Home » » UMUHIMU WA MAFUNZO YA UFUNDI TANZANIA-3

UMUHIMU WA MAFUNZO YA UFUNDI TANZANIA-3

Umuhimu wa elimu na mafunzo ya ufundi unaonekana kutokana na ukweli kwamba rasilimali watu ni suala la muhimu katika mchakato wa maendeleo.
Bila ya rasilimali watu, vigezo vingine kama mtaji, ardhi na rasilimali nyingine haviwezi kuwa na manufaa yoyote.
Hata hivyo, rasilimali watu itakuwa na tija kama tu itapewa nyenzo na ujuzi ili kuboresha utendaji na ufanisi. Hiki ndicho hasa elimu na mafunzo ya ufundi inalenga kukifanya.
Tangu baada ya mapinduzi ya viwanda katika nchi za Ulaya Magharibi katika karne ya 18 na 19, maendeleo na mafanikio ya elimu ya ufundi, vimenasibishwa kwa karibu na maendeleo ya kiuchumi. Na maendeleo yoyote ya kiuchumi ya nchi husika hutokana na ubora wa rasilimali watu wa nchi husika.
Ubora huu wa rasilimali watu hutokana na ubora wa mfumo wa elimu wa nchi husika. Elimu na mafunzo ya ufundi inachukuliwa kama ni mojawapo ya vigezo muhimu katika kukuza uzalishaji na uchumi kwa jumla.
Katika kufanikisha hili, shule na vyuo vina jukumu la kuandaa na kuzalisha nguvukazi yenye ujuzi wa kutosha ili kuongeza ufanisi kazini.
Kama anavyosema mwandishi aitwaye Giroux, elimu na mafunzo ya ufundi nyakati zingine huwa ni zana ya kutatua matatizo ya kiuchumi, kisiasa na kijamii ambayo yanatishia uimara wa kiuchumi na kisiasa wa baadhi ya mataifa.
Kuongezeka kwa idadi ya watu wasio na ajira na mabadiliko ya namna ya utendaji kazi, yameliweka suala la elimu ya nguvukazi kuwa lenye kipaumbele cha juu katika uboreshaji wa mifumo ya elimu.
Katika utafiti nilioufanya mwaka 2009 wilayani Temeke, nilibaini kuwa wahojiwa wengi walikiri kuwa elimu na mafunzo ya ufundi vilikuwa na mchango mkubwa katika maendeleo ya Taifa letu; na vyuo vya ufundi viliandaa wahitimu wa kutosha kutokana na mahitaji ya nchi kwa wakati huo.
Aidha, walikiri kuwa elimu na mafunzo ya ufundi ilikuwa bora zaidi ukilinganisha na elimu ya taaluma katika kukuza ujuzi, teknolojia na ujasiriamali.
Pia, kwenye uwezo wa kujiajiri watahiniwa wa vyuo vya ufundi walionekana kuwa na uwezo zaidi ukilinganisha na watahiniwa katika elimu ya kawaida.
Utafiti ulibaini kuwa vyuo vya ufundi vya umma vinaweza kupata mafanikio zaidi pamoja na ufanisi wa hali ya juu kama vitaendeshwa kibiashara.
Vikiendeshwa kwa sura hiyo vitapata faida kubwa zaidi na hivyo kufidia pengo linalotokana na upungufu wa ruzuku kutoka serikalini.
Zaidi ya hayo, wahojiwa wengi walikubaliana kwamba mtalaa uliopo wa elimu na mafunzo ya ufundi ulikidhi mahitaji ya soko la ajira kwa wakati huo.
Pia, utafiti uliofanywa na Castro na Verdisco mwaka 1998 katika nchi za Argentina na Chile, ulibaini elimu na mafunzo ya ufundi vilikuwa na mchango mkubwa katika kukuza fursa za ajira na kuleta maendeleo ya nchi husika.
Utafiti ulibaini kuwa asilimia 60 ya wahitimu kutoka katika vyuo vya ufundi katika nchi hizo walipata ajira ukilinganisha na wahitimu wa elimu ya kawaida.
Hapa nchini elimu na mafunzo ya ufundi vikitumika vizuri vinaweza kuleta mabadiliko makubwa katika sekta ya kilimo na viwanda. T
Teknolojia rahisi zikifundishwa na kuenezwa katika maeneo ya vijijini zitaweza kukuza uzalishaji vijijini.
Teknolojia hizi ni kama zile za uendeshaji na ukarabati wa mitambo inayotumika katika sekta ya kilimo. Pia, elimu na mafunzo ya ufundi vinaweza kusaidia kuanzishwa kwa viwanda vidogovidogo mijini na vijijini
 Chanzo:Mwananchi
Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
Jika Anda menyukai Artikel di blog ini, Silahkan klik disini untuk berlangganan gratis via email, dengan begitu Anda akan mendapat kiriman artikel setiap ada artikel yang terbit di Creating Website

0 comments:

Post a Comment

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Rukwa Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa