Home » » ARFI ‘ABEBA’ AJENDA ZA UKAWA

ARFI ‘ABEBA’ AJENDA ZA UKAWA

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399. 
  

Wajumbe wa Kamati Namba 10 ya Bunge Maalumu, juzi walijikuta katika wakati mgumu baada ya kubanwa kwa karibu saa nzima na Mbunge wa Mpanda Mjini (Chadema), Saidi Arfi.
Habari kutoka ndani ya kamati hiyo zinasema tofauti na fikra za wajumbe wengi kwamba mjumbe huyo angewaunga mkono kwa kila jambo, hali imekuwa tofauti kwani amekuwa na misimamo kama iliyoonyeshwa na wajumbe wa Ukawa ambao wamesusia Bunge hilo.
“Yule bwana pamoja na mjumbe mmoja hivi kutoka kundi la 201 upande wa Zanzibar wametuhenyesha sana maana misimamo yao ni ileile ya Ukawa, yaani wameamua kuandika maoni ya wachache, jambo ambalo awali hatukulitarajia,” alisema mmoja wa wajumbe.
Gazeti hili limebaini kuwa mbunge huyo kutoka Zanzibar ni Adil Mohamed Ali ambaye pamoja na Arfi wameamua kuandika maoni ya wachache kuhusu eneo la madaraka ya Rais lililokuwa likibishaniwa.
Kanuni ya 32 (10) inatoa fursa kwa wajumbe wasiokubaliana na uamuzi kwenye kamati kuandika maoni ya wachache na maoni hayo yamepewa dakika 60 (saa moja) kusomwa bungeni kwa mujibu wa Kanuni ya 33 (5).
Juzi, Makamu Mwenyekiti wa Kamati hiyo namba 10, Salim Awadhi Salim akizungumza na waandishi wa habari alisema walilazimika kuweka kando ibara za 72 na 73 ambazo zinazungumzia mamlaka ya Rais wa Jamhuri ya Muungano baada ya kutokea mvutano makali.
“Sura namba saba ibara ya 72 na 73 ambayo inahusiana na uongozi tuliahirisha ili wajumbe waweze kutafakari,” alisema Salim huku akifafanua kwamba wajumbe wengi walisema kuwa majukumu aliyopewa Rais katika Katiba ya sasa ni mengi, hivyo apunguziwe.
Habari kutoka ndani ya kamati hiyo zimesema mbali na madaraka ya Rais, suala jingine lililozua mvutano likimhusisha Arfi na Ali ni pendekezo la wajumbe wa kamati hiyo kutaka uwapo wa makamu watatu wa rais.
“Kulikuwa na pendekezo kwamba tuwe na makamu wa rais watatu ambao ni yule anayetokana na mgombea mwenza, Rais za Zanzibar ambaye anakuwa makamu wa pili na makamu watatu anakuwa Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,” kilisema chanzo chetu.
Habari zinasema kutokana na hali hiyo, Arfi na Ali waliibua hoja kwamba ikiwa kuna pendekezo la makamu watatu wa rais, kwa nini pendekezo la serikali tatu linakataliwa na hapo ndipo mvutano ulipoanzia na kusababisha mjadala mkali uliochukua takriban saa nzima.
Alipoulizwa jana, Arfi hakuwa tayari kuzungumzia suala hilo kwa maelezo kwamba kama kuna chochote kitakachotakiwa kufahamika basi kitawasilishwa bungeni baada ya kamati kumaliza kazi yake.
“Mimi sidhani kama ni busara kuzungumza kwa sasa, kuweni na subira maana mahali sahihi pa kusemea mambo haya ni kule bungeni,” alisema Arfi ambaye ameingia katika mgogoro mkubwa na chama chake kutokana na kukiuka makubaliano ya kususia vikao hivyo.

Kwa upande wake, Ali hakuthibitisha wala kukanusha kuwapo kwa mpango wa kuwasilisha maoni ya wachache, lakini akasema asingeweza kuzungumza kwani alikuwa na kazi nyingi ndani ya kamati.
Habari kutoka ndani ya kamati hiyo pia zilisema kuwa wajumbe hao wawili wamekuwa wakivutana na wenzao pale kunapotolewa mapendekezo ya kufutwa kwa maneno ‘shirikisho’ au ‘Tanganyika’.
“Hoja yao ni kwamba kwa nini tufute maneno hayo wakati Bunge Maalumu halijaamua kuhusu muundo wa muungano?
Tumekuwa kwenye wakati mgumu kweli na katika baadhi ya ibara tumeacha hivyo,” kilifafanua chanzo chetu.
Chanzo;Mwananchi
Jika Anda menyukai Artikel di blog ini, Silahkan klik disini untuk berlangganan gratis via email, dengan begitu Anda akan mendapat kiriman artikel setiap ada artikel yang terbit di Creating Website

0 comments:

Post a Comment

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Rukwa Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa