Home » » KIGUGUMIZI CHA NINI UCHAGUZI SERIKALI ZA MITAA?

KIGUGUMIZI CHA NINI UCHAGUZI SERIKALI ZA MITAA?

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399. 
 
Tunashangazwa na Serikali kuendelea kushikwa na kigugumizi linapokuja suala la kutaja tarehe ya kufanyika kwa Uchaguzi wa Serikali za Mitaa. Kwa kawaida uchaguzi huo hufanyika Septemba kila mwaka wa uchaguzi, kwa maana ya mara moja kila baada ya miaka mitano. 
Uchaguzi wa Serikali za Mitaa ni muhimu pengine kuliko uchaguzi mkuu katika nchi yoyote, kwani ndiyo hasa hutoa sura na taswira ya mamlaka ya wananchi walio wengi kuanzia ngazi za chini ambako ndiko viongozi wa kitaifa hupata uhalali wa kuongoza nchi husika.
Kwa maana hiyo, uchaguzi huo ni muhimu katika kudumisha demokrasia na utawala bora.
Ndiyo maana serikali nyingi duniani huelekeza nguvu nyingi katika kuhakikisha kwamba uchaguzi wa serikali za mitaa siyo tu unafanikiwa, bali pia unakuwa huru na haki.
Licha ya kuhitaji fedha na rasilimali nyingi katika maandalizi yake, uchaguzi huo uhitaji muda wa kutosha kuhamasisha wananchi wajitokeze kupiga kura siku ya uchaguzi ili kuunda serikali ambayo itashughulikia matatizo ya wananchi katika ngazi hiyo.
Hivyo, malalamiko yaliyotolewa juzi na viongozi wa vyama vya upinzani nchini kuhusu ukimya wa muda mrefu wa Serikali katika suala hilo ni za msingi kabisa. Kwamba vyama vya Chadema, CUF na NCCR-Mageuzi vimekwazwa na ukimya wa Serikali kuhusu lini hasa uchaguzi huo utafanyika, ni malalamiko ambayo hayapaswi kupuuzwa hata kidogo.
Kinachofanyika sasa ni kama mchezo wa kuigiza, kutokana na wahusika wa uandaaji wa uchaguzi huo wanatupiana mpira na hakuna aliye tayari kuzungumzia suala hilo. Hali hiyo inaonyesha kwamba Serikali iko njia panda pengine kutokana na hali ngumu ya kifedha inayoikabili, ingawa imeshindwa kutambua madhara ya kisiasa yanayoweza kutokea kutokana na ukimya wake huo wa muda mrefu katika suala hilo zito.
Tayari mazingira yanayoashiria shari za kisiasa yameanza kujengeka. Vyama vya upinzani vimejenga dhana kwamba chama tawala kimeng’amua kitashindwa katika uchaguzi huo, kutokana na vyama hivyo vya upinzani kuunda Umoja wa Katiba ya Watanzania (Ukawa) na kuamua kushirikiana chini ya umoja huo katika chaguzi zijazo.
Umoja huo unadai chama tawala kimeiagiza Serikali yake kutotangaza tarehe ya uchaguzi hadi kitakapokuwa kimejipanga vizuri kwa kinyang’anyiro hicho, kwa maana kwamba Serikali itatangaza tarehe ya kufanyika kwa uchaguzi huo kwa njia ya kushtukiza ili vyama hivyo vijitoe kwa kutoweza kujiandaa.
Baadhi ya wananchi nao wametoa madai kuhusu ukimya wa Serikali katika suala hilo.
Imejengwa dhana kuwa, licha ya tatizo la fedha, Serikali iko njia panda ikifikiria uwezekano wa kupisha uchaguzi huo kwa kuahirisha Bunge la Katiba pasipo kujenga picha kwamba hatua hiyo imetokana na shinikizo la Ukawa.
Jambo hilo sasa linaonekana kuwa juu ya mamlaka ya wizara inayohusika na Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), ambayo kisheria ndiyo inayosimamia uchaguzi huo, ingawa wananchi wengi wametaka Tume ya Taifa ya Uchaguzi ndiyo isimamie uchaguzi huo.
Tunaishauri Serikali itangaze tarehe ya uchaguzi huo mapema iwezekanavyo ili kuepusha vurugu zinazoweza iwapo uchaguzi huo utatangazwa kwa kushtukiza.
Kwa kuwa Serikali imesema haina mpango wa kusitisha Bunge la Katiba, haina budi kuusogeza mbele na kutangaza mapema tarehe ya kufanyika kwa uchaguzi huo.
 Chanzo;Mwananchi
Jika Anda menyukai Artikel di blog ini, Silahkan klik disini untuk berlangganan gratis via email, dengan begitu Anda akan mendapat kiriman artikel setiap ada artikel yang terbit di Creating Website

0 comments:

Post a Comment

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Rukwa Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa