Home » » WAKULIMA WAILALAMIKIA HIFADHI YA LWAFI

WAKULIMA WAILALAMIKIA HIFADHI YA LWAFI

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.

BAADHI ya wakulima wa Kitongoji cha Chaulima Kijiji cha Mkole Kata ya Mtenga wilayani Nkasi Mkoa wa Rukwawameulalamikia uongozi wa hifadhi ya pori la Lwafi na Msitu wa Mfili kwa kuendesha zoezi la kuwahamisha kwa nguvu.
Wananchi hao walidai kuwa askari wa wanyamapori wa hifadhi ya Lwafi, waliendesha msako hivi karibuni na kuchoma nyumba zao za kuishi na kuharibu mimea iliyokuwa mashambani ili kuwashinikiza kuhama kutoka ndani ya hifadhi hiyo ambayo wamedai wamekuwa wanafanya shughuli zao za kibinadamu kwa zaidi ya miaka 10 iliyopita.
Mmoja wa wakulima hao, Denya Nyabahamba, alisema doria hiyo ambayo ilifanyika bila ya taarifa yoyote, iliwatia hasara kubwa baada ya kuchomwa kwa nyumba zao na pia kuharibiwa kwa mazao yaliyokuwa yameoteshwa kwenye mbuga za hifadhi ya Lwafi na kusababisha kupotea kwa fedha na vitu vingine vya thamani vilivyoteketea ndani ya nyumba hizo.
Alisema kimsingi wao hawapingi sheria iliyopo inayodhibiti shughuli za kibinadamu ndani ya hifadhi hizo, ila kinachoshangaza ni kwamba yeye na wakulima wenzake wengi tu wamekuwa wanaendesha shughuli zao muda mrefu bila kuzuiwa na mamlaka yoyote, badala yake hivi sasa doria zinafanywa bila taarifa wala ushirikishwaji wa aina yoyote.
Katibu Tawala Wilaya ya Nkasi, Festo Conya,  akijibu tuhuma hizo kwa niaba ya Mkuu wa Wilaya hiyo, alipinga kuwapo kwa doria zinazofanywa bila kuwashirikisha wananchi kwa maana ya kuwaelimisha kupitia viongozi wa serikali zao za kata na vijiji, kwa kutoa tangazo la kuzuia na kukataza shughuli za kibinadamu kuendeshwa ndani ya hifadhi na kudai kuwa, lawama hizo zina lengo la kuficha maovu yao ya kukiuka sheria halali za serikali.
Alisema katika doria ya hivi karibuni iliyoendeshwa baada ya matangazo na maagizo ya muda mrefu ya kuzuia shughuli za kilimo kwenye vyanzo vya maji vya misitu ya Mfili vinavyotoa huduma kwa wakazi wa mji wa Namanyere makao makuu ya wilaya ya Nkasi, watu 21 walikamatwa kwa tuhuma za kulima bustani kwenye vyanzo vya maji ya misitu hiyo, ambako saba kati yao wamehukumiwa kutumikia jela mwaka mmoja kila mmoja na wengine kesi zao zinaendelea.
Meneja wa hifadhi ya Lwafi, Ramadhani Isomanga, aliungumzia hali halisi ya utekelezaji wa amri halali ya serikali juu ya kuzuia shughuli za binadamu ndani ya hifadhi ya Lwafi, alisema wakulima na wafugaji hao wanazielewa sheria za udhibiti wa hifadhi hizo na kwa hali hiyo hujenga majengo ya muda kwa maana ya vibanda vya nyasi ili wasipate hasara ikiwa vitabomolewa wakati wa doria za kisheria
Chanzo Tanzania Daima
Jika Anda menyukai Artikel di blog ini, Silahkan klik disini untuk berlangganan gratis via email, dengan begitu Anda akan mendapat kiriman artikel setiap ada artikel yang terbit di Creating Website

0 comments:

Post a Comment

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Rukwa Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa