Home » » MKUU WA MKOA RUKWA AWAONYA WANAOTETEA WANAFUNZI WENYE MIMBA KUENDELEA NA MASOMO

MKUU WA MKOA RUKWA AWAONYA WANAOTETEA WANAFUNZI WENYE MIMBA KUENDELEA NA MASOMO

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399. 


Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Kamishna Mstaafu Zelote Stephen ameonya vikali wale wanaoendeleza gumzo la kuwatetea wanafunzi wanaopata mimba wakitaka warudishwe shule huku watoto wao wakiwa wanawalinda na kuhakikisha wanafanikiwa katika maisha.

Ameyasema hayo alipofanya ziara kujionea maandalizi ya mapokezi ya wanafunzi wa kidato cha tano katika shule mbili za Wilaya ya Nkasi kwa muhula wa mwaka 2017/2018, ambapo kwa Mkoa wa Rukwa wanafunzi 1,155 wamepangiwa kujiunga na shule 13 zinazochukua wanafunzi wa kidato cha Tano. 

Mkuu wa Mkoa alisema kuwa kwa Mkoa wa Rukwa pekee kuna kesi 165 za wanafunzi kupata mimba tangu Januari hadi Juni mwaka huu na kesi zao zinaendelea kushughulikiwa ili kuwapata watuhumiwa na kuwachukulia hatua.

“Katika Mkoa wangu huu adui yangu namba moja ni yule ambae anampa mtoto wa kike mimba na yeyote anayetetea masuala yanayozunguka mimba, tusije tukaruhusu watu ambao wameshafanikiwa na watoto wao kielimu halafu wanakuwa kwenye majukwaa ya kuwaharibia watoto wa wazazi wengine, shule siyo Clinic wala siyo Maternity, wanafunzi hawaji shuleni kuapata mimba ni kusoma tu,” Mh. Zelote alisisitiza.

Sambamba na hilo aliwataka wazazi wote kukemea vitendo hivi vinavyolenga kukatisha ndoto za wanafunzi hawa ambao wanaandaliwa kuijenga Tanzania ya viwanda, na kuongeza kuwa watoto ni wa watanzania si lazima awe wa kumzaa hivyo inampasa kila mzazi kuwa na uchungu pale anapoona mtoto wa mwenziwe amekatishwa ndoto zake kwa kupata mimba.

“Kwa wazazi na watu wazima hili lazima tulisimamie wote, mzazi, mtu mzima akimwona mtoto anafanya kitu kibaya achukue hatua, akemee na sio kupiga makofi na kutetea,” Alisema.

Katika kulisisitiza hilo Mh. Zelote aligawa nakala ya Marekebisho ya Sheria Mbalimbali Namba 2 ya mwaka 2016 ambayo katika kifungu 60A (1 – 4) imebainisha adhabu kwa watu wanaowapa mimba au kuoa ama kuolewa na mwanafunzi, kwa kifungo cha miaka 30 jela.

Awali akisoma taarifa fupi ya hali ya mimba katika Shule zilizopo Wilaya ya Nkasi Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Nkasi Abel Adam Ntupwa alisema kuwa wananchi na wazazi wengi hawaifahamu sharia ya elimu inayotaka mwanafunzi akipata mimba taarifa na vielelezo vinapelekwa kwa afisa mtendaji kata au Kijiji na kesi kupelekwa polisi kisha mahakamani.

“Baadhi ya wazazi na watendaji wanakula njama ya kutaka kumaliza kesi kienyeji kwa wazazi wa pande mbili kupatana, hivyo uongozi wa wilaya utatoa elimu pana juu ya haki ya msichana kusoma mpaka kumaliza na kuwachukulia hatua wale wanaosaidia kuficha wahalifu wa mimba,” Alisema. 

Katika kuonesha umakini wa kulifuatilia suala hilo Afisa Elimu wa Mkoa wa Rukwa Robert Nestory alisisitiza kuwa upimwaji mimba kwa wanafunzi ufanywe mara kwa mara isiwe tu wakati shule zinapofunguliwa.

“Huu utaratibu wa kuwapima wanafunzi wakati shule zinapofunguliwa tuuache, upimwaji huu uwe ni wa mara kwa mara, na maafisa elimu wanapokwenda kutembelea shule mbali mmbali basi ni jukumu lao kuonana na wazazi ili wawape elimu ya sharia hii na sio tu kumuachia Mkuu wa Wilaya kazi hiyo,” Aliongeza.

Wakati akimkaribisha Mkuu wa Mkoa nae Mkuu wa Wilaya ya Nkasi Mh. Said Mtanda alibainisha mpango wa kuwatangaza kwenye redio watuhumiwa wote ili jamii isikie na kuondoa dhana ya kuwaficha katika maeneo yao wanayoishi.

“Orodha yao watuhumiwa wote tunayo na redio tunayo, Nkasi FM, tutawangaza kwa majina ili wafamu kwamba wanatafutwa ili kuwatia hofu hasa maeneo ya huku vijijini,” Mh. Mtanda alimalizia.

Jika Anda menyukai Artikel di blog ini, Silahkan klik disini untuk berlangganan gratis via email, dengan begitu Anda akan mendapat kiriman artikel setiap ada artikel yang terbit di Creating Website

0 comments:

Post a Comment

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Rukwa Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa