SERIKALI kupitia wakala wake wa kununua na kuhifadhi mazao ya
chakula nchini (SGR), imezitikisa halmashauri nne za Mkoa wa Rukwa
baada ya kushindwa kuzilipa zaidi ya sh bilioni 2 za mahindi
yaliyonunuliwa.
Kilio cha halmashauri hizo kimetolewa juzi na wajumbe wa Jumuiya ya
Serikali za Mitaa Tanzania (ALAT) Mkoa wa Rukwa kutokana na hatua ya
Mkuu wa Wilaya ya Nkasi, Iddy Kimanta, alipozitupia lawama halmashauri
hizo kwamba zina ulegevu katika ukusanyaji wa mapato.
Kutokana na kauli hiyo, wajumbe wa ALAT wameitaka serikali kupitia
SGR/ NFRA kuzilipa halmashauri zote fedha wanazozidai kwa kuwa huko ni
kuchelewesha utoaji wa huduma za kijamii kwa muda unaotakiwa.
Mwenyekiti wa ALAT Mkoa wa Rukwa, Godfrey Schona, alisema halmashauri
za Mkoa wa Rukwa nyingi zinategemea mapato ya ndani kupitia ushuru wa
mazao ya mahindi kiasi cha kupanga mipango mbalimbali ya maendeleo na
moja kati ya fedha hizo ni za makusanyo ya ushuru wa mahindi, hivyo
serikali inavyoshindwa kupeleka fedha hizo kwa wakati ni kuziua.
Alisema taarifa za serikali zinaonyesha Mkoa wa Rukwa ni wa mwisho
katika ukusanyaji wa mapato ya ndani na kuwa moja kati ya vitu
vinavyochangia mapato kushuka ni serikali kushindwa kuzipatia
halmashauri fedha zake za ushuru wa mahindi kwa wakati.
Mmoja wa wajumbe wa kikao hicho na ambaye pia ni Meya wa Manispaa ya
Sumbawanga, Sebastian Katepa, alisema ni mambo ya kushangaza kuona kuwa
serikali imekuwa ikisisitiza suala la makusanyo ya ndani kwa
halmashauri wakati yenyewe kupitia wakala wake wa SGR/NFRA inashindwa
kuzilipa ushuru uliowekwa kwa mujibu wa sheria ndogondogo.
Awali akifungua kikao hicho, mkuu huyo wa wilaya alisema suala la
makusanyo ya mapato ya ndani, ni muhimu na kuwa kushuka kwa mapato hayo
kutaziua halmashauri husika, jambo ambalo halipaswi kufikiwa.
Chanzo;tanzania daima
Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
0 comments:
Post a Comment