Home » » WANAFUNZI 21 WATIMULIWA KWA KUVAA 'YEBO YEBO', ZACHOMWA.

WANAFUNZI 21 WATIMULIWA KWA KUVAA 'YEBO YEBO', ZACHOMWA.

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399. 

WANAFUNZI wapatao 21 wanaosoma Shule ya Msingi Kilambo cha Mkolechi, Kata ya Kala mwambao mwa Ziwa Tanganyika wilayani Nkasi, wamefukuzwa shule kwa muda usiojulikana kwa kuvaa viatu maarufu yeboyebo.
Imeelezwa kwamba yeboyebo hizo zilikusanywa na kuchomwa kwa kile kilichoelezwa kwamba ni kunatokana na waraka uliotolewa na Ofisa Elimu Halmashauri ya Nkasi (Msingi) ukipiga marufuku wanafunzi kuvaa aina hiyo ya viatu shuleni.

Hata hivyo, akizungumza na gazeti hili jana kwa njia ya simu akiwa mjini Namanyere wilayani Nkasi mkoani Rukwa, Ofisa Elimu Halmashauri ya Wilaya ya Nkasi (Msingi), Misana Kwangula, alikanusha kutoa waraka huo kwa shule hiyo.
“Sina taarifa rasmi ila jana jioni (Jumatatu) alinipigia simu mkazi mmoja akinitaarifu kwamba kuna mwalimu wa shule ya msingi Kilambo cha Mkolechi amechoma moto viatu vya wanafunzi kwa madai kuwa ofisa elimu (msingi) ametoa waraka kwamba wanafunzi hawatakiwi kuvaa yeboyebo shuleni…

“Hakuna waraka wala marufuku yoyote iliyotolewa, isitoshe sio sahihi hata kidogo wala sio kitu kizuri kuchoma vifaa walivyonavyo wanafunzi…. Sasa kama amewachomea wanafunzi hao viatu hivyo vya yeboyebo basi awanunulie viatu vya ngozi,” alisema Kwangula.
Mkasa huo wa wanafunzi hao kufukuzwa shule na kuchomewa yeboyebo walizovaa ulitokea juzi wakati wanafunzi hao walipofika shuleni wakiwa wamevaa viatu hivyo. Inaelezwa kwamba mwalimu wa zamu, Baraka Mwakasege aliwazuia kuingia darasani, badala yake akawaamuru wavue viatu vyao.

Taarifa kutoka shuleni hapo zinaeleza kuwa, baada ya hatua hiyo, mwalimu huyo wa zamu alizikusanya yeboyebo na kuzitia kiberiti kisha akawafukuza wanafunzi hao kwa muda usiojulikana hadi wazazi na walezi watakapowanunulia viatu vya ngozi.

Mwalimu Mkuu wa shule hiyo, Posian Ally alikanusha kumtuma mwalimu wa zamu kuwafukuza wanafunzi hao shule kwa muda usiojulikana wala kuteketeza kwa moto yeboyebo zao. Alisema ataitisha kikao ili kujadili suala hilo na kwamba mwalimu huyo akibainika kutenda kosa hilo ataamriwa kuwanunulia watoto hao viatu vingine.

Akizungumza na gazeti hili kwa njia ya simu, mmoja wa wazazi wa wanafunzi hao, Privatus Yoram, alithibitisha kutokea kwa mkasa huo. “Jana jioni nilimwona mwanangu anayesoma darasa la tano shuleni hapo akirudi nyumbani akiwa peku.
Nikamuuliza kulikoni, akanieleza kuwa mwalimu wa zamu (Mwakasege) amewafukuza shule na kuchoma yeboyebo zao kutokana na waraka wa Ofisa Elimu Nkasi unaopiga marufuku yeboyebo shuleni,” alisema Yoram.
CHANZO: GAZETI LA HABARI LEO.
Jika Anda menyukai Artikel di blog ini, Silahkan klik disini untuk berlangganan gratis via email, dengan begitu Anda akan mendapat kiriman artikel setiap ada artikel yang terbit di Creating Website

0 comments:

Post a Comment

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Rukwa Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa