Halmashauri ya Manispaa ya Sumbawanga imefanikiwa kupunguza kiwango cha Utapiamlo mkali kwa watoto chini ya mwaka mmoja na kufikia chini ya asilimia moja tofauti na kipindi cha miaka miwili iliyopita.
Taarifa ya Mganga Mkuu wa Manispaa ya Sumbawanga Dk. Makori Mussa katika maazimisho ya wiki ya Utepe Mweupe inayoazimishwa mkoani Rukwa imeeleza kuwa mafanikio hayo yamefikiwa kutoka na jitihada za Idara ya Afya kuendelea kutoa elimu ya Lishe bora ya watoto wachanga kwa wazazi wanaofika kwenye zahanati na vituo vya afya kupata huduma kliniki.
Dkt. Makori amesema kuwa katika kipindi cha mwaka 2012 na 2013 asilimia moja wa watoto wachanga wa Manispaa hiyo, walikuwa wakikabiliwa na Utapiamlo mkali, ambapo kufuatia elimu inayotolewa na watoa huduma za afya, kiwango hicho kimeshuka hadi kufikia aslimia 0.1
Kwa upande wake Mgeni Rasmi katika maazimisho hayo yanayofanyika katika kila halmashauri mkoani Rukwa, Mkuu wa wilaya ya Sumbawanga Bw. Mathew Sedoyeka amesema licha ya mkoa wa Rukwa kusifika kwa kuzalisha chakula kingi, lakini bado watoto wengi wanaonekana kutokuwa na afya imara kwa kukosa lishe ya uhakika.
Bw. Sedoyeka amesema hali hiyo inatokana na wananchi wengi kupendelea kula mlo wa aina moja, huku wakisahau kutumia baadhi ya vyakula, ili kukamilisha mlo bora, hivyo akiwataka wananchi kubadilika kifikra na kuanza kuwapa lishe bora akinamama wajazito kisha watoto wao wachanga badala ya kula kimazoea.
Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
0 comments:
Post a Comment