MAHAKAMA ya Mwanzo Namanyere, wilayani Nkasi, imelalamikiwa kuvunja
ndoa iliyokuwa na mgogoro bila kugawanya mali iliyochumwa na wanandoa
wakiwa pamoja.
Maria Tarafa (25), mkazi wa Kijiji cha Isale ambaye ni mmoja wa
wanandoa hao, alitoa malalamiko hayo mjini hapa alipozungumza na
mwandishi wa habari hizi, huku akiituhumu mahakama kutompa nafasi ya
kujitetea.
Alisema mumewe, Ndebile Kazuri (31) alikuwa akitaka kumtelekeza yeye
na watoto wao wanne kwa muda mrefu kwa kutaka kuivunja ndoa kinyemela,
lakini alikuwa akimshinda kila alipoitisha vikao vya wazazi na viongozi
wa vijiji na kata akitaka kuivunja ndoa hiyo bila kutoa haki kwake na
watoto.
Maria alisema mume huyo ameishi naye tangu mwaka 2003 na kufanikiwa
kupata watoto wanne ambao alikuwa akiishi nao, huku mzazi mwenzie huyo
akiishi na mwanamke mwingine eneo hilo ambaye pia amezaa naye.
“Licha ya kuishi naye, amekuwa akinipiga na kunifukuza niondoke kwake
na watoto wangu nirudi kwetu, lakini mimi nimekataa mara zote na
kumwambia nitakuwa tayari kuondoka baada ya kupata haki zangu na
watoto,” alisema.
Alisema mumewe aliamua kwenda baraza la kata na kuomba barua ili
aende mahakamani kuiomba ivunje ndoa hiyo. Kazuri alifungua kesi hiyo
namba 26/2013 Oktoba 28 mwaka jana.
Alisema mahakama ilimwita kwa mara ya kwanza na kumsomea maelezo ya
mdai (mumewe) ya kuomba ndoa yao ivunjwe, lakini yeye alipinga na
kutaka awasilishe maelezo yake, lakini iligoma kwa madai ilichohitaji
kwa mlalamikiwa ni kujibu kama yupo tayari au la.
“Niliomba nipewe nafasi ya kuzungumza upande wangu, lakini walikataa
na kuniambia wamekuja kusikiliza kesi ya talaka na si maelezo mengine,”
alisema.
Alieleza Novemba 18 mwaka jana baada ya kukiri kuwa yupo tayari
kuachana na mumewe iwapo atapata haki zake na watoto, mahakama ilivunja
ndoa hiyo na kuamuru aondoke na watoto wawili bila kueleza namna
watakavyopata huduma toka kwa baba yao.
Alisema mahakama iliamuru watoto wa miaka 7 na 9 watabaki kwa baba yao na yeye kuondoka na wawili wenye miaka chini ya saba.
Aliongeza kuwa mahakama iliamuru apewe magunia 9 ya mahindi kati ya 10 ambayo walilima pamoja na bati saba.
Akizungumzia sakata hilo, Hakimu Mkazi Mfawidhi Mahakama ya Wilaya,
Ramadhan Rugemalira, alisema mama huyo ana haki ya kufungua kesi ya
madai kuomba mgawanyo wa mali na matunzo kwa watoto endapo hakuridhika
na hukumu iliyotolewa.
Hata hivyo, Hakimu Rugemalira alisema huenda mtoa hukumu wa mwanzo
aliteleza kwa kitendo cha kutoainisha namna watoto wanaobaki kwa mama
watalelewa vipi.
Kazuri alipoulizwa juu ya mali ambazo mke wake anazilalamikia, yaani
ng’ombe 127, nyumba mbili, mbuzi 30 na ardhi hekari 70, alisema mali
hizo alipewa na baba yake wakati anaanza maisha.
Uchunguzi uliofanywa na mwandishi wa habari hizi umebaini baba yake
Kazuri (yaani Kazuri Moshi) ni marehemu, alifariki tangu Machi 2004 na
mali zake kugawiwa kwa watoto wake.
Chanzo:Tanzania Daaima
0 comments:
Post a Comment