Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
HALMASHAURI ya Wilaya ya Sumbawanga mkoani Rukwa, imetoa siku 14
kwa watendaji wa vijiji kuhakikisha shule zilizopo katika vijiji vyao
zinatoa chakula cha mchana kwa wanafunzi, na atakayeshindwa awekwe
ndani kwa siku saba.
Agizo hilo lilitolewa juzi na Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa
halmashauri hiyo, Chrispin Luanda katika mkutano wa hadhara wakati
akizungumza na wakazi wa Kijiji cha Kaengesa wilayani hapa wakati wa
ukaguzi wa utekelezaji wa sera ya Matokeo Makubwa Sasa (BRN).
Alibainisha kuwa halmashauri imelazimika kutoa agizo hilo kufuatia
taarifa kuwa baadhi ya watendaji wa vijiji wamekuwa ni kikwazo kikubwa,
ambapo wamekuwa wakikwamisha utekelezaji miradi ya maendeleo katika
maeneo yao.
Aliongeza kuwa kutokana na baadhi ya watendaji wa vijiji kukaidi
utekelezaji wa miradi ya maendeleo, sasa ni wakati muafaka kuanza
kuwawajibisha wanaolegalega.
“Natoa siku kumi na nne kwa watendaji wa vijiji wote wahakikishe kuwa
kuanzia sasa wanafunzi wa shule zote za msingi wilayani humu
wanapata chakula cha mchana shuleni, yeyote atakayeshindwa akamatwe na
kuwekwa ndani kwa siku saba ili iwe fundisho si kwake tu bali pia kwa
wengine wanaoendekeza tabia hiyo,” aliagiza.
Luanda alieleza kuwa changamoto kadhaa zinazozikabili shule za
msingi wilayani humo zinaweza kutatuliwa, lakini tatizo kubwa ni
baadhi ya viongozi wa serikali kutowajibika kutekeleza majukumu yao
ipasavyo.
Naye Ofisa Elimu Shule za Sekondari wilayani hapa, Emiliana Fungo,
alisema wazazi wanao wajibu wa kutatua changamoto za shule wanazosoma
watoto wao ili matokeo bora yapatikane.
Chanzo:Tanzani Daima
0 comments:
Post a Comment