Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
MWALIMU wa Shule ya Msingi Misunkumilo, Kata ya Namanyere, wilayani
Nkasi, mkoani Rukwa, Oswald Kapota (33) amehukumiwa kwenda jela miezi
sita kwa kosa la kutelekeza familia yake na kwenda kuishi kwa kimada.
Mwalimu huyo ambaye ameshindwa kubaki njia kuu na kuendeleza
michepuko, amepata hukumu hiyo jana baada ya Mahakama ya Mwanzo
Namanyere, kumtia hatiani.
Akitoa hukumu hiyo, Hakimu wa Mahakama ya Mwanzo Namanyere, Baraka
Stanley, alisema kuwa mahakama hiyo imeridhika na ushahidi uliotolewa
na upande wa mashitaka ambao unaonyesha kuwa Mwalimu huyo alifanya
kitendo hicho kwa kukusudia.
Mwalimu huyo alidaiwa kuitelekeza familia yake ya watoto wawili na
mke, kisha kuhamia nyumbani kwa mwanamke mwingine na kuifanya familia
hiyo kuishi katika mazingira magumu kwa kipindi cha zaidi ya miezi
sita, hali iliyomlazimu mkewe kufungua kesi polisi ya kudai huduma ya
malezi ya familia hiyo.
Licha ya hukumu hiyo mahakama imeamuru mwalimu huyo atakapomaliza
adhabu yake ya kifungo jela atalazimika kuitunza familia yake kama
wajibu unanavyomtaka kama mzazi.
Awali upande wa mashitaka uliieleza mahakama hiyo kuwa mwalimu huyo
alimtelekeza mke wake, Lucy Malambugi, ambaye amezaa naye watoto
wawili kiasi cha kuifanya iishi maisha magumu huku mkewe akihangaika
kuomba omba ilhali yeye akiponda raha na nyumba ndogo.
Kabla ya kutolewa kwa hukumu hiyo, mshitakiwa alitakiwa kujitetea
ambapo alikataa kutoa utetezi wake kwa madai kuwa hawezi kujitetea
mbele ya mwanamke huyo, akimtuhumu kuwa si mwaminifu kwenye ndoa na
ndiyo chanzo cha yeye kuamua kuhamia kwa nyumba ndogo.
Kutokana na kosa hilo, mahakama imemtia hatiani mtuhumiwa huyo
chini ya kifungu cha sheria namba 167, sura ya 16, ambayo imefanyiwa
marekebisho mwaka 2002.
Chanzo:Tanzania Daima
0 comments:
Post a Comment