.
Kama anavyosema mwandishi aitwaye Giroux, elimu na
mafunzo ya ufundi nyakati zingine huwa ni zana ya kutatua matatizo ya
kiuchumi, kisiasa na kijamii ambayo yanatishia uimara wa kiuchumi na
kisiasa wa baadhi ya mataifa.
Kuongezeka kwa idadi ya watu wasio na ajira na
mabadiliko ya namna ya utendaji kazi, yameliweka suala la elimu ya
nguvukazi kuwa lenye kipaumbele cha juu katika uboreshaji wa mifumo ya
elimu.
Katika utafiti nilioufanya mwaka 2009 wilayani
Temeke, nilibaini kuwa wahojiwa wengi walikiri kuwa elimu na mafunzo ya
ufundi vilikuwa na mchango mkubwa katika maendeleo ya Taifa letu; na
vyuo vya ufundi viliandaa wahitimu wa kutosha kutokana na mahitaji ya
nchi kwa wakati huo.
Aidha, walikiri kuwa elimu na mafunzo ya ufundi
ilikuwa bora zaidi ukilinganisha na elimu ya taaluma katika kukuza
ujuzi, teknolojia na ujasiriamali.
Pia, kwenye uwezo wa kujiajiri watahiniwa wa vyuo
vya ufundi walionekana kuwa na uwezo zaidi ukilinganisha na watahiniwa
katika elimu ya kawaida.
Utafiti ulibaini kuwa vyuo vya ufundi vya umma
vinaweza kupata mafanikio zaidi pamoja na ufanisi wa hali ya juu kama
vitaendeshwa kibiashara.
Vikiendeshwa kwa sura hiyo vitapata faida kubwa zaidi na hivyo
kufidia pengo linalotokana na upungufu wa ruzuku kutoka serikalini.
Zaidi ya hayo, wahojiwa wengi walikubaliana kwamba
mtalaa uliopo wa elimu na mafunzo ya ufundi ulikidhi mahitaji ya soko
la ajira kwa wakati huo.
Pia, utafiti uliofanywa na Castro na Verdisco
mwaka 1998 katika nchi za Argentina na Chile, ulibaini elimu na mafunzo
ya ufundi vilikuwa na mchango mkubwa katika kukuza fursa za ajira na
kuleta maendeleo ya nchi husika.
Utafiti ulibaini kuwa asilimia 60 ya wahitimu
kutoka katika vyuo vya ufundi katika nchi hizo walipata ajira
ukilinganisha na wahitimu wa elimu ya kawaida.
Hapa nchini elimu na mafunzo ya ufundi vikitumika vizuri vinaweza kuleta mabadiliko makubwa katika sekta ya kilimo na viwanda. T
Teknolojia rahisi zikifundishwa na kuenezwa katika maeneo ya vijijini zitaweza kukuza uzalishaji vijijini.
Teknolojia hizi ni kama zile za uendeshaji na
ukarabati wa mitambo inayotumika katika sekta ya kilimo. Pia, elimu na
mafunzo ya ufundi vinaweza kusaidia kuanzishwa kwa viwanda vidogovidogo
mijini na vijijini
Chanzo:Mwananchi
Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
0 comments:
Post a Comment