Kila mmoja alikuwa na hofu yake kwa wakati huo, si unajua
tena wengine walikuwa wanafunzi wa chuo, wengine ndiyo kama Suzy.
Kwa Joy hofu yake kuu ilikuwa ni kwa rafiki yake Batuli
ambaye kama akigundua amekamatwa, ndiyo atapata neno la kuzungumza kuthibitisha
kazi yake ya baa ni bora kuliko kujiuza, na Joy hakutaka hilo litokee.
Akatulia tuli, kiasi kwamba hata aliposimamishwa na kupakiwa
ndani ya basi la magereza, akakaa zake siti ya nyuma akitafakari.
Katika maisha yake hiyo ikiwa ni safari ya kwanza kupelekwa
jela, japo kuwa alishawahi kulazwa kituo cha polisi mara nyingi sana.
Mara nyingine humalizana na polisi wanaowakamata hukohuko
vijiweni mwao aidha kwa kuwapa penzi au kiasi cha pesa. Tena walifikia hatua ya
kujuana na maaskari wengi sana wa vituo vya polisi, lakini mpaka kufikia
wanakamatwa basi huenda ni oparesheni maalumu ya Kanda na siyo amri ya maOCD wa
vituo vya polisi vidogo.
Walishinda jela siku hiyo nzima na hadi siku ya pili,
wakapelekwa tena mahakamani, muda huu kesi yao ilisikilizwa mapema na wakalipa
faini na kuruhusiwa kuondoka. Kila mmoja akimlaani hakimu wa mahakama wa jana
yake kwa kushindwa kufika mahakamani.
Akiwa anafikiria uongo wa kumpelekea rafiki yake Batuli,
akashtukia anaitwa alipogeuka alishangaa kumuona Batuli, lakini kilichomfanya
kidogo azimie kwa presha, ni mtu aliyeongozana na Batuli, si mwingine bali ni
yule mteja wake aliyemzima zile laki mbili siku mbili zilizopita kule, gesti
huku akiviziua vitambulisho vyake nyumbani kwao.
Je, nini kitaendelea, Kwa nini Batuli alifika na yule kaka
pale mahakamani, usikose kufuatilia kesho.
“Shoga pole sana, nini kimekukuta? umenipa wasiwasi kweli
yaani,” alizungumza Batuli na kumkumbatia mwenzake, kama vile marafiki wakike
wafanyavyo pindi wanapomisiana kwa muda mrefu.
Joy akatumia muda huo kumnong’oneza mwenzake amueleze nini
kinachoendelea kati yake na yule kaka aliyongozana naye.
“Niliona kimya nikajua upo naye sehemu. Basi nikampigia simu
kutumia zile namba kwenye ile kadi nikashangaa kusikia na yeye mwenyewe akasema
anakutafuta kweli, ndiyo tumekuja na nilijua kama sijakukuta hapa jiji basi
niende kuulizia mochwari,” alinong’ona Batuli.
Kwa jibu hilo Joy alijikuta akiishiwa nguvu akafikiria kuwa
ni bora angemueleza ukweli mwenzake haya yasingetokea, lakini kwa kuwa
alimficha basi hayo yalikuwa ni majuto na hana budi kuyapokea.
Akamuachia Batuli na kumfuata yule kaka aliyesimama pembeni,
wakati huo akitunga uongo harakaharaka kichwani; “Mambo? Unaitwa nani vile? “
aliuliza yule jamaa huku akimtazama vizuri Joy kama vile alikuwa akiinakili
sura yake ili asiisahau.
“Naitwa Joy, najua umefuata waleti yako na kweli nilitaka
kukupigia sema ndiyo haya matatizo yamenikuta,” alijitetea.
“Usijali, nafahamu ugumu wa kazi yako, mimi sitaki chochote
zaidi ya kile kitambulisho, ile hela unaweza ukakaa nayo tu.”
“waooh kweli?” alijikuta akishangaa Joy kwa sababu wanaume
wa Kiswahili hapo ndiyo wangemuanzishia kipigo kikali na matusi huku wakitaka
kila mtu ajue kuwa anamdai, lakini tofauti na yule kaka kwani alikuwa mstaarabu
sana.
“Yah twendeni, nimekuja na gari,” alizungumza yule kaka
akiongozana nao kutoka nje ya eneo la mahakama.
Wakapanda gari ya yule kaka na Joy akawa anaelekeza njia
hadi wakafika eneo la Tandale Yemen na kupandisha mtaa wa juu hadi maeneo ya
Mafioso kisha hapo wakapaki na safari ya kuelekea mabondeni mtaa wa
Bitikilembwe ukaanza.
Hii kitu itaendelea usitoke hapa kuwa nasi kesho
0 comments:
Post a Comment