Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
Tunashangazwa na Serikali kuendelea kushikwa na kigugumizi
linapokuja suala la kutaja tarehe ya kufanyika kwa Uchaguzi wa Serikali
za Mitaa. Kwa kawaida uchaguzi huo hufanyika Septemba kila mwaka wa
uchaguzi, kwa maana ya mara moja kila baada ya miaka mitano.
Uchaguzi wa Serikali za Mitaa ni muhimu pengine
kuliko uchaguzi mkuu katika nchi yoyote, kwani ndiyo hasa hutoa sura na
taswira ya mamlaka ya wananchi walio wengi kuanzia ngazi za chini ambako
ndiko viongozi wa kitaifa hupata uhalali wa kuongoza nchi husika.
Kwa maana hiyo, uchaguzi huo ni muhimu katika kudumisha demokrasia na utawala bora.
Ndiyo maana serikali nyingi duniani huelekeza
nguvu nyingi katika kuhakikisha kwamba uchaguzi wa serikali za mitaa
siyo tu unafanikiwa, bali pia unakuwa huru na haki.
Licha ya kuhitaji fedha na rasilimali nyingi
katika maandalizi yake, uchaguzi huo uhitaji muda wa kutosha kuhamasisha
wananchi wajitokeze kupiga kura siku ya uchaguzi ili kuunda serikali
ambayo itashughulikia matatizo ya wananchi katika ngazi hiyo.
Hivyo, malalamiko yaliyotolewa juzi na viongozi wa
vyama vya upinzani nchini kuhusu ukimya wa muda mrefu wa Serikali
katika suala hilo ni za msingi kabisa. Kwamba vyama vya Chadema, CUF na
NCCR-Mageuzi vimekwazwa na ukimya wa Serikali kuhusu lini hasa uchaguzi
huo utafanyika, ni malalamiko ambayo hayapaswi kupuuzwa hata kidogo.
Kinachofanyika sasa ni kama mchezo wa kuigiza,
kutokana na wahusika wa uandaaji wa uchaguzi huo wanatupiana mpira na
hakuna aliye tayari kuzungumzia suala hilo. Hali hiyo inaonyesha kwamba
Serikali iko njia panda pengine kutokana na hali ngumu ya kifedha
inayoikabili, ingawa imeshindwa kutambua madhara ya kisiasa yanayoweza
kutokea kutokana na ukimya wake huo wa muda mrefu katika suala hilo
zito.
Tayari mazingira yanayoashiria shari za kisiasa
yameanza kujengeka. Vyama vya upinzani vimejenga dhana kwamba chama
tawala kimeng’amua kitashindwa katika uchaguzi huo, kutokana na vyama
hivyo vya upinzani kuunda Umoja wa Katiba ya Watanzania (Ukawa) na
kuamua kushirikiana chini ya umoja huo katika chaguzi zijazo.
Umoja huo unadai chama tawala kimeiagiza Serikali
yake kutotangaza tarehe ya uchaguzi hadi kitakapokuwa kimejipanga vizuri
kwa kinyang’anyiro hicho, kwa maana kwamba Serikali itatangaza tarehe
ya kufanyika kwa uchaguzi huo kwa njia ya kushtukiza ili vyama hivyo
vijitoe kwa kutoweza kujiandaa.
Baadhi ya wananchi nao wametoa madai kuhusu ukimya wa Serikali katika suala hilo.
Imejengwa dhana kuwa, licha ya tatizo la fedha,
Serikali iko njia panda ikifikiria uwezekano wa kupisha uchaguzi huo kwa
kuahirisha Bunge la Katiba pasipo kujenga picha kwamba hatua hiyo
imetokana na shinikizo la Ukawa.
Jambo hilo sasa linaonekana kuwa juu ya mamlaka ya
wizara inayohusika na Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi),
ambayo kisheria ndiyo inayosimamia uchaguzi huo, ingawa wananchi wengi
wametaka Tume ya Taifa ya Uchaguzi ndiyo isimamie uchaguzi huo.
Tunaishauri Serikali itangaze tarehe ya uchaguzi huo mapema
iwezekanavyo ili kuepusha vurugu zinazoweza iwapo uchaguzi huo
utatangazwa kwa kushtukiza.
Kwa kuwa Serikali imesema haina mpango wa
kusitisha Bunge la Katiba, haina budi kuusogeza mbele na kutangaza
mapema tarehe ya kufanyika kwa uchaguzi huo.
Chanzo;Mwananchi
Chanzo;Mwananchi
0 comments:
Post a Comment