Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
Baraza la Taifa la Biashara (TNBC) limeyashauri mabaraza ya
biashara ya mikoa ya nyanda za juu kusini kuanzisha vituo vitakavyotoa
huduma za pamoja ili kukuza uwekezaji katika maeneo yao.
Ushauri huo ni moja ya mapendekezo yaliyotolewa
katika kongamano la uwekezaji lililomalizika mjini Mbeya hivi karibuni,
ambapo mikoa na halmashauri zake zilitakiwa kuanzisha vituo vya
kuwawezesha wawekezaji kupata vibali, leseni na huduma zote
zinazohitajika katika eneo moja.
Katibu Mtendaji wa TNBC, Raymond Mbilinyi alitoa
ushauri huo alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari mjini hapa
wakati wa kongamano hilo.
Alizitaka mamlaka za Serikali za Mitaa zijenge mazingira wezeshaji na zisiwe vikwazo kwa uwekezaji ili kuharakisha maendeleo.
“Kila kanda au mkoa uainishe sifa za kipekee za
uwekezaji kulingana na hali halisi kiuchumi, kijamii na kijiografia kwa
ustawi wa wananchi wake na kuondoa umaskini,” alisema.
Aliitaka mikoa hiyo kuhamasisha uwekezaji wa
viwanda vya kusindika mazao ya kilimo na mifugo ili kuongeza thamani na
kuleta tija katika uzalishaji.
“Mikoa hii ihamasishe matumizi sahihi ya pembejeo
na zana za kilimo kwa lengo la kuongeza uzalishaji wa mazao hayo ya
kilimo,” alisema.
Katika kongamano hilo, Serikali iliwataka
wawekezaji wa ndani kuangalia ni namna gani wanaweza kunufaika na
shughuli za Kituo cha Uwekezaji nchini (TIC) na kuondokana na dhana
potofu kuwa kituo hicho ni cha wawekezaji wa nje pekee.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Uwekezaji na
Uwezeshaji, Dk Mary Nagu alisema kuna wawekezaji wengi wa ndani ambao
wamefanya uwekezaji mkubwa katika mikoa ya kusini wanaostahili kupata
hadhi ya uwekezaji mahiri, lakini hawajapata nafasi hiyo.
“Kwa kutokujua ni kwa jinsi gani Kituo cha
Uwekezaji kinatoa vivutio kwa wawekezaji wenye hadhi, hawakupata kutumia
fursa hiyo kama ilivyotarajiwa,” alisema waziri huyo.
Takwimu zilizopo zinaonyesha kuwa katika kipindi
cha mwaka 1997 hadi Machi 2014, miradi 220 iliandikishwa katika mikoa ya
kanda hiyo, ikiwa na thamani ya Dola za Marekani 4 bilioni na
inatazamiwa kuleta ajira 36,191.
Chanzo:Mwananchi
Chanzo:Mwananchi
0 comments:
Post a Comment