Imeandikwa na Lucy Lyatuu
AHADI ya Rais John Magufuli ya kutoa fedha Sh milioni 50 kwa kila
kijiji inatarajiwa kufika katika baadhi ya vijiji nchini kuanzia mwezi
ujao na tayari Sh bilioni 59 zimekwishatengwa.
Utolewaji wa fedha hizo kwa kila kijiji ni hatua mojawapo ya
utekelezaji wa ahadi ya Rais Magufuli kupitia Ilani ya Uchaguzi ya Chama
Cha Mapinduzi ya 2015/2020 ambayo aliitoa mwaka juzi wakati akiwania
nafasi hiyo katika Uchaguzi Mkuu.
Akizungumza kupitia kipindi cha Tunatekeleza kinachorushwa na
Televisheni ya TBC, Katibu Mtendaji wa Baraza na Uwezeshaji Wananchi
(NEEC), Beng’i Issa alisema baraza limefikia hatua ya mwisho kabisa ya
uratibu wa fedha hizo na kinachosubiriwa ni kibali kutoka serikalini
kuhusu fedha hizo.
“Sisi kama baraza tumemaliza kutengeneza na kuratibu na kilichobakia
ni hatua za mwisho kwa serikali kutoa kibali cha fedha hizo,
zilizotengwa zitakwenda katika baadhi ya vijiji kupitia halmashauri,
lakini vikundi vitakapopata ni vile vitakavyofikia vigezo,” alisema Issa
na kuongeza kuwa vikundi hivyo viwe na uzoefu wa kuweka akiba na
kukopeshana kwa ndani ya mwaka mmoja na kuendelea.
Kuhusu vigezo vya vikundi vitakavyopata fedha hizo ni vile ambavyo
vinatoka katika kijiji husika, lakini pia halmashauri zitahusika kwa
kuunda kamati na pia kuwepo kwa mratibu katika halmashauri husika
atakayesimamia utekelezaji wa fedha hizo pamoja na kutoa elimu.
CHANZO GAZETI LA HABARI LEO
0 comments:
Post a Comment